Bw. Cosmas Mwaisobwa (katikati), Mkurugenzi
Msaidizi (Habari, Elimu na Mawasiliano) wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu
ya Juu (HESLB) akiongea na wanahabari jijini Dar es Salaam leo (Ijumaa, Agosti
14, 2015). Wengine ni Bw. Omega Ngole, Meneja kutoka HESLB na Bi. Fatma Salum (kulia),
Afisa Habari kutoka Idara ya Habari (MAELEZO). Picha na HESLB.
--------
Na Mwandishi
Wetu
Idadi ya
wanafunzi wanaopata mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu
(HESLB) imeongezeka kutoka 42,729 mwaka 2005/200 wakati Bodi hiyo ilipoanza
kazi hadi kufikia wanafunzi 98,000 kwa mwaka katika mwaka wa masomo 2014/2015.
Akizungumza na
waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo (Ijumaa, Agosti 14, 2015),
Mkurugenzi Msaidizi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa Bodi hiyo Bw. Cosmas
Mwaisobwa amesema ongezeko hilo limetokana na Serikali kuongeza fedha za bajeti
ya ukopeshaji wanafunzi inayotolewa kwa Bodi hiyo.
Mafanikio
“Katika
kipindi hicho cha miaka 10 ya uhai wa Bodi, bajeti ya fedha za mikopo
zinazotolewa kwa wanafunzi imeongezeka kutoka Tshs 56.1 bilioni mwaka 2005/2006
hadi kufikia Tshs 345 katika mwaka wa fedha uliopita (2014/2015) na hivyo
kuwezesha kuwakopesha wanafunzi hao,” amesema.
Bw. Mwaisobwa
alikuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na changamoto
katika utekelezaji wajukumu ya Bodi hiyo katika kipindi cha miaka 10 ya uhai
wake.
Akizungumzia
urejeshaji wa mikopo iliyotolewa, Bw. Mwasobwa amesema HESLB imepata mafanikio
makubwa kwa kuongeza kasi na kiasi cha fedha zinazokusanywa kama madeni kutoka
kwa wanufaika.
“Katika
kukusanya madeni nako tumepiga hatua kubwa kwani mwaka 2006/2007, tulikusanya
Tshs 53.6 milioni tu lakini katika mwaka wa fedha uliopita pekee, tumekusanya
Tshs 74.7 bilioni, hii ni hatua kubwa na inaiwezesha Serikali kukopesha
wanafunzi wengi zaidi,” amesema.
Kwa mujibu wa
Mkurugenzi Msaidizi huyo, ingawa HESLB ilianza kazi rasmi mwaka 2005, lakini
sheria iliyoanzisha Bodi imeipa jukumu la kukusanya madeni ya mikopo ya
wanafunzi iliyoanza kutolewa na serikali tangu mwaka 1994/1995 – kazi ambayo
Bodi inaendelea nayo.
Mafanikio
mengine aliyoyataja Bw. Mwaisobwa ni pamoja na kusogeza huduma karibu na wateja
wa Bodi kwa kufungua ofisi nne za kanda katika mikoa ya Dodoma mwaka 2009;
Mwanza (2014); Arusha (2015) na Zanzibar iliyofunguliwa mwaka 2011. Aidha,
ameongeza kuwa idadi ya watumishi wa Bodi imeongezeka kutoka tisa mwaka 2005
hadi kufikia 135 hivi sasa.
Katika
kipindi cha miaka 10 iliyopita, HESLB imeboresha utoaji wa huduma zake kwa
kuanzisha utaratibu mpya wa kuomba mikopo kwa njia ya mtandao yaani ‘Online
Loan Application and Management System (OLAMS)’. Kupitia mfumo huu,
waombaji wa mikopo wanaweza kuingia katika mtandao wa Bodi (www.olas.heslb.go.tz),
kujaza fomu ya maombi na kuwasilisha fomu zao kwa njia ya mtandao kutoka popote
walipo.
Changamoto
Pamoja na
mafanikio hayo, kwa mujibu wa Bw. Mwaisobwa, Bodi ya Mikopo imekumbana na
changamoto kadhaa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita. Amezitaja changamoto
hizo kuwa ni pamoja na kutokubalika ipasavyo kwa Sera ya Uchangiaji wa gharama
za elimu ya juu na imani potofu kwamba mikopo inayotolewa na Bodi ni ruzuku na
kwamba haipaswi kurejeshwa.
“Kuhusu hili
la sera ya uchangiaji, kuna wananchi wanachangia huduma nyingine za kijamii,
lakini kuchangia elimu hawataki...na kuhusu hili la imani potofu, kuna watu
wenye uwezo wa kujigharamia elimu ya juu lakini wanaomba wakidhani ni ruzuku,”
amefafanua Bw. Mwaisobwa na kuongeza kuwa changamoto nyingine kubwa ni baadhi
ya wajiri kutotimiza wajibu wao wa kisheria wa kuwatambua na kuwasilisha
taarifa za wanufaika wa mikopo kwa HESLB.
Hata hivyo,
Bw. Mwaisobwa amesema Bodi itaendelea kujenga ushirikiano na kuwaelimisha
waajiri na umma kwa ujumla kuhusu umuhimu wa kushirikiana na Bodi katika zoezi
la kurejesha Mikopo na utekelezaji wa majukumu mengine.
Bodi ya
Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) ni taasisi ya Serikali
iliyoanzishwa kwa mujibu wa Sheria Na. 9 ya mwaka 2004 na kuanza kazi rasmi
mwezi Julai, 2005. Pamoja na majukumu mengine, ina wajibu wa kutoa mikopo kwa
wanafunzi wahitaji; na kukusanya mikopo kutoka kwa wanufaika wa mikopo hiyo ili
kuufanya mfuko wa mikopo ya elimu ya juu kuwa endelevu.
No comments:
Post a Comment