KAMATI ya Utendaji
ya Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) ilikutana Dar es
Salaam juzi Jumatatu na kujadili masuala mbalimbali yahusiyo chama hicho.
A: Mjadala
wa Michezo
Kikao kilikubaliana
TASWA iendeshe mjadala kuhusiana na masuala mbalimbali ya kimichezo kila
Jumatano ya kwanza ya mwezi, ambapo
wataalikwa wataalamu mbalimbali kutoka
vyama vya michezo, wanamichezo maarufu, wahariri wa habari za michezo na
waandishi wa habari za michezo kujadili hoja husika.
Kutakuwa na
wazungumzaji maalum kuhusu mada husika, ambapo wageni waalikwa watachangia kwa
nia ya kuboresha kwa maslahi ya ustawi wa michezo hapa nchini.
Kwa kuanzia
mjadala huo utafanyika Juni 4, mwaka huu katika ukumbi ambao utatangazwa hivi karibuni
na mada itakuwa nafasi ya Tanzania katika Michezo ya Jumuiya ya Madola
itakayofanyika Glasgow, Scotland kuanzia Julai 23 hadi Agosti 3 mwaka huu,
ambapo Tanzania itashiriki katika michezo ya ngumi, riadha, kunyanyua vitu
vizito, mpira wa meza, judo na kuogelea.
Pamoja na
kuwaalika viongozi wa vyama mbalimbali vya michezo, pia utaratibu umeanza ili
kuwaalika baadhi ya Watanzania waliopata medali katika mashindano hayo ili nao
waweze kuzungumza na kuwahamasisha wanamichezo wa sasa wafanye vizuri.
B:TUZO
ZA WANAMICHEZO BORA
Kamati ya Utendaji imepongeza juhudi zinazofanywa na
Kamati ya Tuzo za Wanamichezo Bora inayoongozwa na Mkurugenzi wa Redio Times
FM, Rehure Nyaulawa katika kuhakikisha tuzo hizo zinakuwa bora na za aina yake
mwaka huu.
Tayari wadau
kadhaa wameonesha nia ya kudhamini tuzo hizo, ambapo maelezo zaidi yatatolewa
baada ya kikao cha Kamati ya Tuzo kufanyika Jumatatu wiki ijayo kujadili
maendeleo kuhusiana na tuzo hizo.
C;UANZISHAJI WA SACCO’S
Kikao kiliteua
wanachama sita wa TASWA, kuratibu na kuandaa Katiba ya Chama cha akiba na
Mikopo (SACCO’S) kwa ajili ya wanachama wa TASWA na kusimamia uanzishwaji wake.
Kamati hiyo
itaongozwa na Mhariri wa michezo wa gazeti HabariLeo, ambaye pia ni Mwenyekiti
wa Bodi ya Mikopo ya SACCO’S ya Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), Mgaya
Kingoba na Katibu wa kamati atakuwa Mhazini Mkuu wa TASWA, Shija Richard ambaye
kitaaluma ni Mhasibu.
Wengine
walioteuliwa ni Mhazini Msaidizi wa TASWA, Zena Chande, mwandishi wa habari wa
TBC1, Angela Msangi, Mwandishi wa habari wa gazeti la Majira, Masau Bwire na
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TASWA, Chacha Maginga. Kamati imepewa miezi
mitatu kukamilisha mchakato huo kuanzia Juni mosi mwaka huu.
D; MAFUNZO
Kikao
kilikubaliana kufanyike semina mbili kabla ya Agosti mwaka huu, ambapo bajeti
ya suala hilo imeshapitishwa, hivyo sekreterieti ya TASWA imeagizwa kufanyia
kazi suala hilo kwa kupanga Mkoa ambao itafanyika. Semina ya kwanza itafanyika
Dar es Salaam na nyingine nje ya Mkoa wa Dar es Salaam. Kabla ya Jumanne wiki
ijayo agizo hilo litakuwa limeshafanyiwa kazi.
Lengo la mafunzo
hayo ni kuwekana sawa katika masuala mbalimbali ya kitaaluma na pia yale
yahusiyo ripoti za michezo. Msisitizo ukiwa ni kuhakikisha wanachama wengi
zaidi wa TASWA wanashiriki mafunzo yote hayo.
Kamati pia ilijadili
kuhusiana na mafunzo ya waandishi chipukizi wanaotakiwa na Chama cha Kimataifa
cha Waandishi wa Habari za Michezo (AIPS),
ambapo Makamu Mwenyekiti wa TASWA, Egbert Mkoko ameteuliwa kusimamia
mchakato wa kupata waandishi chipukizi
ambao wasifu wao utatumwa AIPS ili waombewe kushiriki mafunzo hayo.
Hivyo
kinachotakiwa waandishi wa habari za michezo ambao wana chini ya miaka minne
katika fani na umri wao ni chini ya miaka 25, wana elimu kuanzia ngazi ya
stashahada mpaka shahada watume wasifu wao binafsi na vyeti vya kitaaluma kwa
Makamu Mwenyekiti TASWA kwa email: njali5@yahoo.com
na taswatz@yahoo.com, ambapo mwisho ni
Mei 30 mwaka huu.
E; MEDIA DAY
Hili pia
lilijadiliwa kwa kirefu, ambapo mazungumzo na wadhamini bado yanaendelea na
kesho Alhamisi kutakuwa na kikao kingine kati ya TASWA na wadhamini kuweka
tarehe mpya ya tamasha hilo kwa mwaka huu.
Imetolewa na,
Amir Mhando
Katibu Mkuu TASWA
14/05/2014
No comments:
Post a Comment