Mkuu wa Wilaya ya Ikungi mkoani
Singida, Mhe.Miraji Mtaturu ametoa onyo kali kwa bodi ya uongozi wa Chama cha
Ushirika cha wachimbaji wadogo wa dhahabu cha Aminika kilichopo kijiji cha Mang’onyi
wilayani humo kutokana na kuendesha chama hicho kiholela.
Mhe.Mtaturu alitoa onyo hilo jana
Agosti 18,2017, alipokutana na wanachama pamoja na uongozi wa chama hicho
kufuatia malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa wanachama.
Awali Katibu wa chama hicho, Ally
Nkingi alisema baada ya chama kupokea fedha hizo kilinunua mashine (compressor)
kwa ajili ya shughuli za uchimbaji iliyogharimu zaidi ya shilingi Milioni 30,
milioni 41 zikalipa madeni, milioni kumi zikatumika kulipia leseni ya uchimbaji
na milioni 15 zikatumika kwa ajili ya ununuzi wa mafuta, baruti, kusafirisha
mashine kutoka Dar es salaam na uendeshaji wa kambi.
Baadhi ya wanachama wa chama hicho walieleza
kwamba hawajawahi kusomewa mapato na matumizi kwa kipindi cha miaka mitatu na
kwamba hawajui pesa walizosaidiwa na serikali pamoja na mwekezaji kutoka kampuni
ya Shanta Gold Mining zimefanya kazi gani.
“Miaka mitatu hatujawahi kukaa na bodi
yetu kuelezwa taarifa ya mapato na matumizi ya fedha zetu. Tunasikia tu imenunuliwa
mashine (Compressor) lakini sisi hatujawahi kuiona na tunaambiwa huwa
inakodishwa lakini fedha zake hatuzioni, tukiwauliza viongozi wanakuwa wakali”.
Alieleza Bi.Patrice Petro.
Wanachama wengine ambao ni pamoja na
mzee Masoud Hassan, Florentina Yohana na Anna Petro walisema uongozi uliopo
madarakani unawapeleka shimoni kwani maisha yao ya uchimbaji yamekuwa magumu
kutokana na kukosa vifaa kwa ajili ya uchimbaji hivyo wanaomba serikali
iwasaidie wapate ripoti ya utafiti wa madini katika eneo la Mang’onyi kwa ajili
ya kuingia makubaliano na mwekezaji ambaye alisema baada ya ripoti hiyo kutoka na
kubaini kiwango cha dhahabu kilichopo atatoa vifaa kwa ajili ya uchimbaji na
faida itakayopatikana watagawana.
Baada ya maelezo hayo, Mhe.Mtaturu
alimwagiza Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kati, Sosthenes Massola
kuhakikisha ripoti hiyo inapatikana katika kipindi kisichozidi wiki mbili huku
akimtaka Afisa Ushirika Gurisha Msemo kuhakikisha anasimamia vyema ushirika huo
ikiwemo kufanya uchaguzi wa uongozi kwani kwa mjibu wa katiba, muda wa ushirika
huo kufanya uchaguzi umewadia.
Mwenyekiti wa bodi ya Chama cha
Ushirika Aminika Mang’oni, Francis Mbassa awali hakuwa wazi kukiri malalamiko
juu ya uongozi wake na baada ya DC Mtaturu kumuonya kuacha tabia hiyo akakiri
kuwepo kwa baadhi ya mapungufu ya kiuongozi na kuahidi kumaliza mvutano uliopo
ikiwemo kuitisha mkutano wa wanachama kwa ajili ya uchaguzi kwani muda wa
uongozi uliopo madarakani umekwisha.
Tazama video hapo chini
Mkuu wa wilaya ya Ikungi, Mhe.Miraji Mtaturu akizungumza kwenye mkutano huo
Mwenyekiti wa bodi ya Chama cha Ushirika Aminika Mang’oni, Francis Mbassa (aliyesimama), akijitetea kwenye mkutano huo
Katibu wa Chama cha Ushirika Aminika, Ally Nkingi, akisoma taarifa fupi mbele ya DC Ikungi
Afisa Ushirika wilayani Ikungi, Gurisha Msemo, akitoa maelezo kuhusiana na Chama cha Ushirika Aminika ambapo alisema muda wa bodi kuendelea kuwa madarakani umeisha na kwamba amekwisha toa fomu kwa ajili ya chama hicho kufanya uchaguzi ingawa fomu hizo bado hazijarejeshwa
Baadhi ya wachimbaji wadogo wa dhahabu wanaounda Chama cha Ushirika Aminika kilichopo Mang'onyi wilayani Ikungi. Mwenye miwani ni mwakilishi wa kampuni ya madini ya Shanta Gold Mining
Wanachama wa Chama cha Ushirika Aminika wakiwasilisha kero zao mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Ikungi
Mkuu wa wilaya ya Ikungi, Mhe.Miraji Mtaturu (wa pili kushoto) akiwasili eneo la mkutano.
BMG Habari
No comments:
Post a Comment