Tangazo

July 21, 2016

MAN UTD DORTMUND KUFUNGUA PAZIA LA MICHUANO YA ICC ITAKAYOONEKANA KUPITIA STARTIMES




 Na Dotto Mwaibale

 IKIWA chini ya kocha wake mpya Mreno, Jose Mourinho, Manchester United wanatarajia kushuka dimbani jijini Shanghai, China kuwakabili Borrusia Dortmund siku ya Ijumaa Julai 22, 2016 mechi itakayopigwa saa tisa za alasiri kwa saa za hapa nyumbani kupitia ving’amuzi vya StarTimes.

Akizungumzia juu ya habari hiyo njema kwa wapenda soka nchini Makamu wa Rais wa StarTimes Tanzania, Bi. Zuhura Hanif amebainisha kuwa michuano hiyo itakuwa ni ya kusisimua kutokana na orodha ndefu ya timu kubwa zitakazoshiriki kama vile Real Madrid, Barcelona, Manchester United, Manchester City, Paris Saint-Germain, Juventus, Liverpool, Chelsea na Bayern Munich kwa uchache.

“Tunayofuraha kuwatangazia wateja wetu na watanzania kwa ujumla kuwa watapata fursa ya kutazama timu zao katika mechi za awali kabla ya kuanza kwa ligi kuu mbalimbali duniani kupitia ving’amuzi vya StarTimes pekee. Mechi zote za michuano ya ICC itaonekana moja kwa moja kupitia chaneli ya World Football inayopatikana katika kifurushi cha Mambo kwa malipo ya shilingi 12000/- tu kwa mwezi. Michezo yote itakuwa ni yenye msisimko mkubwa kwani timu zinazoshiriki ni kubwa, nyingi zikiwa ni mabingwa katika ligi kuu zao, zina wachezaji nyota na kikubwa zaidi zingine hazikuwahi kukutana kabla.” Alisema Bi. Hanif

“Hii ni fursa ya pekee kwa watanzania kwani tunafahamu ya kuwa ni wapenzi wakubwa wa mchezo huu na siku zote StarTimes tunajitahidi kuwapatia kile wanachokipenda. Hii ni mara ya pili tunaonyesha moja kwa moja michuano hii kwani mwaka jana tulifanya hivyo ambapo timu ya Real Madrid waliibuka mabingwa. Hivyo basi mashabiki watakuwa na shauku kubwa ya kujua ni timu gani itakayoibuka mabingwa au kama utarudi kwa Real Madrid,” alisema na kumalizia Bi. Hanif kuwa, “Ni wajibu wetu kuhakikisha wanafikiwa na matangazo ya vipindi vizuri na kusisimua kama hivi kwa ubora wa hali ya juu na gharama nafuu ambazo kila mtu atazimudu.”

Mchezo huo ni sehemu ya ufunguzi wa michuano ya kombe la mabingwa wa kimataifa almaarufu kama International Champions Cup au ICC itakayoanza kutimua vumbi Julai 22 na kumalizika Agosti 13, 2016 katika viwanja mbalimbali nchini Marekani, Ulaya, Australia na China.

Katika michuano hii wapenzi wa soka duniani watapat fursa kujionea kwa mara kwanza mechi ya watani wa jadi kutoka jiji la Manchester au unavyojulikana kama ‘Machester Derby’ miongoni mwa mashabiki wengi. Mechi hiyo itapigwa siku ya Jumatatu ya Julai 25 jijini Beijing, China.

Mchezo huo utanogeshwa si tu na ushindani baina ya wachezaji au mashabiki bali safari hii ni makocha waliopewa vibarua vya kunoa vikosi hivyo, Jose Mourinho wa Manchester United na Pep Guardiola wa Manchester City.

Ukiachana na mechi hiyo, pia macho ya mashabiki wengi yatakuwa yakisubiria kwa hamu kutazama mechi kali zitakazozikutanisha timu za, Real Madrid na  PSG,  Chelsea na Liverpool, Real Madrid na Chelsea, Bayern Munich na Real Madrid pamoja na Liverpool na Barcelona.

Kwa ujumla timu zitazoshiriki  michuano hii ni pamoja na Real Madrid, Barcelona, Manchester United, Manchester City, Paris Saint-Germain (PSG), Juventus, Liverpool, Chelsea, Bayern Munich, Liverpool, Tottenham Hotspurs, AC Millan, Inter Millan, Leicester City FC, Celtic FC, Atletico Madrid, Melbourne Victoria na South China.

No comments: