Mama Salma Kikwete |
Na Anna Nkinda- Maelezo, Lindi
Wakazi wa kata ya Msinjahili wilayani Lindi wametakiwa
kutoogopa kuvuta umeme majumbani mwao kwa kuhofu kuwa wakifanya hivyo
wataonekana ni matajiri kwani matumizi ya umeme ni ya gharama naafuu
ukilinganisha na mafuta
ya taa.
Mwito huo umetolea jana na Mjumbe wa Halmashauri
Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa (NEC) wilaya ya Lindi mjini wakati
akiongea kwa nyakati tofauti na viongozi wa Halmashauri kuu ya tawi
ya Chama hicho katika matawi ya Muungano, Jitegemee, Sinde na Mnali
yaliyopo katika kata ya Msinjahili wilaya ya Lindi mjini.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mke wa Rais Jakaya Mrisho
Kikwete alisema ili kuboresha maisha ya wananchi Serikali imejitahidi
kupitisha umeme wa gesi katika vijiji vilivyopo katika kata hiyo na
kupunguza gharama ya uvutaji ambazo ni nafuu jambo la muhimu ni kwa
wananchi kuutumia.
“Kuwa na umeme nyumbani kwako na kuutumia ni mwanzo wa
maendeleo, hata watoto wako wataweza kuutumia mwanga huo kwa kujisomea
hasa nyakati za usiku na hivyo kufanya vizuri katika mitihani yao”,
alisema Mama Kikwete.
Aidha Mjumbe huyo wa NEC pia aliwataka
viongozi hao wa Halmashauri kuu ya tawi kuwahimiza watu
wanaowaongoza katika maeneo yao kutumia mvua zinazoendelea kunyesha kulima
chakula cha kutosha jambo ambalo litawafanya kuwa na chakula cha ziada na hivyo
kuepukana na kitendo cha kuomba chakula kwa majirani.
Akizungumzia kuhusu suala la uongozi Mama Kikwete
aliwahimiza wanawake kutoogopa kuomba na kugombea nafasi mbalimbali za
uongozi katika chaguzi zijazo ili waweze kupata nafasi ya kuongoza
na hivyo kufika katika ngazi ya maamuzi.
Mama Kikwete alisisitiza , “Sisi wanawake tunakabiliwa
na changamoto nyingi na mtu pekee anayeweza kuziongelea changamoto zetu
kiusahihi ni mwanamke mwenyewe hivyo basi msiogope kugombea nafasi mbalimbali
za uongozi wakati wa uchaguzi ukifika mkifanya hivyo kutakuwa na viongozi wengi
wanawake ambao wataweza kuwakilisha matatizo na mawazo yetu katika ngazi za juu
za uongozi wa chama na Serikali”.
MNEC huyo alimalizia kwa kuwahimiza viongozi hao wa
Halmashauri kuu ya tawi ya CCM kuishi maisha ya upendo, mshikamano na
amani kwani jamii ikiishi maisha hayo itaweza kufanya shughuli mbalimbali za
maendeleo kwa kushirikiana.
Kwa upande wake katibu wa Jumuia ya Wazazi mkoa
wa Lindi Haji Tajiri aliwataka viongozi hao kuwa waaminifu katika ndoa
zao na kuepuka tabia ya kuwa na mpenzi zaidi ya mmoja (michepuko) kwa
kufanya hivyo wataepukana na ugonjwa wa Ukimwi.
“Chama Cha Mapinduzi kinahitaji kuwa na watu
wenye afya njema ili waweze kufanya vizuri kazi za chama nawaomba muwe
waaminifu kwa wapenzi wenu mkifanya hivyo mtaepekana na Ugonjwa wa Ukimwi”,
alisema Tajiri.
Katibu huyo wa Jumuia ya Wazazi mkoa pia aliwaomba
kinamama kuiga mfano wa Mama Salma Kikwete ambaye anafanya
kazi kubwa ya kujitoa katika shughuli mbalimbali za kijamii na kutetea haki
zao, wasichana na watoto na kuongeza kwamba anastahili
pongezi kwani yeye ni mama na mlezi wa taifa.
Mjumbe huyo wa NEC taifa akiwa katika kata ya
Msinjahili alifungua mashina ya wakereketwa wa CCM Jumuia ya wazazi
katika tawi namba tatu la Sinde na namba mbili la
Mnali.
Mama Kikwete ambaye ni mjumbe wa NEC Taifa kupitia
wilaya ya Lindi mjini alikutana na viongozi hao wa Halmashauri kuu ya tawi ya
CCM kwa ajili ya kuimarisha kazi za chama hicho ikiwa ni pamoja na kufanya
vikao na viongozi.
No comments:
Post a Comment