Tangazo

August 12, 2011

Kumbukumbu za Ukombozi Kusini mwa Afrika kuhifadhiwa

Dr. Hifikepunye Pohamba
Mkutano wa Viongozi Wakuu wa Vyama vya Siasa vilivoshiriki katika Ukombozi Kusini mwa Afrika, umekubaliana kuweka kumbukumbu na kuhifadhi yaliyokuwa maeneo yao makuu yaliyotumika wakati wa harakati za ukombozi.

Vyama hivyo vimekutana mjini Windhoek, Namibia tarehe 11 Agosti, 2011 chini ya uenyekiti wa Rais wa Namibia, Dr. Hifikepunye Pohamba ambaye pia ni Rais wa Chama  kinachotawala cha SWAPO.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi ameshiriki na kuelezea kuunga mkono uamuzi huo wa kuainisha maeneo hayo muhimu ambayo mengi yako nchini Tanzania kutokana na mchango wake mkubwa katika ukombozi wa bara la Afrika.

« Tumekubaliana kila Chama kiainishe na kuyatambua maeneo yake muhimu  kwa ajili ya kulihifadhi kama kumbukumbu na historia ya nchi hizi, ambapo Tanzania tutasaidia katika kuyatambua lakini suala la kuyagharamia itakua jukumu la nchi husika ».

Rais amesema nchini Tanzania maeneo ya historia ya Ukombozi wa Kusini mwa Afrika yako katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu ikiwemo Chunya, Kongwa, Morogoro na Nachingwea.

Vyama vingine vilivyoshiriki katika mkutano huo wa viongozi ni Chama cha ZANU-PF kikiongozwa  na Katibu wake Mkuu wa Kwanza ambaye pia ni Rais wa Zimbabwe, Rais Robert Mugabe, Chama cha MPLA, kimewakilishwa  na Makamu wa Rais wa chama hicho Ndugu Robert De Almeida akimwakilisha Rais wa MPLA ambaye pia ni Rais wa Angola Rais Jose Eduardo Dos Santos.

Chama cha ANC kikiwakilishwa na Katibu Mkuu wake Ndugu Gwede Mantashe, ambaye amemwakilisha Rais wa ANC ambaye pia ni Rais wa Afrika ya Kusini, Rais Jacob Zuma na FRELIMO chini ya Katibu wake Mkuu Ndugu Filipe Paunde akimwakilisha Rais wa FRELIMO ambaye pia ni Rais wa Msumbiji Rais Armando Guebuza.

Pamoja na mambo mengine vyama hivi vimekutana kwa nia ya kuimarisha mahusiano baina ya vyama hivi ambavyo vina historia kubwa na muhimu sana katika Nchi za Kusini mwa Afrika.
Rais Kikwete na ujumbe wake wamerejea Dar-Es-salaam jana jioni (11 Agosti, 2011) mara baada ya kikao hicho cha siku moja kukamilika
 
Imetolewa na Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi
Windhoek, Namibia
11 Agosti, 2011

No comments: