Tangazo

February 17, 2012

RAIA WA DENMARK ACHAGULIWA KUWA RAIS MPYA WA ICTR

Na Hirondelle, Arusha

Majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) wamemchagua jaji mwenzao, raia wa Denmark, Vagn Joensen kuwa Rais mpya wa Mahakama hiyo,taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na ICTR imeeleza.

Jaji Joensen anachukua nafasi ya Rais wa sasa wa Mahakama hiyo,Jaji  Khalida Rashid Khan wa Pakistani kuanzia Machi 2, mwaka huu. Jaji Khan kuanzia mwezi ujao atakuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa ya ICTR, ililyopo mjini The Hague, Uholanzi.

Rais huyo mpya wa ICTR, alijiunga na mahakama hiyo Mei 2007 na amekuwa Makamu wa Rais tangu Agosti 2011.Wakati huohuo Jaji Florence Rita Arrey kutoka Cameroon amechaguliwa kuwa Makamu wa Rais mpya, akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Jaji Joensen, kwa mujibu wa taarifa hiyo.

Jaji Joensen ambaye alizaliwa mwaka 1950, ana shahada ya pili ya sheria kutoka Chuo Kikuu cha Arhus. Kabla ya kujiunga na ICTR, alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Denmark mjini Copenhagen tangu mwaka 1994. Pia ameshawahi kutumika kama Jaji wa Umoja wa Mataifa (UN), Kosovo kati ya 2001 na 2002 na pia kuwa mhadhiri wa sheria katika vyuo vikuu viwili vya Denmark.

Miongoni mwa kesi alizowahi kuziongoza katika ICTR ni pamoja na usikilizaji wa ushahidi maalum katika kesi dhidi ya mtuhumiwa anayesakwa vikali na ICTR, Felicien Kabuga, anayesadikiwa kuwa ni mfadhali wa mauaji ya kimbari ya Rwanda mwaka 1994.

Jaji Joensen anakuwa Rais wa sita wa ICTR tangu kuanzishwa kwa mahakama hiyo ya UN, mwaka 1994.Rais wa kwanza alikuwa Laity Kama wa Senegal, akifuatiwa na Navanethem Pillay wa Afrika Kusini na kisha Jaji Eric Mose wa Norway.Na Jaji Dennis Byron wa visiwa vya St.Kitts na Nevis alifuatia kushika wadhifa huo kabla ya kukabidhi kwa Jaji Khan.

ICTR inalenga kuhitimisha kazi zake za usikilizaji wa kesi kwa hatua ya awali ifikapo mwishoni mwa Juni, mwaka huu na kukamilisha kesi zote za rufaa ifikapo mwishoni mwa 2014.

No comments: