Na Anna Nkinda – Maelezo,
Kigoma
Jamii
imetakiwa kujenga tabia ya kuchangia damu kwa hiari kitendo ambacho
kitapunguza vifo vya kina mama
wajawazito 363 vinavyotokea kila mwaka kutokana na tatizo la ukosefu wa damu
wakati wa kujifungua.
Mwito huo umetolewa
jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete (pichani), wakati akiongea na wananchi wa mkoa wa
Kigoma kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya wachangia damu Duniani
zilizofanyika kitaifa mkoani humo.
Mama Kikwete ambaye pia
ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema takwimu
zinaonyesha kuwa takribani wanawake 454 kati ya vizazi hai laki moja hufa kila
mwaka kutokana tatizo la uzazi na asilimia 80 ya vifo hivyo husababishwa na
ukosefu wa damu.
“Ni dhahiri vifo
vinavyotokana na uzazi viko juu na kwa bahati mbaya waathirika wakubwa ni
wasichana chini ya umri wa miaka 15, makundi mengine yanayohitaji kuongezewa
damu ni kina mama wajawazito wakati wa mimba na kujifungua , watoto wenye umri
wa chini ya miaka mitano kwa ukosefu wa damu unaosababishwa na malaria kali na
magonjwa mengine, ajali, wagonjwa wa saratani, upasuaji mkubwa wa moyo, anemia,
seli mundu na hemophilia.
Ni wajibu wetu sote
kuhakikisha kwamba tunatoa damu ili jamii yetu iweze kutimiza mahitaji yake
kwani tunapokuwa na akiba ya damu iliyo salama tunajihakikishia tiba ya ndugu
zetu pale wanapopata matatizo bila ya siye kulazimika kutoa damu ya papo kwa
hapo”, alisema Mama Kikwete.
Mwenyekiti hiyo wa WAMA
alisema mtu yeyote mwanamke au mwanaume anaweza kuchangia damu ikiwa ana afya
njema, umri kati ya miaka 18 hadi 65, uzito usiopungua kilo 50, uwingi wa damu
zaidi ya gramu 12 kwa desilita, kutokuwa na shinikizo la damu na kwa mwanamke asiwe mjamzito au ananyonyesha.
Kwa upande wake Naibu
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt.
Stephen Kebwe alisema tangu kuanzishwa kwa mpango wa damu salama mwaka 2004
kumekuwa na ongezeko la wachangia damu kwa hiari kutoka kiasi cha chupa 5000 kwa
mwaka 2005 hadi chupa 160000 kwa mwaka 2013.
“Changamoto
zinazoukabili mpango huu ni mahitaji makubwa kuliko upatikanaji wa damu inakadiriwa
mahitaji ya damu kwa mwaka kitaifa ni
wastani wa chupa 400000 hadi 450000,
uelewa mdogo wa jamii kuhusu suala zima la uchangiaji damu kwa hiari, uuzwaji
wa damu usio halali Hospitalini jambo ambalo linakatisha tamaa wachangia damu
wa hiari na matumizi yasiyo sahihi ya damu katika Hospitali”, alisema Dkt.
Kebwe.
Naibu waziri huyo wa
Afya na Ustawi wa Jamii alisema mpango wa taifa wa damu salama unaendelea
kufanya kampeni ya kuhamasisha uchangiaji wa damu katika jamii, kuendelea
kujenga vituo vidogo vya kuchangia damu,
kutoa majibu, nasaha, na malezi kwa wiki mbili mpaka nne baada ya mtu
kuchangia damu na kuongeza mazao mbalimbali ya damu.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Luteni
Kanali Mstaafu Issah Machibya aliwashukuru wananchi wa mkoa huo kwa kujitoa
kwao katika zoezi zima la uchangiaji wa damu salama na kuweza kukusanya chupa
3620 kwa kipindi cha wiki tatu kabla ya kilele cha maadhimisho hayo na hivyo kuvuka
malengo kwa asilimia 121 kwani kabla ya kuanza kwa zoezi hilo walijipangia
kukusanya chupa salama za damu 3000.
“Mkoa
wa Kigoma hupata Damu salama kutoka kituo cha Kanda ya magharibi kilichopo
Tabora, umbali wa karibu Km 450 kutoka Kigoma mjini. Ambapo pia upatikanaji wa
damu salama umekuwa hautoshelezi mahitaji halisi ya Kimkoa yanayokadiriwa kuwa
chupa 22000 kwa mwaka”, alisema Kanali Mstaafu Machibya.
Alisema
ili kukabliana na tatizo hilo Mkoa kwa kushirikiana
na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na wadau wengine wa maendeleo uliamua
kujenga kituo kidogo cha Damu Salama katika eneo la Hospitali ya Maweni ujenzi wa kituo hicho ambacho kikikamilika kitaboresha upatikanaji wa damu ndani ya Mkoa
na kuboresha utoaji wa huduma za afya umeshaanza na utakamilika ndani ya wiki
mbili zijazo.
Katika maadhimisho hayo
Mama Kikwete alizindua mfumo wa kiektronic wa kuhifadhi kumbukumbu za wachangia
damu nchini. Pia alitoa kikombe kwa mshindi wa kitaifa kwa mwaka 2013/14 cha
sisi ni mashujaa tumeokoa maisha na
cheti kwa Shule ya Sekondari ya Bihawana iliyopo mkoani Dodoma kwa kutoa chupa nyingi za damu kwa mkupuo ukilinganisha na idadi ya wananchi
waliokuwepo na katika ngazi ya mkoa kikombe kidogo kama hicho kilienda kwa
Shule ya Sekondari Kasulu.
Mke huyo wa Rais pia
alitoa cheti kwa mwanaume aliyechangia
damu nyingi kuliko wote nchini kwa mwaka 3013/14 hii ikiwa ni mara 53 katika maisha yake Emmanuel
Essay kutoka mkoa wa Kilimanjaro na kwa upande wa mwanamke cheti hicho kilienda
kwa Restituta Mushi kutoka mkoa wa Mwanza ambaye amechangia mara 28.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Dkt. Leonard Subi
alitambuliwa na mpango wa damu salama kwa mwaka 2013/2014 na kupewa cheti kutokana
na juhudi za ziada alizozifanya za kufuatilia upatikanaji wa damu katika
Hospitali zake, kwa kushirikiana na mpango wa Taifa wa Damu salama ameweza na kuhamasisha Halmashauri kutenga bajeti ya
kukusanya damu salama na amefanikisha ujenzi wa kituo kidogo cha kukusanyia
damu.
Siku ya wachangia damu
Duniani ambayo Kauli mbiu ya mwaka huu
ni DAMU SALAMA UHAI WA MAMA ni
ukumbusho wa siku ya kuzaliwa kwa Karl Landsteiner ambaye ndiye aliyegundua mfumo wa makundi yay
a damu A, B na O na alizawadiwa tuzo ya Nobel kutokana na ugunduzi huo.
No comments:
Post a Comment