Tangazo

June 3, 2013

Mama Ban Soon – taek: Kuna uwezekano wa kuwa na kizazi kisicho na Ukimwi Barani Afrika

Na Anna Nkinda – Yokohama

 Imeelezwa kwamba inawezekana kuwa na kizazi kipya barani Afrika kisichokuwa na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi kama jamii nzima itaamua kupambana na ugonjwa huo unaosababisha vifo vya watu wengi hasa kina mama wajawazito na watoto.

Hayo yamesemwa  leo na Mke wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) mama  Ban Soon –taek (pichani), wakati akifungua kongamano la kimataifa la siku mbili la Tuongee kuhusu Ukimwi : Afrika na Japani tushirikiane kutatua changamoto  unaofanyika mjini Yokohama.

Mama Ban Soon alisema kuwa ni  wajibu wa wake wa marais wa Afrika kuhakikisha kuwa  hakuna maambukizi mapya yaUkimwi, unyanyapaa na vifo vya watoto chini ya umri wa miaka mitano katika nchi zao.

Jambo ambalo siyo rahisi kwa nchi maskini kwani  kila siku watoto mia tisa wanapata maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) ,  kama hali hii itaendelea watoto zaidi ya milioni watakuwa wamepata maambukizi ifikapo mwaka 2015.

Alisema kuwa nia ni kuwafikia wanawake wajawazito wote  wanaohitaji kuangaliwa na kupewa matibabu hii inawezekana kama watashirikiana kwa pamoja na hivvyo kuzaliwa watoto wasio na maambukizi  na baada ya miaka michache hakutakuwa na ugonjwa wa Ukimwi barani Afrika.

“Kama itatokea mama mjamzito anaugonjwa wa Ukimwi basi ajifungue  salama bila ya kumuambukiza mtoto wake,  pia  amtunze mtoto huyo kwani ni wajibu wetu kuwalinda mama na mtoto wa bara la Afrika”, alisema Mama Ban Soon.

Akiwakaribisha wake hao wa marais katika mkutano huo mke wa waziri mkuu wa Japani Mama  Akie Abe alisema kuwa wanawake na watoto  wote Duniani wanapambana na matatizo yanayofanana ingawa ukubwa wa matatizo unatofautiana hivyo basi wao kama viongozi wanatakiwa kuungana kwa pamoja na kuwasaidia wanawake hao.

Mama Abe alisema, “Hapa nchini Japani idadi ya watu wanaoishi na VVU inazidi kuongezeka na Serikali inawapatia huduma mbalimbali,  lakini wanawake wengi Duniani wanaogopa kuongea kuhusu ugonjwa wa Ukimwi, wakati umefika sasa wasiogope waongee ili waweze kupata haki zao za msingi”

Kwa upande wake Rais wa Umoja wa wake wa Marais wa  Afrika wa kupambana na Ugonjwa wa Ukimwi (OAFLA) Mama Penehupifo Pohamba aliishukuru Serikali ya Japan kwa kuandaa mkutano huo na kutoa zaidi ya dola bilioni moja za Kimarekani barani Afrika kwa ajili ya kupambana na magonjwa ya Ukimwi, Maralia na kifua kikuu.

Alisema kuwa ni jambo la muhimu kuweka ushirikiano wa  pamoja baina ya Afrika na Japani  na kuwaomba wasaidiwe  rasilimali fedha ambazo zitawasaidia kutatua matatizo mbalimbali yanayowakabili wanawake na watoto. 

“Wanawake wengi na watoto wanakufa na ugonjwa huu hii ni kutokana na baadhi ya mila zinazowakandamiza katika jamii zao pia baadhi ya nchi zetu zinakabiliwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe jambo la muhimu ni kuungana kwa pamoja ili tuweze kuwasaidia na kutimiza malengo yetu”, alisema mama Pohamba.  

Baadhi ya wasomi  na wataalamu mbalimbali waliowasilisha mada katika  mkutano huo waliwaomba wake hao wa Marais kupaza sauti zao kwa pamoja na kuwasaidia watu wanaoishi na VVU hasa kina mama na watoto ambao hawana mahali pa kusemea matatizo yao.

Walisema kuwa tatizo  la unyanyapaa ni kubwa sana Barani Afrika hivyo basi wanatakiwa kuielimisha jamii inayowazunguka ili iweze kutambuwa kuwa ugonjwa Wa UKimwi ni sawa na magonjwa mengine na kutowatenga watu wenye VVU.

"Wasomi peke yao hawawezi kukabiliana na tatizo la Ukimwi bali jamii nzima inatakiwa kuungana kwa pamoja  kutatua changamoto hii, hali hiyo itapunguza unyanyapaa miongoni mwa jamii inayotuzunguka", alisema Dk. Peter Piot kwa niaba ya wenzake.

Wakitoa mawazo yao  wake hao wa marais waliohudhuria mkutano huo walisema kuwa licha ya ugonjwa wa UKimwi kuua watu wengi Barani Afrika pia kuna ugonjwa wa kansa ya Shingo ya kizazi, matatizo ya uzazi hasa wakati wa kujifungua ambayo yanaua wanawake na watoto wengi na unyanyasaji wa kijinsia.

Walisema, “Ili kuweza kutatua matatizo haya ushirikiano wa pamoja unatakiwa kati ya nchi zilizoendelea na bara la Afrika ,  tuwekeze  zaidi kwa kutoa elimu kwa jamii hasa kina mama wa majumbani ambao hawana mahali pa kupata elimu”.

Nao baadhi  ya wanawake  wanaoishi na VVU kutoka barani Afrika   waliuomba umoja huo uweze kuwasaidia kwani bado kuna unyanyapaa mkubwa hasa kwa wanawake na watoto katika  jamii inayowazunguka.

Kongamano hilo ambalo kwa mara ya kwanza limehudhuliwa na wake wa marais wa Afrika akiwemo Mke wa Rais Mama Salma Kikwete ambaye kupitia taasisi yake ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) anafanya kazi ya kuhakikisha kuwa tatizo la vifo vya kina mama wajawazito na watoto vinapungua nchini, kuwawezesha wanawake kiuchumi na kuhakikisha kuwa mtoto wa kike ambaye ni yatima na anatoka katika mazingira hatarishi anapata elimu sawa na watoto wengine.

Wizara ya mambo ya Nje ya Japani ndiyo iliyoandaa Kongamano hilo kwa kushirikiana na Kituo cha Kimataifa cha Japani  cha mabadilishano na mradi maalum wa wanafunzi kwa ajili ya Mkutano wa tano wa kimataifa wa Tokyo kwa maendeleo ya Afrika (TICAD).

No comments: