Tangazo

November 8, 2012

TASWA yafikisha MOAT suala la kuzuiwa Televisheni na Redio kukutangaza moja kwa moja Ligi Kuu Tanzania Bara

Mwenyekiti wa MOAT, Reginald Mengi
CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kimeamua kulipeleka kwa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT), suala la kuzuia televisheni na redio kutangaza moja kwa moja michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na wapiga picha za televisheni kuchukua picha kwa ajili ya kutumia kwenye habari.

Hatua hiyo ya TASWA ina lengo la kuomba mwongozo kwa chama hicho ambacho ndio kinachomiliki vyombo vya habari kuhusiana na suala hili ambalo limekuwa likilalamikiwa kwa kiasi kikubwa na wanachama wetu.

Tayari TASWA imefanya mazungumzo ya awali na MOAT, ambayo imeridhia iandikiwe barua rasmi ili jambo hilo lijadiliwe kwenye vikao vyake na baada ya hapo TASWA itapewa mwongozo ambao itautoa kwa waandishi wa habari za michezo.

Kwa kuwa Mwenyekiti wa TASWA, Juma Pinto pia ni mjumbe wa MOAT, basi suala hilo tunaamini litafanyiwa kazi haraka iwezekanavyo, hivyo tunawaomba waandishi wa habari za michezo waendelee kuwa watulivu na wavumilivu kipindi hiki na wafanye majukumu yao kama kawaida.

Siku zote chama chetu kimekuwa na uhusiano mzuri na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na wadau wengine wote na TASWA haitaki ifike mahali iwe na mgogoro na chama chochote cha michezo, lakini pia haitakuwa tayari kuona wanachama wake wakishindwa kutekeleza majukumu yao.

Kama mnavyojua wiki iliyopita kulifanyika kikao cha Kamati ya Ligi na baadhi ya klabu zinazoshiriki ligi hiyo kuhusiana na tukio la kuzuia televisheni na redio kutangaza moja kwa moja michezo ya Ligi Kuu pamoja na wapiga picha za televisheni kuchukua picha kwa ajili ya kutumia kwenye habari.

Katika kikao hicho ambacho Mwenyekiti wa TASWA, Juma Pinto  alihudhuria kulitoka maelezo mbalimbali ambayo baadhi ya wanahabari hawakubaliani nayo na wamekuwa wakitaka TASWA ichukue hatua uamuzi mgumu.

Sekreterieti ya TASWA imeona si vizuri kukurupuka kuchukua uamuzi wowote ule kwa sasa kwani yenyewe haina chombo cha habari, lakini wanaofanya kazi kwenye vyombo vya habari ndiyo wanachama wake. Itawasilisha MOAT maazimio ya kikao cha Kamati ya Ligi kuhusiana na jambo hili, tuna hakika tutalimaliza.

B.MKUTANO MKUU

Jumatano Novemba 16, 2012 Kamati ya Utendaji ya TASWA itakutana Dar es Salaam kupitia ajenda za Mkutano Mkuu wa chama chetu, kisha Jumatatu Novemba 18 Mwenyekiti wa TASWA atafanya mkutano na wanahabari kutangaza mdhamini wa mkutano huo pamoja na tarehe rasmi na mahali utakapofanyika.

Kutokana na kuandaliwa kwa ajenda mpya ya kuboresha chama na maslahi ya wanachama wake, TASWA inaendelea kutafuta wadhamini zaidi ili kuufanya mkutano huo uwe wa siku mbili.

Imetolewa na:
Amir Mhando
Katibu Mkuu TASWA
08/11/2012

No comments: