Na Jumia Travel Tanzania
Ni hali ya kawaida kujisikia hali ya uchovu mahala pako pa kazi hususani baada ya kurudi kutoka likizo au mapumziko. Na inawezekana bado miongoni mwa wafanyakazi wenzako hawajarudi kutoka mapumzikoni. Achilia mbali bado kusikia salamu za, “likizo yako ilikuaje?” Au “Natumaini ulikuwa na mapumziko mema,” zikitawala kila unapokutana na watu.
Endapo unajisikia mwili na akili ni vizito kuanza na majukumu ya mwaka huu mpya basi kuna uwezekano mkubwa hizo ni dalili za uchovu wa likizo. Na ukweli ni kwamba haupo peke yako, ni hali ya kawaida ambayo watu wengi hupitia kipindi kama hiki sehemu tofauti duniani.
Changamoto ni kwamba watu wengi huwa hawajijui kama bado wana uchovu wa likizo au mpaka waje kugundua inakuwa ni muda mrefu umepita. Jumia Travel ingependa kukushirikisha mambo yafuatayo ambayo ni dhahiri kwamba bado una uchovu wa likizo na namna yakukabiliana nao.
Akili yako. Endapo kumbukumbu za matukio uliyoyafanya kipindi cha mapumziko bado zinajirudia mara kwa mara basi ujue ni dalili upo kwenye uchovu wa likizo.
Nguvu yako. Endapo mwili bado unajisikia uchovu, kwa maneno mengine tunaweza kusema kwamba kila unachotaka kukifanya unakuwa ni mzito kufanya hivyo, basi ujue una uchovu wa likizo.
Hali yako. Kuna wakati unakuwa na ari ya kufanya kazi iliyopo mbele yako lakini kila ukijitahidi kuanza inakuwa ni vigumu akili yako kuwa makini. Hii ni dalili nyingine kwamba bado una uchovu wa likizo.
Usingizi wako. Kipindi cha mapumziko ilikuwa ni vigumu kulala kwa wakati kwani haukuwa na hofu ya kuwa na majukumu siku inayofuatia. Hivyo ulikuwa unalala muda wowote unaotaka na kwa kiwango chochote ulichokitaka. Lakini sasa itabidi kulala kwa wakati na kuamka muda ambao utakufanya uwahi kwenye shughuli zako ipasavyo. Kama unajisikia usingizi unaupata kwa tabu au haupati usingizi ndani ya muda muafaka basi hiyo ni dalili nyingine ya uchovu wa likizo.
Hamu yako ya kula. Kipindi cha likizo watu wengi huwa hawazingatii ratiba ya kula au aina ya vyakula wanavyokula. Kwa sababu huwa ni kipindi ambacho tunaupumzisha mwili na akili kutokana na pilikapilika za mwaka mzima, suala la kuzingatia vyakula vya kula huwa halipo. Endapo bado haujisikii kula chochote au aina fulani ya vyakula basi ujue hali ya kujisikia bado upo mapumzikoni haijatoka mwilini na akilini mwako.
Dalili zote hizo hapo juu ni kwamba bado unakabiliana na uchovu wa likizo ambao ni vigumu kuondoka mwilini na akilini mwako kwa haraka kama unavyotarajia. Umefikia wakati sasa wa kuondokana na hali hiyo ili uendelee na majukumu yako kama kawaida kwani kipindi cha mapumziko kimekwishapita.
Namna ya kurudia hali yako ya kawaida.
Fuatilia kwa karibu mienendo yako ya sasa. Inawezekana kwamba ulikuwa na wakati mzuri kipindi cha likizo, moyo na akili yako bado unakukumbusha namna ilivyokuwa. Suluhu ni kubadili ratiba ya shughuli ulizozifanya ili kuendana na shughuli ulizonazo kwa sasa.
Fanya mazoezi. Mbinu nyingine itakayokusaidia zaidi ni kwa kufanya mazoezi mepesi aidha ya viungo au hata kutembea jioni mara baada ya kazi. Mazoezi huufanya mwili na akili kuondokana na uchovu na kuupatia ari na nguvu mpya ya kufanya mambo mengi kwa ufanisi zaidi.
Hakikisha unazingatia mlo wenye afya na usingizi wa kutosha. Ni wakati sasa wa kurudi kwenye ratiba ya mlo wenye afya kama ilivyokuwa awali. Kwani inaaminika kwamba namna pekee ya kuufanya mwili na akili yako kujisikia vizuri ni kupitia mlo wenye afya na usingizi wa kutosha. Kujinyima usingizi wa kutosha ni sawa na kujipatia mateso bila ya kujijua. Kwa hiyo, acha kujitesa!
Mshirikishe rafiki au mtu wako wa karibu namna unavyojisikia. Hii hali haikutokei wewe peke yako bali ni watu wengi. Hivyo basi, kwa kumshirikisha mtu wako wa karibu inaweza kuwa ni tiba mbadala. Huwezi kufahamu atakuwa na ushauri wa aina gani ili kukusaidia kuishinda hiyo hali.
Jumia Travel inaamini kwamba lazima utakuwa na mtu wako wa karibu ambaye unaelewana naye, anakufahamu vya kutosha na kamwe hatosita kukusaidia pale unapohitaji msaada katika kujinasua na hali kama hii. Kushindwa kufanya hivyo kunaweza kukuhatarishia shughuli zako kutoenda sawa na kukupoteza fursa mbele yako bila ya kujijua.
No comments:
Post a Comment