Tangazo

March 15, 2012

ICTR: Rufaa ya Kesi ya Kanyarukiga kutolewa Mei 8

Gasper Kanyarukiga
Na Shirika la Habari la Hirondelle, Arusha

Mahakama ya Rufaa ya Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) itatoa hukumu ya kesi ya rufaa ya mfanyabiashara wa zamani nchini Rwanda, Gasper Kanyarukiga, Mei 8, 2012.

Kanyarukiga anapinga adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela alichopewa baada ya kutiwa hatiani kwa mashitaka ya mauaji ya kimbari na kuteketeza kizazi kama ukatili dhidi ya binadamu Novemba 1, 2010.

Alitiwa hatiani kwa kushirikiana na wenzake kupanga ubomoaji wa kanisa la Nyange, katika wilaya ya Kivumu, mkoa wa Kibuye, Magharibi ya Rwanda Aprili 16, 1994. Karibu wakimbizi wa Kitutsi wapatao 2,000 waliokuwa wanapata hifadhi ya maisha ya maisha yao katika kanisa hilo waliuawa.

‘’Mahakama ya rufaa inaamuru kuwepo kwa usikilizaji hadharini wa utoaji hukumu ya kesi ya rufaa ya Gasper Kanyarukiga Jumanne Mei 8, 2012,’’ inasomeka sehemu ya amri ya Mahakama ya Rufaa iliyotolewa Machi 13, 2012.

Mwishoni mwa mwezi uliopita Mahakama hiyo ilitangaza kwamba tarehe hiyo pia itatoa hukumu kwenye kesi mbili za rufaa za maafisa wawili wa zamani wa jeshi la Rwanda. Maafisa hao ni pamoja na Meja Aloys Ntabakuze na Luteni Idelphonse Hategekimana ambao kila mmoja wao anapinga adhabu ya kifungo cha maisha jela aliyopewa na mahakama ya awali baada ya kutiwa hatiani kwa kuhusika katika mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.

Wakati wa kusikiliza rufaa ya Kanyarukiga Desemba 14, 2011, mwendesha mashitaka aliiomba mahakama hiyo imwongezee adhabu mfungwa huyo ya zaidi ya miaka 30 aliyopewa.

Kwa upande wake, Wakili Kiongozi upande wa utetezi, David Jacobs aliiomba mahakama kumpunguzia mteja wake adhabu aliyopewa iwapo itathibitisha adhabu hiyo. Alieleza kwamba Kanyarugika ameshitakiwa na kutiwa hatiani kwa mashitaka ambayo hakuyafahamu.

Kanyarukiga siyo mnyarwanda pekee anayehusishwa na mauaji yaliyofanyika katika kanisa la Nyange. Wengine ni pamoja na aliyekuwa Padre wa kanisa hilo, Athanasse Seromba ambaye anatumikia adhabu ya kifungo cha maisha jela na meya wa zamani wa wilaya hiyo ya Kivumu, Gregoire Ndahimana ambaye anatumikia jela miaka 15.

Mwingine anayetuhumiwa kushiriki pia katika uhalifu huyo ni Inspekta wa zamani wa Polisi katika wilaya ya Kivumu, Fulgence Kayishema ambaye bado anasakwa na ICTR na hivi karibuni mahakama hiyo ya Umoja wa Mataifa iliamuru kesi hiyo ikasikilizwe nchini Rwanda.

Kesi ya Kanyarukiga ilianza kusikilizwa Agosti 31, 2008. Alitiwa mbaroni Afrika Kusini Julai 16, 2004 na kuhamishiwa makao makuu ya ICTR mjini Arusha, Tanzania siku tatu baadaye.

No comments: