Amir Mhando |
KONGAMANO kuhusu mifumo ya kiuendeshaji ambayo klabu kongwe nchini za Simba na Yanga zipo mbioni kuingia litafanyika Jumamosi Oktoba 22 mwaka huu ukumbi wa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na litarushwa live (mubashara) na kituo cha televisheni cha Azam.
Kongamano hilo limeandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), likiwa na lengo la kupata maoni ya kitaalamu kuhusu mifumo hiyo, ambapo Simba ipo mbioni kuingia mambo ya hisa, wakati Yanga utaratibu wa kukodishwa.
Kongamano halina nia ya kuzuia mabadiliko au kuharakisha mabadiliko katika klabu hizo, badala yake inataka litumike kutoa elimu ya kutosha kwa wadau wa mpira wa miguu kuhusu mifumo hiyo na aina nyingine ya mifumo ya uendeshaji wa klabu duniani, hivyo kusaidia kujibu maswali mbalimbali ambayo pengine hayajibiwi ipasavyo.
Baadhi ya mambo yatakayozungumziwa ni umuhimu wa mabadiliko katika klabu hizo, pia harakati za kuzibadili zilivyoanza miaka ya nyuma na matokeo yake na itazungumziwa pia mifumo ya uendeshaji ya klabu mbalimbali duniani.
Lengo ni kujadili kitaalamu bila ushabiki wa namna yoyote kwani nia ni kujenga na kuimarisha soka na michezo kwa ujumla hapa nchini na ndiyo sababu tumealika wataalamu wa kada mbalimbali, viongozi wa zamani wa soka kwa tofauti na baadhi ya wadau wa soka.
Tunaomba mashabiki na wadau wengine mbao hawakualikwa watambue tunathamini mawazo yao, lakini nafasi ya wanaotakiwa kuhudhuria ni chache hivyo wafuatilie kupitia vyombo vya habari.
Nawasilisha,
Amir Mhando
Katibu Mkuu TASWA
20/10/2016
No comments:
Post a Comment