Tangazo

December 11, 2012

Suala la TSM9 Wanafunzi, Walimu Watupiana Lawama

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Bungu, Dismas Kimweli

Na Mwandishi wa Thehabari.com, Korogwe

SUALA la kuwepo na utata kwa baadhi ya wanafunzi kukwamishwa na fomu namba 9 ya Takwimu za Shule za Msingi kwa mwanafunzi (TSM9) kufanya mitihani yao katika shule anuai za sekondari limezua mvutano kati ya wazazi wa wanafunzi na walimu huku kila upande ukitupa lawama kwa mwenzake.

Baadhi ya wanafunzi na wazazi waliohojiwa wamedai uzembe upo kwa walimu ambao hutumia majina ya wanafunzi wengine kuingiza wanafunzi kinyemela, jambo ambalo huzua utata baadaye kwa mwanafunzi aliyeingia kwa njia hiyo anapokaribia kufanya mitihani yake.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi wilayani Korogwe katika shule kadhaa za sekondari na msingi umebaini kuwa wapo wanafunzi ambao wamezuiwa kufanya mtihani wa mwisho wa kidato cha nne na ule wa kidato cha pili wa mchujo kutokana na hali kama hiyo ya utata katika suala hilo la TSM9.

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Bungu, Dismas Kimweli ambaye shule yake ilikuwa miongoni mwa shule zilizolalamikiwa, akizungumza na mwandishi wa habari hizi alipinga kuwepo na wanafunzi waliozuiliwa kufanya mitihani yao kutokana na utata wa fomu namba 9.

Mwalimu huyo alisema idadi kubwa la wanafunzi ambao hukumbwa na matatizo kama hayo ni wanafunzi ambao huingia shuleni kwa njia ya uhamisho huku wazazi wao wakiomba mwanafunzi aendelee kusoma wakati utaratibu wa kufuatilia uhamisho ukiendelea.

“Unakuta mzazi anamleta mtoto kujiunga na shule yako akitokea shule nyingine na anaomba aendelee kusoma wakati akiendelea kufuatilia uhamisho...lakini baadaye anakaa kimya sasa mtoto anakuwa anaendelea na shule bila kuwa na uhamisho ambao hujumuisha TSM9, ikifika kipindi cha mitihani hapo linakuwa tatizo na mzazi anajifanya kasahau,” alisema.

“Sasa kama mtu hajatimiza vitu kama hizi anarushaje lawama kwa walimu au shule...lakini ikifikia hatua hii wapo ambao huwaeleza nao kuelewa na wapo ambao huwa na mvutano kidogo,” aliongeza mwalimu huyo.

Akitoa ufafanuzi wa suala hilo, Kaimu Ofisa Elimu Sekondari Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, Shaban Shemzighwa alikiri kuwepo kwa malalamiko ya baadhi ya wanafunzi kutokuwa na TSM9 hasa wa kidato cha pili lakini alidai waliruhusiwa kufanya mitihani yao na wao kuwaagiza wakuu wa shule wanazotoka kuhakikisha wanawasilisha namba zao kwenye vituo inakosahishiwa mitihani.

“Taarifa za malalamiko zilitufikia na baadhi ya Shule za Sekondari ambazo wanafunzi walikuwa na matatizo hayo ni Bungu, Patema, Mfundia na nyinginezo, hapa nipo nje ya kituo cha kazi hivyo ni vigumu kutaja idadi na shule zote,” alisema Shemzighwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu.

Aidha akifafanua zaidi alisema wanafunzi wengi waliokuwa na matatizo kama hayo wa kidato cha pili ni wale waliohama kutoka shule moja kwenda nyingine, ambao hawakuja na TSM9 zao. “…Hata hivyo waliruhusiwa kufanya mitihani na maelekezo tuliwapa wakuu wa shule kuhakikisha wanapeleka namba za wanafunzi hao katika kituo cha kusaishia mitihani ili waweze kutambuliwa kihalali vinginevyo hawawezi kutambulika,” alisema ofisa huyo.

Alisema inaonekana kuna baadhi ya walimu wakuu walipokea wanafunzi bila TSM9, hata hivyo haikujulikana kama ni kwa njia ya kinyemela au matatizo ya uhamisho kwa wanafunzi hao kutoka shule moja hadi nyingine. Hata hivyo licha ya kiongozi huyu kuitaja Bungu kuwa miongoni mwa shule zilizotolewa tarifa kuwa na tatizo la fomu namba 9, mkuu wa shule hiyo alipinga shule yake kuwemo.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com kwa kushirikiana na HakiElimu

No comments: