Mkurugenzi wa Takwimu za
Jamii na Sensa ya Watu na Makazi, Bw. Ephraim Kwesigabo akizungumza na
waandishi wa habari jijini Dar es salaam Julai 08/2014, kuhusu kupungua kwa
mfumuko wa bei nchini.
XXXXXXXXXXXXXXXX
Na. Aron Msigwa – MAELEZO.
Dar es salaam.
Ofisi
ya Taifa ya Takwimu imeeleza kuwa mfumuko wa bei nchini kwa mwezi Juni 2014
umepungua ikilinganishwa na mwezi uliopita kutokana na kupungua kwa bei ya
bidhaa na huduma za jamii katika maeneo mbalimbali.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam
Mkurugenzi wa Takwimu za Jamii na sensa ya Watu na Makazi Bw. Ephraim Kwesigabo
amesema kuwa mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwezi Juni, 2014 umepungua na kufikia
asilimia 6.4 kutoka asilimia 6.5.
Amesema kasi ya upandaji wa bei za bidhaa na huduma mbalimbali kwa
mwezi Juni 2014 imepungua ikilinganishwa na ile iliyokuwepo mwezi
Mei kutokana na hali ya kupungua kwa bei kwenye bidhaa na
huduma
Ameeleza kuwa mfumuko wa bei za bidhaa za vyakula na
migahawa kwa mwezi Juni umeongezeka hadi asilimia 8.5 kutoka asilimia 7.9 za
mwezi Machi mwaka huu na kuongeza kuwa bei za bidhaa za vyakula na vinywaji
baridi imeongezeka hadi asilimia 7.8 kutoka asilimia 7.2 za mwezi uliopita huku
badiliko la fahirisi za bidhaa zisizo za vyakula likipungua hadi asilimia 4.9
kwa mwezi Aprili 2014 kutoka asilimia 7.2 iliyokuwepo mwezi uliopita.
Kwa upande wa mfumuko wa bei unaopimwa kwa kipimo cha mwezi
Bw. Kwesigabo amesema kuwa umepungua kwa asilimia 0.6 ikilinganishwa na
kupungua kwa asilimia 0.4 kama ilivyokuwa kwa mwezi Mei mwaka huu, huku
fahirisi za bei za taifa zikiongezeka hadi kufikia 148.98 kwa mwezi Juni 2014
kutoka 140.00 za mwezi Juni 2013.
Amezitaja bidhaa zilizochangia ongezeko la fahirisi za bei nchini
kuwa ni pamoja na mchele, mahindi,unga wa Muhogo, Viazi vitamu, dagaa,
matunda jamii ya machungwa,mbogamboga na vitunguu maji.
Kuhusu mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula zinazotumika nyumbani
na migahawani amefafanua kuwa kwa mwezi Juni umepungua hadi kufikia asilimia
8.7 kutoka asilimia 9.3
Aidha, amesema uwezo wa shilingi 100 ya Tanzania katika
kununua bidhaa na huduma za jamii kutoka mwezi Septemba 2010 hadi
Juni 2014 umeongezeka hadi shilingi 67 na senti 12 kutoka shilingi 66 na senti
72 za mwezi Mei mwaka huu.
“Kupungua kwa bei ya bidhaa kwa mwezi Juni kunamaanisha kwamba,
uwezo wa fedha yetu umeongezeka,hii inamaanisha mfumuko wa bei unaposhuka,
thamani ya shilingi nayo inapanda” Amesema.
Kuhusu ulinganifu mfumuko wa bei wa Tanzania na baadhi ya
nchi za Afrika Mashariki amesema kuwa una mwelekeo unaofanana na kueleza kuwa
mfumuko wa bei nchini Kenya umeongezeka na kufikia asilimia 7.39 kwa mwezi Juni
2014 ikilinganishwa na asilimia 7.30 za mwezi Mei , huku
Uganda ikiwa na mfumuko wa asilimia 4.9 kwa mwezi huu ikilinganishwa na 5.4 za
mwezi uliopita.
No comments:
Post a Comment