Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu
Hassan akizungumza na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA)
Bw. Charles Kichere (kushoto) aliyemtembelea leo ofisini kwake, Ikulu
jijini Dar es Salaam.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu
Hassan akizungumza na Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Charles Kichere
(kushoto)ambaye aliongozana na Mkurugenzi wa Elimu ya Mlipa Kodi TRA Bw.
Richard Kayombo (kushoto), Ikulu jijini Dar es Salaam.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu
Hassan akizungumza na Afisa Mahusiano Mwandamizi wa Mamlaka ya Mapato (TRA)Tanzania Bi. Mariamu Mwayela mara baada ya kumaliza mazungumzo yake na Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo Bw. Charles Kichere.
...........................................................
Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan amemwagiza Kamishna
Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Charles Kichere ahakikishe anaweka
utaratibu wa kukutana na wafanyabiashara mara kwa mara kama njia ya kujadili na
kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wafanyabiashara hao.
Makamu wa
Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amesema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Charles Kichere kuhusu namna
bora ya kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wafanyabiashara nchini kama
hatua ya kuongeza kasi ya ukusanyaji wa kodi wa kwa ajili ya maendeleo ya
Taifa.
Makamu wa Rais
ameonyesha kusikitishwa na baadhi ya Maafisa wa TRA kuwanyanyasa
wafanyabiashara na wengine kuwabambikizia kodi kubwa hali ambayo inazua
malalamiko mengi kutoka kwa wafanyabiashara hao jambo ambalo amesema ni muhimu
likatafutiwa ufumbuzi haraka iwezekanavyo.
Amesisitiza
kuwa ni muhimu kama TRA itafanya mabadiliko yeyote ya ulipaji wa kodi ikawafahamisha
wafanyabiashara hao mapema ili kuondoa usumbufu mkubwa unaoweza kutokea katika
ulipaji wa kodi pindi wanapoagiza bidhaa mbalimbali kutoka nje ya nchi.
Makamu wa
Rais amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha ulipaji wa kodi kwa ajili ya
maendeleo ya Taifa unafanyika kwa kuzingatia kanuni, sheria na taratibu na sio
kuwakandamiza Watanzania kwa kuwalipiza kodi mara mbili jambo ambalo amesema
halifai hata kidogo.
Makamu wa
Rais amemtaka Kamishna wa TRA kukomesha mara Moja tabia ya baadhi ya Maafisa wa
mamlaka hiyo kutoa lugha chafu na kuudhi kwa wafanyabiashara bali watumie lugha
nzuri ili kuhamasisha wafanyabiashara kulipa kodi kwa hiyari bila kulazimishwa
na mtu.
Makamu wa
Rais pia ameipongeza TRA kwa kazi kubwa inayoifanya katika ukusanyaji wa mapato
na amewapa moyo wa kuongeza bidii katika ukusanyaji wa kodi hizo ambazo Serikali
inatumia katika ujenzi wa miundombinu mbalimbali nchini.
Kwa upande wake, Kamishna Mkuu wa TRA nchini Charles
Kichere amemuahidi Makamu wa Rais kuwa atafanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha
malalamiko mbalimbali yanayotolewa na Wafanyabiashara yanapata ufumbuzi haraka
iwezekanavyo.
Kamishna
Kichere amesisitiza kuwa kwa baadhi ya maafisa wa Mamlaka hiyo wanaokiuka maadili
ya kazi ataendelea kuwachukulia hatua stahiki ili kurejesha nidhamu katika utendaji
wa kazi na ukusanyaji wa mapato.
No comments:
Post a Comment