Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi, Abdulrahmani Kaniki
(kushoto) akiwasili katika chuo cha Polisi Moshi (CCP) wakati alipokuwa katika
ziara ya kikazi kukagua mafunzo yanayoendelea chuoni hapo.Katikati ni Mkuu wa
Chuo hicho, Kamishna msaidizi mwandamizi wa Polisi (SACP) Matanga Mbushi na
Mkuu wa Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Naibu Kamishna Omar Rashid (Picha na Frank
Geofray wa Jeshi la Polisi)
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Na Frank Geofray-Jeshi la Polisi, Moshi.
Wakufunzi wa Chuo cha Polisi
Moshi (CCP) wametakiwa kuendelea kutoa mafunzo kwa weledi ili kuweza kupata
askari bora ambao watashirikiana na jamii katika kupambana na uhalifu hasa
katika kipindi hiki ambapo kumeibuka uhalifu mpya kwa njia ya mitandao na
unaovuka mipaka.
Wito huo umetolewa jana mjini
moshi na Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi, Abdulrahman Kaniki wakati
alipokuwa katika ziara ya kikazi chuoni hapo ambapo alizungumza na wakufunzi
hao na kuweka mikakati mbalilmbali ya kuboresha mafunzo katika chuo hicho.
Naibu IGP Kaniki alisema,
askari wakipata mafunzo bora wataongeza mbinu zitakazowezesha kukabiliana
na uhalifu huo na hivyo kuendelea kuimarisha usalama wa raia na mali zao
kwa kushirikiana na jamii ambayo imekuwa msaada mkubwa wa kutoa taarifa za
uhalifu na wahalifu.
“Ili kuhakikisha kwamba raia
wa Tanzania na mali zao wanalindwa ipasavyo, Jeshi la Polisi hatuna budi
kuendelea kubuni mbinu mpya za kukabiliana na uhalifu wa kila aina unaobadilika
mara kwa mara na hilo linawezekana kwa kuendelea kuwapatia askari wetu mafunzo
yenye viwango vya kupambana na uhalifu unaokua kwa kasi”alisema Kaniki.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo
cha Polisi moshi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Matanga Mbushi
alisema wanaendelea na juhudi za kuhakikisha kuwa mafunzo wanayotoa yanalenga
katika mitaala ambayo wamekuwa wakiiboresha mara kwa mara ili kuendana na
wakati kulingana na mazingira ya uhalifu unaotokea katika jamii.
Alisema, mbinu za uhalifu
zimekuwa zikibadilika kila siku hivyo, na wao kama chuo wamejikita kuhakikisha
kuwa askari wanaopita katika chuo hicho wanazipata mbinu mpya na hivyo kuwa
zaidi ya wahalifu ili waweze kupambana nao.
No comments:
Post a Comment