RAIS
JAKAYA KIKWETE APOKEA TUZO YA KIONGOZI BORA BARANI AFRIKA.
Na.
Aron Msigwa- MAELEZO.
Dar es salaam.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete Ikulu jijini
Dar es salaam amepokea Tuzo ya Utumishi Bora wa Umma Barani Afrika kufuatia
mchango mkubwa alioutoa kwa maendeleo ya
wananchi wa Tanzania na Bara la Afrika.
Akiwa
mwenye furaha mara baada ya kupokea tuzo hiyo ambayo awali ilipokelewa kwa
niaba yake na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Bernard
Membe jijini Washngton Marekani, Rais
Kikwete amesema kuwa ameipokea tuzo hiyo kwa moyo wa shukrani na heshima kubwa
kufuatia imani kubwa iliyoonyeshwa kwake na kwa watanzania.
“Nimeipokea
tuzo hii kwa moyo wa ukunjufu, ni tuzo ya watanzania wote kwa sababu mambo yote
niliyoyafanya sikuwa peke yangu nimeyafanya kwa kushirikiana na watanzania
wote” Amesema Rais Kikwete.
Rais
Kikwete amesema kuwa amepokea tuzo hiyo kufuatia wasomaji na wadau wa Jarida la
African Leadership Magazine ambalo huchapishwa mjini London, Uingereza na mjini
Washington kuonyesha imani juu yake kwa kumchagua kwa njia ya kura ya maoni
kama kiongozi aliyetoa mchango mkubwa zaidi kwa maendeleo ya wananchi wake
katika Bara la Afrika kwa mwaka 2013.
“Nawashukuru
sana African Leadership Magazine, kwangu ni heshima kubwa nawaomba watanzania
tuendelee kushirikiana wenzetu duniani wanaona, wanatambua na kuthamini mchango
wetu” Amesisitiza Rais Kikwete.
Awali
kabla ya kumkabidhi Rais Jakaya Kikwete Tuzo hiyo na cheti cha shukrani Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mh. Benard Membe amesema kuwa tuzo
hiyo ni heshima kwa taifa la Tanzania kufuatia juhudi kubwa alizoonyesha Rais
Jakaya Kikwete katika kuboresha maisha ya watanzanzania.
Amesema kuwa wasomaji na wadau wa jarida maarufu la
kimataifa la African Leadership Magazine wamemuona Rais Kikwete kuwa Kiongozi Bora
wa Afrika aliyetoa mchango mkubwa zaidi katika maendeleo ya kiuchumi ya
wananchi wake kwa mwaka 2013 kwa kumpigia kura nyingi za maoni.
Aidha
ameeleza kuwa Rais Kikwete alitangazwa kuwa mshindi wa tuzo hiyo katika sherehe
kubwa iliyotangazwa na kuonyeshwa moja kwa moja na mitandao mbali mbali ya
kijamii duniani pia kuhudhuriwa na watu mbali mbali mashuhuri wakiwemo mabalozi
wanaoziwakilisha nchi zao Marekani na Naibu Spika wa Bunge la Tanzania
Mheshimiwa Job Ndugay ambaye alikuwa Washington kikazi.
Wengine
ni Mwakilishi katika Bunge la Wawakilishi wa Jimbo la Georgia nchini Marekani
na mwenyekiti wa wabunge weusi katika Bunge hilo, Bi. Dee Dawkins-Haigler na
Balozi wa Tanzania nchini Marekani Mheshimiwa Liberata Mulamula.
Rais
Kikwete amepata tuzo hiyo akimfuatia Rais wa Sierra Leone , Mheshimiwa Ernest Bai
Koroma, ambaye alishinda Tuzo hiyo mwaka 2012.
No comments:
Post a Comment