Tangazo

February 9, 2015

NAPE: CCM HAIWEZI POTEZA HISTORIA YA TANU


Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi CCM Taifa akizungumza kwenye ofisi ya gazeti la Jambo leo ikiwa sehemu ya ziara yake kwenye vyombo vya habari.

Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi Ndg. Nape Nnauye amesema CCM haiwezi na wala haina mpango wa  kupoteza historia ya mahali ilipozaliwa TANU.


Ameyasema hayo wakati akizungumza na wahariri wa gazeti la JamboLeo siku ya Ijumaa tarehe 6 februari 2015 alipotembelea ofisini kwao katika ziara ya kutembelea vyombo mbalimbali vya habari nchini. 

Alisema kumekuwa na maneno mengi kama vile ukarabati unaofanywa kwenye ofisi ndogo ya CCM Lumumba ni kupoteza historia ya TANU.

Alisema kinachofanyika ni maboresho ya ofisi ndogo ya CCM Lumumba ifanane na hadhi, mahitaji na wakati wa Chama hicho, lakini historia itabaki kama kielelezo cha Mahala ilipozaliwa TANU.

Alifafanua kuwa awali ofisi ya mwanzo ilikuwa nyumba ya udongo iliyoezekwa kwa makuti, kisha ikaondolewa makuti na kuezekwa mabati ya madebe,baade ikabadilishwa na kuwekwa bati za kisasa.

“Historia ya TANU iliyopo kwenye jengo la Lumumba, tutaendelea kuitunza na hatutoibomoa kwani ni kielelezo cha tulikotoka na tunajivunia historia hiyo, tutaitunza”

Alisema kama tusingefanya maboresho maana yake tungekuwa na jengo la udongo ambalo limeezekwa makuti mpaka leo. Akadai wanaolalamika hawajui historia ya eneo hilo, ila akawashukuru kwa mapenzi yao mema kwa Chama hicho.

Aliongeza kuwa hakuna namna CCM itaruhusu historia ifutike na huku ikiendelea kuhifadhi historia za vyama vingine, hasa bile vya ukombozi kusini mwa bara la Afrika. 

Nape pia alikanusha uvumi kuwa CCM inawekeza kitega uchumi eneo hilo, akasema wanakarabati ofisi na itakuwa ofisi sio kitega uchumi.

No comments: