Serikali ya Tanzania imepokea shilingi bilioni 24.1 kutoka Serikali ya Japani kwa ajili ya shughuli za maendeleo hapa  nchini.
 
Akizungumza katika hafla hiyo ya kutiliana saini , Waziri  wa Fedha Sada Salum Mkuya aliishukuru Serikali ya Japani kwa kuwa na  ushirikiano mzuri na Tanzania.
 
“Mkopo huu utachangia bajeti ya serikali ya mwaka wa fedha wa 2014/2015, na fedha hizo zitaelekezwa katika sekta ya Maji, Elimu na Afya” alisema Waziri Mkuya.
                                                                                     
Mkuya aliishukuru Serikali ya Japani kwa misaada mbalimbali ambayo imekuwa ikiitoa ambayo imeleta mafanikio makubwa Tanzania.
 
Alisema kuwa kwa mujibu wa taarifa ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 ,misaada hiyo imesaidia kupunguza umaskini na kuongeza kipato kwa wananchi.
                                                                                     
Akijibu swali kuhusu fedha hizo za mikopo kuchelewa kufika, Waziri Mkuya alisema kuwa changamoto kubwa ambayo Serikali imekuwa ikiipata ni kutokana na taratibu  za sera za nchi husika ambapo kila nchi wana sera zao.
 
Kwa upande wake Balozi wa Japan Nchini Tanzania Masaki Okada alisema kuwa msaada huo unahusiana na ushirikiano wa pamoja na Benki ya Dunia katika mkopo wa kumi na moja wa kusaidia kupunguza umaskini ambao umekuwa ukitolewa tangu mwaka 2001.
 
Mikopo hiyo imekuwa ikitolewa kwa masharti ya mkataba wa mkopo nafuu wa riba ya asilimia 0.01 kwa Serikali  hapa nchini.
 
Balozi Okada alisema kuwa nchi yake imekuwa ikitoa mikopo mabalimbali ili kusaidia Serikali ya Tanzania katika kupunguza umaskini ambapo misaada hiyo imekuwa ikitumika kufuatana na GBS hapa Tanzanaia kwa kutoa fedha moja kwa moja ambazo zinalenga kuharakisha juhudi za kupunguza umasikini hususani MKUKUTA.
 
Naye Mwakilishi wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japani (JICA) nchini Yasunori Onioshi alisema kuwa shirika lake litaendelea kushirikiana na Serilkali ya Tanzania katika kusaidia bajeti yake kwani Tanzania inakua kwa haraka na mahitaji yake yanaendelea kuongezeka kila mara.
 
Makampuni ya Kijapani yanayofanya kazi na Serikali ya Tanzania ni pamoja na Kampuni ya Sigara (TCC) inayomilikiwa na Kampuni ya Kimataifa ya Tumbaku ya Kijapani, Panasonic Energy Tanzania na JICA.
 
Hali ya hewa ya Dodoma ni baridi na majadiliano kuhusu Bajeti ya Serikali yameanza na yanaendelea.
 
 
Imetolewa na:
Msemaji Mkuu
Wizara ya Fedha
16/06/2014