Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw.
George Masaju (kushoto) akibadilishana mawazo na Waziri wa Katiba na Sheria
Dkt. Asha-Rose Migiro Jumatano, Januari 7, 2015, wakati alipofika Wizarani kwa
mara ya kwanza tangu ateuliwe na Rais jakaya Kikwete hivi karibuni.
XXXXXXXXXXXXX
Na Mwandishi Wetu
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. George Masaju
amewakumbusha watumishi wa umma katika sekta ya sheria kufanya kazi kwa
ushirikiano na uzalendo ili kulinda maslahi ya taifa.
Bw.
Masaju, ambaye ameteuliwa na kuapishwa hivi karibuni na Rais Jakaya Kikwete
kushika wadhifa huo, amefafanua kuwa watumishi wa umma wanapozingatia uzalendo
katika utendaji wao, wanapata nguvu ya kusimama na kukemea maovu.
Bw. Masaju ameyasema hayo leo (Jumatano, Januari 7,
2015) jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na viongozi wa Wizara ya Katiba
na Sheria alipokwenda kubadilishana nao mawazo.
“Sisi kama Wizara kwa ujumla wetu, tunapaswa kuwa
mfano wa uzalendo katika taifa hili ili tunaposimama mbele ya watu, tuwe na
nguvu kwa kuwa tupo safi,” amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye kabla ya
uteuzi huo, alikuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Akizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Katiba na
Sheria Dkt. Asha-Rose Migiro alimpongeza Bw. Masaju kwa heshima aliyopewa na
Rais Jakaya Kikwete na kuahidi kuwa yeye na Wizara itaendelea kumpa ushirikiano
wa kutosha katika kutekeleza majukumu yake.
“Tunakupongeza kwa heshima kubwa uliyopewa na
Mheshimiwa Rais na sisi kama wasimamizi wa sera, tutaendelea kutoa ushirikiano
kwako kama tulivyofanya kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliyetangulia,”
alisema Waziri Migiro.
Aidha, Waziri Migiro aliahidi kuongeza ushirikiano
katika kuimarisha kada ya Mawakili wa Serikali pamoja na watumishi wengine ili
kuongeza ufanisi katika utoaji haki.
Bw. Masaju aliteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa
Serikali tarehe 2 Januari mwaka huu na kuapishwa tarehe 5 Januari. Kabla ya
uteuzi huo, alikuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Aidha, Bw. Masaju
amewahi kuwa Mshauri wa Sheria wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
No comments:
Post a Comment