Na
Mwandishi Wetu
KAMPUNI
ya Simon Group Limited imesisitiza dhamira yake ya kuboresha sekta ya usafiri
katika Jiji la Dar es Salaam licha ya kampeni zinazoendelea kutoka kwa
washindani binafsi ikiwa na lengo la kuvuruga mpango unaoendelea wa
uwezekezaji katika Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) ili waweze kuitawala
biashara ya usafiri.
Kwa
mujibu wa taarifa ya UDA, mpango unaendelea wa kuifanya Dar es Salaam liwe jiji
lenye urahisi katika usafiri kwa kufanya kazi kwa karibu na Serikali na Jiji.
“Tumeona
taarifa ambazo zimekuwa zikichapishwa katika vyombo mbalimbali vya habari
ikiwamo mitandao ya kijamii kutoka katika kundi linalojiita Consortium of
Concerned Tanzanians International wakijaribu kuwafanya watu waamini kila
uwekezaji unaofanywa katika kuboresha mfumo wa usafiri jijini Dar es Salaam
kupitia UDA hauna maana.
“Hili
ni hatua inayosikitisha sana, tunajaribu kuuboresha mfumo wa usafiri Dar es
Salaam kutoka katika msongamano ili kuwa katika hali inayoridhisha kwa kuongeza
idadi ya magari na kuboresha huduma za usafirishaji lakini watu wengine
wanatumia muda mwingi kufanya kampeni zenye lengo la kuhakikisha malengo hayo
hayatimii,’’ ilisema taarifa hiyo kutoka kwa mwenyekiti ambaye pia ndiye Ofisa
Mtendaji Mkuu, Robert Kisena.
Aliitaja
kampeni hiyo iliyopewa jina la “Kampeni ya Kurudisha Shirika la Usafiri Dar es
Salaam (UDA) Mikononi mwa wananchi” inajaribu kuligeuza mtaji suala la
kujivunia umiliki wa kampuni hiyo kwa umma bila ya kuangalia ni vipi kampuni
inaweza kusimamiwa kwa namna bora na kufanikiwa kutimiza malengo ya kurahisisha
usafiri Dar es Salaam.
Alisema
kwamba kampuni yake iliamua kuwekeza UDA baada ya kutangazwa kubinafsishwa
kwake kwa sababu kampuni ya Simon Group Limited ilitaka kuleta mabadiliko yenye
maana katika mfumo wa usafiri katika Jiji la Biashara la Dar es Salaam hasa
katika mabasi ya abiria na usafirishaji kwa ujumla.
“Mpango
wa kuboresha usafiri umeelezwa vizuri katika mipango yetu ya muda mfupi na muda
mrefu inayoonyesha ni jinsi gani tuna mpango wa kusimamia mabadiliko haya hatua
kwa hatua. Katika mpango wetu pia tumebainisha ni vipi tunajipanga kuihusisha
Serikali na Jiji katika mpango mzima wa usafiri Dar es Salaam. Naamini hii ndio
maana hasa ya uzalendo, kufanya kazi na serikali yako ili kutoa huduma bora kwa
wananchi wake,’’ alieleza Kisena katika taarifa hiyo.
Katika
taarifa hiyo ofisa huyo mtendaji mkuu alibainisha kwamba mpango walioudhamiria
wa kampuni hiyo kuboresha huduma ya usafiri Dar es Salaam uko pale pale
ukihusisha mradi wa kuwa na mabasi zaidi ya 3,000 pamoja na mabasi mengine ya
kifahari 50 yenye viyoyozi na huduma ya internet.
Alisema
kwamba sambamba na mpango huo, kampuni itasimamia sera ya kuwaajiri wataalamu
wazawa badala ya kuwapa wataalamu wa kigeni kazi ambazo Watanzania wanazimudu.
“Kampuni
ya Simon Group Limited inamilikiwa na Watanzania, katika hilo nitakuwa mtu wa
mwisho kumkubali mtaalamu wa kigeni kuajiriwa katika nafasi ambayo
inaweza kushikwa na Watanzania wenzangu. Kama hatutopata mtaalamu Mtanzania,
tutaleta wataalamu wa kuwapa mafunzo Watanzania ili baadaye wazichukue nafasi
hizo. Kampuni yetu inalifanya hilo kama njia mojawapo ya kuwawezesha wazawa
kiuchumi na kuwapa utaalamu.
Alisema
kwamba tathmini inaonyesha kuwa ili kuwezesha mabasi yapatayo 3000 kufanya kazi
hapo baadaye wataalamu wapatao 7800 watahitaji kupewa mafunzo na kuajiriwa.
Aliongeza
kwamba mara baada ya mpango huo kukamilika, unyanyapaa miongoni mwa wanajamii
kuhusu utumiaji wa mabasi ya uma hautokuwepo tena na watu wataacha kupaki
magari yao katikati ya jiji, watanunua tiketi za UDA kwa njia ya mtandao jambo
ambalo litapunguza msongamano Dar es Salaam.
“Ninataka
kuwahakikishia Watanzania wote na wale wanaoendelea na kampeni zao kwamba
mpango wa UDA kuboresha mfumo wa usafiri Dar es Salaam ni jambo linalowezekana,
Tutafanya kazi kwa karibu na Serikali pamoja na Jiji ili kuona wakazi wa Dar es
Salaam wanapata huduma rahisi na ya uhakika ya usafiri,’’ alisema
No comments:
Post a Comment