Tangazo

August 11, 2011

BONGO MOVIE VS TAFF: Ukimya wa Serikali kuhusu mgogoro huu unatia shaka

Kiongozi wa Kundi la Bongo Movie, Jacob Steven 'JB'
NI wazi kuwa mgawanyiko uliopo wa wasanii na wadau wa tasnia ya filamu nchini kati ya kundi la Bongo Movie Club na Shirikisho la Filamu Tanzani (TAFF), umezidi kukua huku kila kundi likipanga mbinu mbalimbali ili kulidhibiti kundi jingine. Kundi moja kwa kusaidiwa na mfadhili wao wamekuja na mpango wa kupandikiza chuki kati ya wasanii wa filamu na kiongozi wao.

Katika muda wote tangu kuanza kwa mtafaruku wa makundi haya mawili serikali imeonekana kuwa kimya pamoja na kwamba Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Emmanuel Nchimbi, wakati fulani kukiri kuwepo matatizo ya kutoelewana kwa wasanii wa filamu hapa nchini, hali ambayo inarudisha nyuma maendeleo ya sanaa.

Nchimbi ambaye aliwataka wasanii wa filamu kumaliza tofauti zao na kuwa na mshikamano na umoja ili waimarishe na kuboresha kazi zao za sanaa, siku Bongo Movie Club walipozuru Bungeni Dodoma, walikokwenda kucheza mechi ya kirafiki na timu ya wabunge, Bunge Sports Club. Lakini imeonekana kauli yake ni kama iliingilia sikio la moja na kutokea sikio jingine.

Katika hili Serikali inapaswa itangaze maslahi yake vinginevyo haitaeleweka na hali hii inaanza kuibua chuki miongoni mwa wasanii na serikali yao, kwa kudhani kuwa imeamua kulibeba kundi mojawapo. Serikali inapaswa ikemee mtafaruku huu na iwasaidie wasanii kuharakisha kufanya marekebisho si katika sheria tu, bali na taasisi zilizoundwa kwa lengo la kuwasaidia wasanii kusonga mbele kikazi na kimapato.

Tunajua zipo taasisi zilizo chini ya serikali zenye dhamana ya sanaa kama Basata, Cosota na kadhalika, ambazo dhamira kubwa ya kuwapo kwao ni kuhakikisha mambo yanakwenda vema.

Nimekuwa nikijiuliza maswali kadhaa: ikiwa sheria ya kulinda haki za wasanii ipo nini kasoro yake? Kwa nini wasanii waendelee kulia kuibiwa haki zao? Na inakuwaje kuwapo na ulazima wa kuwa na sheria kali zaidi kuliko sasa? Sheria ya sasa na hiyo inayofikiriwa itafanya kazi vipi katika dunia yenye njia mbalimbali za mawasiliano?

Siyo siri kwa sasa mtafaruku kati ya makundi haya mawili umezidi kukua na kama hatua madhubuti hazitachukuliwa tunaweza kushuhudia amani ikitoweka kwani baadhi ya wahusika katika sakata hili wameanza kutishiwa maisha, na habari za kuaminika kutoka kwenye chanzo kimoja zimelipasha gazeti hili kuwa kampuni ya usambazaji wa filamu nchini ya Steps Entertainment ndiyo inayofadhili mpango wa kuleta mgawanyiko huu japo yenyewe inakana.

Wiki iliyopita kulikuwa na kikao rasmi cha kuandaa mpango kabambe wa kumfitinisha Mwakifwamba na wasanii, kufuatia tukio la Jumatatu wiki iliyopita kwenye Jukwaa la Sanaa linaloandaliwa na Basata, ambapo wasanii wa filamu walio watiifu kwa Shirikisho la Filamu chini ya Mwakifwamba, walipotoa malalamiko dhidi ya Steps na hatimaye kuanzisha vurugu zilizomkumba Katibu Mtendaji wa Basata, Ghonche Materego kwa kuonekana kuibeba kampuni ya Steps.

Mpango ulioandaliwa na kundi la Bongo Movie ni pamoja na kuvitumia vyombo vya habari kumfitinisha kiongozi huyo wa TAFF na wadau wa tasnia ya filamu. Na tayari kuna magazeti yameanza kutekeleza mpango huo wa kumgombanisha Mwakifwamba na wasanii kwa kudai kuwa yeye ndiye muasisi wa migogoro ndani ya shirikisho.

Pia wamepanga kuvitembelea vikundi karibu vyote vya sanaa na kueneza sumu mbaya dhidi ya Mwakifwamba ili aonekane hafai, na pia wanakusudia kuchukua kazi za wasanii kadhaa wachanga ili zisambazwe na kampuni mojawapo iliyo chini ya Steps Entertainment ili kufuta dhana kuwa Steps inawakumbatia mastaa tu. Steps wana kampuni tatu zikiwemo za Splash na Vision One.

Binafsi naomba nieleze msimamo wangu kuwa sina maslahi na wala sishabikii upande wowote katika sakata hili na wala sina ugomvi wowote binafsi na kampuni ya Steps, ndiyo maana huwa natembelea ofisi zao na ninaandika miswaada (script) inayofanyiwa kazi zao. Nasukumwa kuandika haya bila woga kwa kuwa napenda kuona haki ikitendeka. Pia ukimya wa serikali umenitia hofu na nahisi kuna ajenda fulani miongoni mwa watendaji wa serikali waliokabidhiwa dhamana.

Kwa muda mrefu sasa wasanii wameonekana kuilalamikia kampuni ya Steps kwa kusababisha mgawanyiko mkubwa baina ya wasanii kwa kuwabagua wasio maarufu na kuwakumbatia baadhi ya wasanii maarufu huku wakiwalipa kiasi kikubwa cha pesa, kitendo kinachosababisha soko la filamu kuwa gumu kwa walio wengi.

Kila uchao wasanii wanapiga kelele ya kuibiwa kazi zao kutoka kwa wadau ambao wametega mipangilio yao inayofanikisha kunyonya kazi za wasanii ambao wanaumiza vichwa kusaka namna ya kupiga hatua. Mara nyingi inaonekana wizi wa kazi hizo unatokana na wasanii wenyewe kutofahamu haki zao kisheria, hali ambayo inadhoofisha maendeleo yao ingawa kuna wenye kufahamu haki na sheria zao lakini bado taratibu husika zinakosa nguvu ama meno katika utekelezaji wake.

Hivi karibuni kiongozi wa Bongo Movie Club, Jacob Steven (JB), alikaririwa na chombo kimoja cha habari kuwa kampuni ya Steps ndiye mkombozi halisi wa wasanii kwa kuwa inawalipa vizuri sana, na kuongeza kuwa kuna watu na makampuni fulani wanaoeneza uzushi kuhusu Steps. Wakati huohuo shirikisho la filamu kupitia rais wake likisisitiza kuwa Steps ni kampuni ya kinyonyaji.

Sitaki kuingia kwenye malumbano haya lakini shaka yangu ni pale ambapo hata Chama cha Hakimiliki na Hakishiriki Tanzania (Cosota) ambacho ndiyo msimamizi wa maendeleo ya sanaa kimeonekana kupwaya sana kiasi cha wasanii walio wengi kuhisi kuwa kimewekwa mfukoni na wanyonyaji wa jasho la wasanii.

Hatuoni juhudi zozote za kutoa elimu au kuhakikisha sheria hizi za hakimiliki na hakishiriki zenye upungufu zikifanyiwa kazi ili ziwe na meno yatakayofanikisha kuwadhibiti wezi wa kazi za sanaa hapa nchini na nje ya nchi. Ndiyo maana nadhani Shirikisho la Filamu limeamua kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuangalia namna wanavyoweza kuchangia mabadiliko ya sheria ya hakimiliki na hakishiriki.

Wasanii kupitia mashirikisho yao wanaonekana kuangalia kasoro za sheria ya hakimiliki iliyopo sasa, inavyowagusa wao wenyewe dhidi ya Taifa na kimataifa na kisha kuziba mwanya unaowezesha maharamia kutwaa kazi zao, kuzidurufu na kuwauzia watu wengine, jambo linaloonekana kuwakatisha tamaa walio wengi.

Sheria iliyopo ya Hakimiliki na Hakishiriki ilipitishwa na Bunge tukufu mwaka 1999. Na kupewa jina la Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki No.7 ya 1999. Sheria hii iliiondoa sheria ya zamani iliyotambulika kama 'Copyright Act No. 61 of 1966'. Ujio wa sheria hii ulileta furaha na mategemeo makubwa kwa wanaharakati walioipigania sheria hii. Pia taratibu (Regulations) za Sheria zilianza kupatikana ili kuwezesha utekelezaji wa sheria.

Pia tuna tatizo la wasanii kutoingia mikataba katika kazi zao. Bahati mbaya hata wanaoingia mikataba ya kusambaziwa kazi zao hawajui kama mikataba ina mapungufu makubwa sana kutokana na uelewa wa haki gani ambazo mwenye hakimiliki anazo, na zipi ambazo anaingia katika mkataba kuzitumia. Hivyo mkataba wa kusambaza kazi huonekana kama mkataba wa kuuza kazi. Na hili ni tatizo kwani humnyang'anya mhusika umiliki wa kazi zake kwa malipo kidogo sana.

Mikataba lazima iwe inaeleza vitu vya msingi kama: je mkataba unahusu haki gani? mkataba ni wa muda gani? mkataba ni wa eneo gani? nchini, au nje ya mipaka ya nchi na sehemu hizo zitajwe kabisa. Na ikiwezekana malipo yahusikanayo yatajwe.

Kwa mujibu wa chanzo kimoja cha kuaminika ni kwamba toka mwaka 2006, Waziri wa Viwanda na Biashara wakati huo alikwisha saini ‘regulation’ iliyowezesha kuwekwa alama 'antipiracy device’ katika kila kazi ya muziki na filamu ambayo ni halali, huu ni mwaka wa 5, regulation hiyo inakwama kutumika, Kulikoni?

Inasemekana kuwa viongozi fulani walipewa mshiko na wasambazaji fulani ili kukwamisha matumizi ya regulation hiyo, huku kukiwepo upotoshaji wa kuishauri serikali itunge sheria ya kuweka nembo za TRA kwenye kazi za sanaa, na wanaoshauri hayo wanajua tayari kuna sheria inayohusiana na hilo, hivyo kuongeza muda wa malumbano kuhusu ulinzi wa kazi za sanaa wakati wizi unaendelea.Kwa Hisani ya Bishophiluka blog

No comments: