Na Anna Nkinda – Maelezo
Ushirikiano wa pamoja unatakiwa baina ya wanafunzi,
walezi, wazazi, jamii na walimu ili kuweza kujenga, kuimarisha na kukuza
nidhamu , mwenendo na tabia ya mtoto jambo ambalo litaleta mafanikio chanya
pamoja na kutatua changamoto za kitaaluma na kimazingira.
Hayo yamesemwa jana na Mke wa Rais Mama
Salma Kikwete (pichani), wakati akiongea na walimu pamoja na wanafunzi wa shule ya
Sekondari Salma Kikwete iliyopo kata ya Kijitonyama wilaya ya Kinondoni
jijini Dar es Salaam.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya
Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema nidhamu ya mwanafunzi siyo tu kumuamkia
mwalimu bali pia kujua wajibu wake kama vile kuwahi shuleni, kufanya mazoezi ya
darasani na kusoma kwa bidii.
“Neno nidhamu lina dhana pana kwani linagusa wengi
lakini katika mazingira ya leo walengwa wakubwa ni mzazi,mlezi au jamii,
mwalimu na mwanafunzi. Kazi ya mzazi, mlezi na jamii ni kuhimiza na
kufuatilia maendeleo ya mtoto.
Mwalimu kufundisha, kuingia darasani kwa wakati
na kujiandaa na kwa mwanafunzi ni kupokea maarifa anayopewa na mwalimu
wake na kusoma kwa bidii”, alisema Mama Kikwete.
Kwa upande wa wanafunzi aliwasihi kuongeza juhudi
katika masomo na kufanya vizuri kwenye mitihani, kwani wao na wengine
wote wanategemewa na familia, jamii zao na taifa kwa kuwa watakuwa wakombozi
siku za baadaye na kumuomba Mwenyezi Mungu awape nguvu na ujasiri katika
safari yao ndefu ya kufatuta elimu.
Aidha Mama Kikwete aliwapongeza walimu wa shule hiyo
kwa kazi kubwa wanayoifanya ya uboreshaji wa elimu pamoja na kukabiliwa na
changamoto kadhaa lakini kadri siku zinavyokwenda mbele ndivyo Serikali
inavyozidi kutatua changamoto mbalimbali zinazowahusu walimu.
Mwenyekiti huyo wa WAMA alisisitiza, “Walimu
timizeni wajibu wenu kwa kufika kazini mapema, kumaliza silabasi
kwa wakati, kukamilisha maandalio ya masomo, kufundisha kila kipindi bila
kukosa, kujua taarifa na udhaifu wa wanafunzi wenu na kuwa kiungo kati yenu
na wazazi au walezi hiyo ndiyo nidhamu ya mwalimu na ndiyo ualimu”.
Akisoma taarifa ya shule hiyo Mwalimu Elestina Chanafi
alisema shule hiyo ilianza mwaka 2007 ikiwa na wanafunzi 320, walimu 13 na
vyumba vya madarasa sita hivi sasa ina wanafunzi 1229, walimu 33 na
vyumba vya madarasa 22. Hadi sasa jumla ya wanafunzi 1161 wamehitimu masomo yao
tangu walipoanza kutoa kidato cha nne mwaka 2010.
Mwalimu Chanafi ambaye ni Mkuu wa shule hiyo
alisema wamefanikiwa kuchimba kisima cha maji kwa msaada wa wakorea,
kuunganisha umeme, kununua vifaa mbalimbali vya uchapaji na udurushaji, kuboresha
mazingira kwa kiwango cha kutia moyo na kuweza kuwavutia wanafunzi ili
wajisikie kuwa sehemu ya shule.
Kuanzisha maabara ya muda ambayo imewawezesha
wanafunzi wa sayansi kufanya mitihani kwa vitendo na kuongeza kiwango cha
ufaulu kwa masomo hayo na kupata wanafunzi wa kujiunga na masomo ya ngazi ya
juu kwa idadi nzuri.
“Changamoto zinazotukabili ni uchakavu wa baadhi ya
vyumba vya madarasa, mmomonyoko mkubwa wa maadili ambao unasababisha ugumu
katika kudhibiti nidhamu ya wanafunzi, uelewa mdogo wa wazazi juu ya mchango
wao kwa maendeleo ya wanafunzi, kiwango kidogo cha ruzuku toka Serikalini
ambacho hakiletwi kwa ukamilifu na wakati, ufinyu wa bajeti na ulegevu wa
uchangiaji wa ada na michango mingine toka kwa wazazi”, alisema Mwalimu
Chanafi.
Naye Mkuu wa wilaya ya Kinondoni Jordan Rugimbana
alimshukuru Mama Kikwete kwa kupata nafasi ya kuitembelea shule hiyo na
kumpongeza kwa kazi anayoifanya ya kuinua kiwango cha elimu nchini na
kuendeleza fani yake ya ualimu kwa faida ya kizazi cha leo na kijacho kwa
kuwasomesha watoto zaidi ya 600 hawa ni mbali na wanafunzi walioko Shule ya
Sekondari WAMA-Nakayama iliyopo wilaya ya Rufiji mkoani Pwani.
Mama Kikwete aliichangia shule hiyo mifuko 100 ya
simenti ambayo itatumika kuzima mashimo katika vyumba vya madarasa ambapo
wilaya ya Kinondoni itagharamia mchanga pamoja na kumlipa fundi atakayefanya
kazi hiyo.
No comments:
Post a Comment