Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.
Mohammed Gharib Bilal, akihutubia katika Mkutano wa 20 wa Kimataifa kuhusu
Mabadiliko ya Tabianchi, unaoendelea Jijini Lima nchini Peru. Picha na OMR
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.
Mohammed Gharib Bilal jana Desemba 09, 2014 amemuwakilisha Rais Jakaya Mrisho
Kikwete ambaye ni Mwenyekiti Kamati ya Wakuu wa Nchi na Serikali Barani Afrika
kuhusu Mabadiliko ya Tabia Nchi, kwenye mkutano wa Kimataifa wa Mazingira Duniani
(Cop20) unaofanyika jijini Lima, Peru.
Pamoja na shughuli nyingine ambazo zimemuhusisha Mheshimiwa
Makamu wa Rais Dkt. Bilal katika Mkutano huo ikiwa pamoja na kuwa eneo la
Mazingira nchini liko chini ya Ofisi yake, Mheshimiwa Dkt, Bilal alipata fursa
ya kutoa hotuba kwa niaba ya Wakuu wa Nchi za Afrika siku ya Ufunguzi wa
Mkutano huo, huku akisisitiza katika hotuba hiyo umuhimu wa kila nchi kushiriki
katika kukabiliana na hali ya mabadiliko ya tabia nchi na tena akaelezea kuwa,
hakuna anayeweza kupona kwa kujificha ama kuachia kazi hii ifanywe na nchi
baadhi na akaongeza kuwa, wanaochangia kwa kasi kubwa kuathiri mazingira
wanatakiwa kutambua kwamba wanayoyafanya hayatawanufaisha milele hivyo nao
washiriki kwa vitendo katika kukabiliana na janga hili kubwa linaloikumba dunia
kwa sasa.
Awali akihutubia wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Katibu
Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon alieleza kuwa yapo mabadiliko ya tabia
nchi ambayo kimsingi yametengenezwa na binadamu wenyewe na kama binadamu
wakiamua kukabiliana nayo wanaweza kabisa kuyatokomeza. Pia alifafanua
kuhusu nadharia ya nchi kushirikiana kwa kuwa mabadiliko haya kwa sasa athari
zake hazina mipaka na kwamba nchi zote lazima ziwe katika sehemu ya utatuzi wa
tatizo hili kubwa linaloikabili dunia.
“Tutumie mapendekezo ya Lima kufungua njia mpya, tuwe na
vipaumbele vinavyotekelezeka na kuonekana, Tutoke hapa Lima na twende kuandika
historia mpya kwa dunia yetu,” alimalizia Ban Ki-moon.
Kwa upande wa Rais wa mkutano huo (Cop20) Manuel Pulgar-Vida
ambaye pia ni Waziri wa Mazuingira wa Peru, alitumia nafasi hiyo kuwakaribisha
washiriki wa mkutano huo nchini Peru kwa niaba ya Rais wa nchi hiyo Mheshimiwa
Olanta Humala na kisha akafafanua kuwa nchi ya Peru imepitia masaibu kadhaa ya
kimazingira na hivyo kupata nafasi ya kuandaa mkutano huu kwao ni heshima na
wajibu katika dunia na kwamba anategemea maazimio ya Lima yasaidie dunia katika
kukab iliana na tatizo hili linalokuwa la mabadiliko ya tabia nchi.
Kauli ya Mheshimiwa Manuel Pulgar inasadifu ile aliyoitoa
pia Christiana Fugueres, Katibu Mtendaji wa Umoja wa Mataifa wa Mkakati
wa kukabiliana na Mabadiliko ya Tabia Nchi ambaye aliuambia mkutano huo kuwa,
wakati umefika kwa nchi zote kukabiliana na matatizo ya mabadiliko ya tabia
nchi kwa pamoja kwa kuwa yanachangia kuongeza umaskini na ili jamii ipate
ahueni, basi ni wajibu kwa kila binadanmu kuchukua nafasi yake katika
kukabiliana na hali hii iliyopo.
Katika tukio jingine, Mheshimiwa Makamu wa Rais alipata
fursa ya kukutana na Ujumbe kutoka Marekani uliongozwa na Mjumbe Maalum kutoka
Serikali ya Marekani anayehusika na masuala ya Mabadiliko ya Tabia nchi Todd
Stern, ambaye alimueleza Mheshimiwa Makamu wa Rais kuhusu utayari wa serikali ya
Marekani katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi na kwamba
nchi yake itashirikiana nan chi zinazoendelea ikiwemo Tanzania katika suala
hilo.
Vile vile Mheshimiwa Makamu wa Rais alipata nafasi ya
kukutana na ujumbe kutoka Jamhuri ya Watu wa China ulioongozwa na Mheshimiwa
Xie Zhenhua ambaye alizungumzia kuhusu ushirikiano baina ya nchi zinazoendelea
na zile zilizoendelea katika suala la mabadiliko ya tabia nchi na akafafanua
kuwa Tanzania na China zina uhusiano wa kindugu hivyo kama kutakuwa na jambo la
kipekee baina ya nchi hizi mbili basi serikali ya China iko wazi kulipokea.
Mkutano huo pia umehudhuriwa na Rais wa Bolivia Evo Morales,
Rais wa Nauru Baron Waqa, Waziri Mkuu wa Tuvalu Enele Sopoaga, Rais wa Baraza
Kuu la Umoja wa Mataifa Sam Kutesa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban
Ki-Moon. Mkutano huu unafanyika wakati dunia ikiwa imeanza kubadili fikra na
misimamo kuhusu namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ambapo nchi
ambazo awali zilikuwa na misimamo mikali mfano Marekani na China sasa zimaeza
kubadili fikra kuhusu suala hili na kwa sasa zinaanza kulipa uzito kutokana na
athari yake pia kuzikabili nchi hizo.
Pamoja na Mheshimiwa Makamu wa Rais msafara wa Tanzia pia
unawashirikisha Mawaziri Bilinith Mahenge (Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa
Rais Mazingira) Waziri Fatma Fereji (Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa
Rais SMZ), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mahadhi
Juma Maalim pamoja na wataalam wengine wa masuala ya Mazingira na Maliasili pamoja
na wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Imetolewa na: Ofisi ya Makamu wa Rais
Lima, Peru Desemba 10, 2014
No comments:
Post a Comment