Tangazo

January 27, 2012

Lady Jaydee kulikosa Tamasha la Muziki la Sauti za Busara 2012

Lady Jay Dee
Kwa masikitiko makubwa Busara Promotions tunatoa taarifa kuwa mwanamuziki, Lady Jaydee hatatumbuiza kama ilivyopangwa awali, katika ratiba ilikuwa mwanamuziki huyo apande jukwaani alhamisi ya Februari 9.

Taarifa kutoka kwa meneja wake, Gardner G Habash tuliyoipokea leo hii inasema “ Lady Jay Dee alipenda sana kutumbuiza katika tamasha la mwaka huu, lakini nasikitika kuwaambia kuwa hataweza, kutokana na kusumbuliwa na maradhi ambayo daktari ameshauri apate mapumziko kwa kipindi kisichopungua miezi mitatu, Kwa maana hiyo hataweza kupanda katika jukwaa lolote katika kipindi hicho.”

Mkurugenzi wa Tamasha Yusuf Mahmoud,  amejibu, “Tunamtakia afya njema na apone haraka.Lady Jay Dee ni mmoja kati ya wasanii wanaopendwa sana Tanzania. Sisi na mashabiki wa Sauti za Busara tutaukosa uwepo wake katika ufunguzi. Hakuna wa kuweza kuliziba pengo lake, lakini baada ya siku chache kuanzia leo tutatangaza nani ataichukua nafasi yake.” Lady Jay Dee mara ya mwisho alitumbuiza katika tamasha la Sauti za Busara mwaka 2006.

Kifo cha kiongozi wa Seven Survivor Band, Juma Mpogo

Busara Promotions imeshtushwa na kusikitishwa na kifo cha kiongozi wa bendi ya Seven Survivor , Juma Mpogo a.k.a. General Lupozi. Juma alifariki dunia Jumapili ya Januari 22.

Ameacha mke na watoto wawili. Alikuwa ndiye mtunzi mkuu, mwimbaji na mpiga kinanda wa bendi hiyo. Seven Survivor ni moja ya bendi zilizopo jijini Dar es  Salaam inayoongoza katika upigaji wa muziki aina ya Mchiriku, ni muziki maarufu na unaopendwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro. Hata hivyo bendi hiyo imethibitisha ushiriki wake mwaka huu hata baada ya kuondokewa na kiongozi wao, pia bendi hiyo itapambana na Jagwa Music Jumamosi , Februari 11 katika mpambano wa Mchiriku utakaoitwa Nani Zaidi?

Kuhusu Sauti za Busara

Sauti za Busara inatoa jukwaa kwa wanamuziki wa ndani, kujifunza kutoka kwa wanamuziki wa mataifa mbalimbali ya bara la Afrika wanaokuja kutumbuiza, Wakati huohuo inautambulisha muziki wa Afrika Mashariki kwa wageni. Katika jamii yoyote, aina hii ya kubadilishana uzoefu na utamaduni, ni muhimu kwa ukuaji wa kiafya na ukuaji wa muziki wowote duniani. Pia tamasha huonyesha uzuri uliopo katika muziki wetu wa asili, hutoa ajira kwa wakazi na kipato kwa wasanii.

Warsha na semina za kuwajenga kisanii na kiufundi wasanii wetu, ni moja ya nguzo kuu za shughuli za tamasha, ambazo huwalenga wanamuziki, wanahabari, mameneja wa wanamuziki, mafundi na wafanyakazi wa vivutio vya sanaa na maliasili nchini. Mikutano hii imewajengea uelewa mkubwa na wa kudumu.

Wafadhili wa Tamasha

Sauti za Busara music festival, 8 - 12 February 2012 imefadhiliwa na: The Norwegian Embassy, HIVOS, Mimeta, Roskilde Festival Charity Society, Grand Malt, Toyota, Commercial Bank of Africa, Goethe Institut, US Embassy, African Leisure Centre, fly540, Memories, Zanzibar Grand Palace Hotel, Maru Maru Hotel, SMOLE II, Zanlink, Azam Marine, Embassy of France, ZanAir, fROOTS, Times FM, Multi-Color Printers, Ultimate Security, Tabasam Tours, , Emerson Spice, Monsoon Restaurant, Southern Sun Dar es Salaam, Mercury's, Archipelago Restaurant, Stone Town Café, www.zanzibar.net
Maelezo Zaidi : www.busaramusic.org

1 comment:

Vimax said...

nice and good information. thanks