Tangazo

March 20, 2012

Idhaa ya Kiswahili ya BBC kuanzisha kipindi kipya cha 'Haba na Haba' kitakachojenga majadiliano baina ya wananchi wa kawaida na Viongozi wa serikali

Shirika la Utangazaji la Uingereza la BBC (BBC World Service) likishirikiana na Tawi lake la Kimataifa la maendeleo la BBC Media Action limeunganisha nguvu na Redio Free Africa pamoja na redio nyingine kadhaa nchini Tanzania kuzindua kipindi kipya cha kila wiki kitakachotoa fursa ya kujenga majadiliano baina ya wananchi wa kawaida na vongozi wao.

Kuanzia Jumamosi ya tarehe 24 Machi, kipindi hicho kitakachojulikana kama “Haba na Haba” kitaandaliwa na Idhaa ya Kiswahili ya BBC na kitatangazwa na Mtangazaji Hassan Mhelela.  Haba na Haba kitabeba ripoti/Taarifa kutoka kwa waandishi wa redio hizo washirika kutoka pembe mbalimbali za nchi pamoja na kusikia uzoefu wa maisha halisi ya wananchi wa kawaida wakieleza yanayowasibu maishani mwao.

Haba na Haba kitakuwa ni kipindi kinachobeba Ukweli, uhalisi na kitakachogusa maisha halisi ya kila siku ya wananchi.

Kwa takribani dakika 20 kitatoa nafasi kwa wananchi kuwa na nafasi ya kuwauliza maswali maafisa na viongozi wa serikali pamoja na wawakilishi wao.

Pamoja na kuibua masuala kama uhaba wa maji na chakula, ukosefu wa ajira na umasikini, barabara, umeme, rushwa, elimu na afya pia kipindi hiki kitaangazia yale ambayo serikali imefanikiwa kuyafanya na hatua ambazo zimefikiwa mpaka wakati huo.

Mkurugenzi mkazi wa BBC Media Action Rebecca Stringer, amesema “Katika nchi ya Tanzania, vyombo vingi vya habari vimekuwa vikiripoti taarifa nyingi za Dar es salaam na hata habari zinazohusu ufanisi wa serikali zimekuwa zikitazamwa katika ngazi ya kitaifa kwa kuwaangalia zaidi viongozi wa juu.”

 Ikitangazwa pembe zote za nchini na mshirika mkuu Redio Free Africa, pamoja na vituo vya redio washirika vingine takribani ishirini Haba na Haba kitawakilisha matatizo ya wananchi kote nchini Tanzania kikiyatazama kwa undani na kulenga zaidi katika kile kinachowaathiri katika maisha yao ya kila siku. Kwa kuweza kuibua matatizo hayo katika ngazi ya kitaifa ndipo kipindi hiki kitakapoweza kutoa fursa kwa watanzania wa kawaida na Serikali na kuwapa nguvu wasikilizaji wake kuwataka walio kwenye mamlaka kuwajibika katika majukumu yao.

Michango ya habari katika Haba na Haba kutoka mikoani itatolewa na redio sita washirika zilizosambaa kijiografia nchini ambazo ni:-  Nuru FM iliyoko Iringa, FADECO Redio iliyoko Karagwe, Pangani FM iliyoko Pangani Tanga, Jogoo Fm iliyoko Songea, Orkonerei ama ORS iliyoko mkoani Manyara, na Hits FM iliyoko huko Zanzibar.

Mtangazaji mahiri wa makala hiyo ya Haba na Haba Hassan Mhelela, anasema anatarajia makubwa kutoka kwa waandishi hao wa habari waliosambaa kijiografia nchini Tanzania na alikaririwa akisema “Najisikia fahari sana kuwa miongoni mwa wawezeshaji wa Haba na Haba – hiki ni kipindi ambacho kitagusa kwa undani hisia za Watanzania na ikijenga jukwaa huru kwa wote kwa wananchi kwa upande wingine na Serikali kusikiliza, kuchukua hatua na kuelewana kila mmoja kwa nafasi yake.”

Makala ya Haba na Haba itatangazwa na Idhaa ya Kiswahili ya BBC ikirushwa na Redio Free Africa ambaye ndie mshirika mkuu wa BBC nchini Tanzania.

Kwa upande wake Naibu mwenyekiti na kurugenzi Mtendaji wa Redio Free Africa Samwel Nyalla, amesema: “Redio Free Africa imekuwa na ushirika na BBC tangu mnamo mwaka 1996 na kwa kweli tunayo furaha kubwa kwamba watanzania walio wengi wataweza kusikiliza kipindi hiki kipya cha ‘Haba na Haba’ kupitia mtandao wa masafa yetu takriban 29 nchi nzima. Wasikilizaji wetu wapatao ilioni 12 abao huwa wanasikiliza RFA kila wiki watapata fursa bora kabisa kuwa sehemu ya majadiliano haya mazuri yatakayosambazwa na BBC.”

Haba na Haba itatangazwa na idhaa ya Kiswahili saa 10.05 kwa saa za Afrika Mashariki siku za Jumamosi na siku za Jumapili, na kupitia Redio Free Africa itarushwa siku ya Jumamosi saa 12.30 jioni na kurudiwa siku ya Jumapili saa 12.00 asubuhi na saa 11.05 jioni siku hiyohiyo.

Kama ilivyo kwa matangazo mengine ya Idhaa ya Kiswahili ya BBC Haba na Haba pia itapatikana kupitia tovuti yake ya bbcswahili.com.

No comments: