Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Saidi
Meck Sadiki akitoa taarifa ya kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa (RCC) ofisini
kwake leo jijini Dar es salaam.
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Na. Aron Msigwa –MAELEZO.
Dar es salaam.
Jumla ya kata 22 katika manispaa za Ilala, Kinondoni na
Temeke zitaingizwa katika mpango wa utengaji wa maeneo maalum (smart
area) kwa ajili ya kuboresha usafi wa mazingira jijini Dar es salaam.
Akitoa taarifa ya kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa wa Dar
es salaam (RCC) leo jijini Dar es salaam, Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Saidi
Meck Sadiki amesema uanzishaji wa maeneo maalum ya usafi wa mazingira unalenga
kuondoa shughuli zote zinazofanyika katika maeneo mbalimbali ya jiji kinyume
cha sheria na kulifanya jiji la Dar es salaam kuendelea kuwa katika
hali isiyoridhisha ya usafi wa mazingira.
Amesema utekelezaji wa mpango huo wa utengaji wa maeneo
maalum unazingatia sheria ya mipango miji Na. 8 ya mwaka 2007 na sheria ya
mazingira Na. 20 ya mwaka 2004 na kuzitaja kata zitakazohusika katika
mpango huo kuwa ni pamoja Keko, Chang’ombe, Kurasini, Mibulani , Sandali na
kata ya Gerezani zote za manispaa ya Temeke.
Kata nyingine ni Mchafukoge, Kariakoo, Mchikichini,
Jangwani, Kisutu, Kivukoni,Upanga Mashariki na Upanga Magharibi ambazo ziko
manispaa ya Ilala na kata za Hananasif, Kinondoni, Kigogo, Mzimuni na Magomeni
zote za manispaa ya Kinondoni.
Amesema kuwa ili kufanikisha utekelezaji wa mpango huo
hatua mbalimbali zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuondoa shughuli zote
zinazosababisha kero katika eneo husika, biashara zisizo rasmi, biashara za
vyakula, uchomaji nyama na mahindi kando kando ya barabara na maeneo ya
watembea kwa miguu, uondoaji wa gereji bubu, maguta, mikokoteni bajaji na
bodaboda katikati ya jiji.
Shughuli nyingine zitakazofanyika ni zile za uondoaji wa
malori makubwa yenye zaidi ya tani 10 katika maeneo yasiyoruhusiwa na
kubainisha halmashauri zinaendelea kutenga maeneo kwa ajili ya shughuli hizo.
“Halmashauri zetu zinaendelea kutenga maeneo kwa ajili ya
shughuli zote tulizoziainisha kwa ajili ya shughuli mbalimbali za wananchi japo
kuna maeneo tuliyoyatenga kwa wananchi hayatumiki na baadhi ya wahusika hawako
tayari kwenda kwenye maeneo hayo” amesema.
Kuhusu waendesha bodaboda na bajaji kuendelea kuingia katika
maeneo yasiyoruhusiwa hususani katikati ya jiji la Dar es salaam amesema kuwa
serikali haitalifumbia macho suala hilo kwa kuwa liko kisheria.
Amesema watekelezaji wa sheria ya SUMATRA ya kuhifadhi
maeneo yaliyotengwa wanaendelea na zoezi la kuwaondoa wote wanaovunja sheria
hiyo na kutoa wito kwa wahusika wa zoezi hilo kuliendesha kwa kufuata sheria,
taratibu na kuzingatia utu na haki za binadamu.
“Nimeshatoa maagizo kwa watendaji na viongozi wanaosimamia
zoezi hili wahakikishe wanaheshimu utu na haki za binadamu, kama ni kampuni
ikigundulika tutaifungia isipate tenda zozote za serikali, nachosema wahusika
wawe makini serikali hatutawavumilia wanaoendesha vitendo vya hujuma, uonevu,
wizi, uporaji na ukiukaji wa haki za binadamu” Amesisitiza.
Aidha ameeleza kuwa mkoa wa Dar es salaa licha ya
kukabiliwa na changamoto ya ufinyu wa bajeti unaendelea kutekeleza
shughuli mbalimbali zenye tija kwa maendeleo ya wananchi zikiwemo
Elimu, Afya, ujenzi na ukarabati wa barabara, madaraja na miundombinu mingine
ya jiji ambayo imeharibiwa na mvua zinazoendelea kunyesha.
Amesema katika kuimarisha huduma za afya mkoa kupitia kamati
ya ushauri ya mkoa (RCC) imepitisha maombi maalum ya zaidi ya shilingi bilioni
45 nje ya bajeti ili kukabiliana na tatizo la msongamano mkubwa wa wagonjwa wa
nje na wale wanaolazwa katika hospitali za mkoa wa Dar es salaam.
Amesema kuwa mkoa wake unapata wagonjwa wengi wa nje kutoka
maeneo mbalimbali yakiwemo ya Kisarawe, Mkuranga, Mafia, wilaya ya
Bagamoyo,Kibaha na Chalinze jambo linaloongeza mzigo kwa hospitali za mkoa huo.
“Mkoa wa wetu wa Dar es salaa una idadi kubwa ya watu kuliko
mikoa mingine nchini pia unahudumia watu wengine wengi kutoka maeneo mbalimbali,
jambo hili linaongeza mzigo kwa hospitali zetu kutokana na kuwahudumia wananchi
kutoka nje ya mkoa” Amesisitiza.
Ameeleza kuwa wagonjwa wa nje sasa wanafikia 1500 hadi 2000
kwa siku jambo linalowafanya kuomba fedha zaidi kwa ajili ya ukarabati na
upanuzi wa hospitali za rufaa za mkoa na ujenzi wa hospitali maalum kwa ajili
ya mama na motto itakayokuwa na uwezo wa kulaza wagonjwa 600 kwa wakati mmoja.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Saidi
Mecki Sadiki ameeleza kuwa mkoa wake una dhamira ya kuongeza maeneo mapya ya
utawala kwa kuongeza kata 113 na mitaa 570 pamoja na kupitia mapendekezo
yaliyowasilishwa kwenye kikao Maalum cha kamati ya ushauri ya mkoa na
mabaraza ya madiwani ya halmashauri husika kuhusu kuugawa mkoa wa
Dar es salaam katika muundo wa wilaya 5.
Amesema kuwa wilaya zilizopendekezwa ni pamoja na Ilala,
Kinondoni, Temeke, wilaya ya Kigamboni na wilaya ya Ubungo.
No comments:
Post a Comment