Assa Mwambene |
Na Fatma Salum- MAELEZO
SERIKALI ya Tanzania imetoa ufafanuzi kuhusu
tuhuma mbalimbali dhidi yake zilizotolewa na mtandao wa kijamii wa nchini Kenya
ujulikanao kama www.standardmedia.co.ke unaosadikika kuendeshwa na kampuni ya gazeti la The Standard la nchini
humo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Msemaji wa
Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari- (MAELEZO) Assah Mwambene , alisema
mtandao huo umeripoti kuwa Serikali
ya Tanzania imekataa kuiuzia Kenya gesi asili ya Songosongo jambo ambalo halina
ukweli kwa kuwa gesi inayozalishwa hivi sasa
bado haijafikia kiasi cha kuweza kuuzwa nje ya nchi.
Mtandao
huo pia umeripoti kuwa Serikali ya Tanzania ilikataa viwanja vyake vya ndege
vya kimataifa kutumiwa na ndege zilizopaswa kutua katika uwanja wa ndege wa
kimataifa wa Jomo Kenyata wakati wa ajali ya moto iliyotokea kwenye uwanja huo
hivi karibuni.
Mwambene
alifafanua kuwa tuhuma hizo ni za uongo kwani mara baada ya uwanja wa ndege wa
Jomo Kenyata kuwaka moto, ndege zilizotakiwa kutua uwanjani hapo ziliruhusiwa
kutua kwenye viwanja vya ndege vya Tanzania vya Julius Nyerere International Airport (JNIA) na
Kilimanjaro International Airport (KIA).
“Sio
kweli hata kidogo kwamba Tanzania ilikataa ndege za Kenya zisitue kwenye
viwanja vyake kwa sababu uwanja wa Jomo Kenyata ulipoungua ndege nyingi
zilizopaswa kutua katika uwanja ule zilitua kwenye viwanja vyetu na hii pia
ilitokana na ukweli kwamba Tanzania na Kenya zinachangia ndege nyingi za nje ya
nchi,” alisema Mwambene.
Aidha
Mwambene alikanusha tuhuma nyingine iliyodai kuwa mwaka 2010 Tanzania ilikataa
kuiuzia Kenya chakula badala yake ikaiuzia nchi ya Uganda taarifa ambazo si za
kweli kwa kuwa mwaka huo nchi nyingi za Afrika zilikumbwa na baa la njaa
ikiwemo Tanzania yenyewe.
Hivyo Tanzania ililazimika kusitisha utoaji wa
vibali kwa wafanyabiashara kuuza chakula nje ya nchi na hakukuwa na taarifa
yoyote ya kuuzwa chakula nchini Uganda.
Kutokana na upotoshaji huo Mwambene
alisema Serikali ya Tanzania imeutaka mtandao huo kuomba radhi na isipofanya
hivyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Katika hatua nyingine Mwambene alifafanua
kuwa zoezi linaloendelea nchini la
kuwataka wahamiaji haramu wanaoishi hapa kinyume cha utaratibu kuondoka kwa
hiari haliwahusu wakimbizi waliopo nchini kisheria.
Pia zoezi hilo linawalenga wahamiaji
haramu wote kutoka nchi za Rwanda, Burundi, Congo DRC, Zambia na Uganda na
hakuna serikali ya nchi yoyote kati ya hizo iliyolalamika kuhusu hatua hiyo.
“Mpaka
sasa zoezi linaenda vizuri hakuna taarifa yoyote ya malalamiko kutoka Zambia,
DRC, Burundi, Rwanda wala Uganda na tayari Rwanda imetuma taarifa rasmi
kuishukuru serikali ya Tanzania kwa kuendesha vema zoezi hilo. Kinachoandikwa
na baadhi ya vyombo vya habari ni upotoshaji unaolenga maslahi binafsi ,”
alisisitiza.
Akizungumzia
usalama wa Watanzania nchini Rwanda, Mwambene alisema hakuna taarifa ya Mtanzania yeyote kunyanyaswa
nchini humo na uhusiano wa kidiplomasia kati
ya Rwanda na Tanzania haujakatika.
No comments:
Post a Comment