Tangazo

December 6, 2014

MAMA SALMA KIKWETE AFANYA KAMPENI KATIKA KATA ZA MTANDI NA MWENGE HUKO LINDI MJINI

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM anayewakilisha Lindi mjini na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akionyesha ishara ya vidole viwili kuashiria kuunga mkono pendekezo la muundo wa serikali mbili nchini wakati alipozungumza na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi wa Kata ya Mtandi tarehe 5.12.2014.PICHA/JOHN LUKUWI WA MAELEZO
XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX

Na Anna Nkinda – Lindi
  Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Lindi mjini wametakiwa kutokubali kurubuniwa kwa kitu chochote kile ili wawapigie kura wagombea wa vyama vya upinzani  bali  waungane kwa pamoja katika kampeni na kuhakikisha chama hicho kinapata ushindi wa kishindo.
Mwito huo umetolewa jana na  Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kupitia wilaya ya Lindi mjini Mama Salma Kikwete wakati akiwanadi kwa wananchi wagombea wa chama hicho wanaowania nafasi za uongozi kwenye uchaguzi wa Wenyeviti na Wajumbe wa Serikali za Mitaa katika Kata ya Mwenge.
Mama Kikwete ambaye ni Mke wa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alisema lengo la chama chochote cha Siasa ni kushika Dola kuanzia ngazi ya mtaa  hadi Taifa hivyo  basi wanachama hao wasikubali kurubuniwa bali waendelee kukitetea na kukipigania Chama chao ili kipate  ushindi katika mitaa yote 117 ya Kata hiyo.
“Viongozi wanaogombea tena wamechaguliwa kutokana na kazi yao nzuri. Nanyi ambao kura zeu hazikutosha wakati wa mchakato wa kuchagua msilaumu, bali muwapiganie  wagombea wote na kuhakikisha wanashinda angalieni maslahi ya chama kwanza  mambo binafsi baadaye”, alisema Mama Kikwete.
Aidha Mama Kikwete aliwaomba wananchi wa wilaya hiyo kutumia maarifa na ujuzi waliopewa na Mwenyezi Mungu wa kutambua mema na mabaya na kutokubali kudanganywa na kundi la watu wachache ili waipoteze amani yao.
Mama Kikwete alisema, “Wenzenu wamepiga hatua kubwa za maendeleo  katika mikoa yao huku Lindi Mwenyezi Mungu katupa neema maendeleo yanakuja sasa. Wanakuja huku kuwadanganya ili mfanye vurugu na kurudisha maendeleo yenu nyumba, msifuate mkumbo na kuchezea  amani kwani vurugu zinarudisha nyuma maendeleo”.
Aliwasihi wananchi waliohudhuria mkutano huo kuhakikisha watoto wao wanaenda shule ili wapate viongozi wazuri wa baadaye ambao watawaletea maendeleo kwani bila ya kuwa na elimu ni vigumu kupata maendeleo.
MNEC huyo pia aliwashukuru wanaume waliowaruhusu wake zao kugombea nafasi mbalimbali za uongozi na kuwapongeza wanawake kwa kutokukubali kubaki nyuma na kuomba kugombea nafasi hizo.

Mama Kikwete yupo wilayani humo kwa ajili ya shughuli za kichama ikiwa ni pamoja na kushiriki  kwenye kampeni na kuwanadi wagombea wa chama hicho wanaowania nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji  utakaofanyika tarehe 14 mwezi huu.

No comments: