NA ELIPHACE MARWA
JAJI Kiongozi
wa Mahakama Kuu Tanzania Mh. Fakih Jundu (pichani), amewaasa waandishi wa habari kuwa
makini pindi wanapo andika habari zinazohusu mahakama ili kuondokana na tatizo
la kuingilia uhuru wa mahakama.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es salaam na
Jaji Kiongozi Fakih
alipokutana na waandishi wa habari ofisini kwake kufuatia taarifa
zilizochapishwa na gazeti moja la kila wiki linalotuhumu muhimili huo kwa
kushindwa kuwachukulia hatua stahiki watuhumiwa wa kesi za madawa ya kulevya.
"Huku ni kutaka kupambanisha wananchi
na mahakama yao ambayo wana imani nayo, ni vyema waandishi kupata ufafanuzi wa
kina wa mambo mbalimbali kabla ya kuandika habari isiyo ya kweli na yenye lengo
la kupotosha Umma", alisema Jaji Fakih.
Aidha
Jaji Fakih aliongeza kuwa ni vema kwa waandishi wa habari kuwa makini na
uandishi wa habari zinazohusu mahakama kwa kuwa na ushahidi wa kutosha kwani
kwenda kinyume na hapo ni kuingilia uhuru wa mahakama na si vizuri kwa
waandishi wenye ueledi kuandika habari kwa ushabiki.
"Mengi ya mashauri yaliyotajwa na gazeti hilo bado yako mahakamani
hivyo si vyema kuingilia uhuru wa mahakama hivyo habari hii inapaswa kukemewa
kwa kosa la kuzungumza mambo yaliyo mahakamani", aliongeza Jaji Fakih.
Akizungumzia
suala la kuwepo mahakama maalumu zitakazosimamia kesi za dawa za kulevya Jaji
Kiongozi huyo amesema kama itaundwa na kuwezeshwa vizuri zinaweza kufanya kazi
ila kama hazitawezeshwa kwa kupatiwa fedha na
rasilimali watu hazitaweza kufanya kazi ipasavyo.
No comments:
Post a Comment