Tangazo

June 10, 2013

Taifa Stars yafa kiume Morocco, yafungwa mabao 2-1

Kikosi cha kwanza cha Taifa Stars kilichoshuka dimbani.


TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars imefungwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Marakech mjini hapa na wenyeji Morocco, katika mchezo wa Kundi C kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia Brazil mwakani.

Hadi mapumziko, Morocco walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililotiwa kimiani na Abderazak Hemed Allah dakika ya 37, baada ya yeye mwenyewe kujiangusha kwenye eneo la hatari baada ya kugongana na Aggrey Morris.

Morris alitolewa kwa kadi nyekundu baada ya hapo na Stars wakabki pungufu.

Morocco ndiyo waliocheza vizuri zaidi kipindi cha kwanza wakishambulia zaidi upande wa kulia alipokuwa akikimbiza Belhanda

Dakika ya 25 Thomas Ulimwengu alifanya kazi nzuri ya kumtoka beki, lakini shuti lake likadakwa na kipa. 

Kocha Kim Poulsen aliwapumzisha kwa mpigo washambuliaji Mrisho Ngassa na Ulimwengu dakika ya 44 na kuwaingiza beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na kiungo Khamis Mcha ‘Vialli’.

Kipindi cha pili Morocco walirejea na moto tena, wakiishambulia zaidi Stars iliyoonekana kudhoofika na katika dakika ya 50 Youssef El Arabi  akafunga  bao la pili kiulaini baada ya kuwatoka mabeki wa Tanzania na kubaki na kipa Juma Kaseja.

Hata hivyo, shambulizi la kushitukiza liliipatia Taifa Stars inayodhaminiwa na Bia ya Kilimanjaro Premium Lager bao la kwanza dakika ya 61 lililofungwa na Amri Kiemba kwa shuti la mbali kutoka wingi ya kushoto.

Morocco waliendelea kutawala mchezo na Stars walikuwa wakifanya mashambulizi ya kushitukiza ambayo kwai kiasi fulani yalikuwa ya matumaini.

Dakika ya 82 Kim alimpumzisha Vialli na kumuingiza John Bocco ‘Adebayor’ ambaye aliongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji.  

Kwa matokeo hayo, Stars inabaki na pointi zake sita baada ya kucheza mechi nne, kushinda mbili nyumbani na kufungwa mbili zote ugenini, nyingine ikiwa dhidi ya Ivory Coast.

Lakini Stars inabaki nafasi ya pili mbele ya Morocco yene pointi tano sasa, wakati Ivory Coast wanaongoza kwa pointi zao saba kabla ya matokeo ya mechi na Gambia leo.

kikosi cha Stars kilikuwa; Juma Kaseja, Shomary Kapombe, Erasto Nyoni, Kevin Yondan, Aggrey Morris, Frank Domayo, Amri Kiemba, Salum Abubakar, Thomas Ulimwengu/Khamis Mchadk44/John Boccodk82, Mbwana Samatta na Mrisho Ngassa/Nadir Haroub dk44.

Stars bado inashika nafasi ya pili katika Kundi c na pointi 6 huku Ivory Coast ikiongoza kwa pointi 10 baada ya kuifunga Gambia 3-0 jana wakati Morocco ni wa tatu na pointi 5 na Gambia pointi 2.

Taifa Stars itacheza na Ivory Coast Jumapili ijayo jijini Dar es Salaam wakati Gambia itacheza na Morocco.

Mechi ilishuhudiwa na watanzania takriban 500 waliotoka Dar, waishio Morocco na nchi jirani wakiongozwa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Amos Makala.

Kamati ya Ushindi ya Taifa Stars pia iliwakilishwa na wajumbe kadhaa akiwemo Kaimu Mwenyekiti Ramadhan Dau, Mohamed Dewji na Zitto Kabwe.

Taifa Stars inatarajiwa kurejea nyumbani kesho Jumatatu saa kumi na moja na nusu alfajiri kwa ndege ya Shirika la Egypt Air.

No comments: