Tangazo

April 23, 2012

JESHI LA POLISI DODOMA LAKAMATA MIRUNGI BUNDA 24

Mnamo tarehe 22/04/2012 majira ya saa 13:15 mchana katika eneo la Kibaigwa  Wilaya ya Kongwa, Jeshi la Polisi limefanikiwa kukamata Mirungi bunda ishirini na nne (24), yenye thamani ya shillingi laki moja na kumi na saba elfu.

Katika tukio hilo watu wawili wanashikiliwa na Jeshi la Polisi wilayani humo kwa tuhuma za kukutwa na mirungi hiyo, watuhumiwa hao ni  ABDUL S/O AHMED FARAH, Maarufu kama CHIFU, mwenye umri wa miaka (40), na OMARY S/O HASH FARAH miaka (50) wote wakazi wa Kibaigwa.

Jeshi la Polisi baada ya kupata taarifa toka kwa wananchi kuwa kuna watu  wanafanya biashara ya kuuza Mirungi, ndipo Polisi waliweka mtego na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja Bw. OMARY S/O HASH FARAH akiwa na ruba moja (bunda moja) alilokuwa anataka kuliuza kwa  mtu aliyewekwa kama mtego.

Aidha Baada ya kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo, ndipo mtuhumiwa mwenzake akajifungia chumbani ili asikamatwe, lakini baada ya kukamatwa na alipopekuliwa akakutwa na ruba nyingine ishirini na tatu (23) ndani ya nyumba walimokuwa wakiishi.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma linapenda kutoa pongezi kwa wananchi, waliohusika kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu hao, ambao kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi walifanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao.

Mwisho napenda kutoa wito kwa wananchi wote kuendelea kutekeleza dhana nzima ya Polisi Jamii na Ulinzi shirikishi, ili kuhakikisha maeneo yetu tunayoishi yanakuwa ya Utulivu, Amani na Salama na  hivyo kusaidia kukuza ustawi wa jamii yetu.

Wakati huo huo,  mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la JOHN S/O LUGANJE, mwenye umri wa miaka hamsini na nne(54) mgogo, na mkulima mkazi wa kijiji cha chunju wilaya ya Mpwapwa amekutwa amekufa porini baada ya kujinyonga kwa shati alilokuwa amelivaa.

Kwa mujibu wa Taarifa za Jeshi la Polisi Wilayani Mpwapwa, marehemu aligundulika amekufa porini majira ya saa nane mchana, siku ya jumamosi  tarehe 21/04/2012, na kwamba alikuwa ametoweka nyumbani kwake toka tarehe 16/04/2012.

Hata hivyo taarifa toka kitongoji cha Ng’ongwa katika kijiji cha Chunyu zinasema marehemu alikuwa mgonjwa wa akili, hata hivyo Jeshi la polisi linaendelea na upelelezi wa tukio hilo.

Imetolewa na: SACP - Zelothe Steven
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma

No comments: