Tangazo

April 17, 2012

TAREHE ZA TAMASHA LA 10 LA SAUTI ZA BUSARA 2013 ZATAJWA

Na Mohammed Mhina, Zanzibar.
 

Sauti za Busara Zanzibar (Busara Promotions) imesema kuwa Tamasha la 10 la Sauti za Busara kwa mwaka ujao 2013 litaanza kufanyika Februai 14 hadi 17, 2013 kwenye ukumbi wa Kihistoria wa Ngome Kongwe mjini Zanzibar.

Tamasha la Sauti za busara ni tukio la muziki linalofanyika kwa kila mwaka Afrika Mashariki na hufahamika zaidi kama ‘tamasha rafiki katika sayari’.

Katika Tamasha lijalo mwakani linatarajiwa kuwaleta wanamuziki zaidi ya 200 kutoka katika vikundi zaidi ya 20 kutoka nchi za Afrika Mashariki na kwingineko Duniani ambavyo vitafanya maonyesho ya moja kwa moja (live)katika ukumbi wa Ngome Kongwe mjini Zanzibar .

Tamasha hilo litafanyika kwa maonyesho ya muziki kwa siku tatu mfululizo, ratiba kuu itaendelea  mpaka jumapili kwa maonyesho yatakayoanzia saa 11 jioni mpaka saa 7 usiku kila siku.

Wakati wa Tamasha hilo pia, kutakuwepo na maonyesho ya filamu za muziki wa kiafrika, Makala, video za muziki na matamasha katika kuangazia uendelezaji wa utajiri na mchanganyiko wa muziki wa afrika.

Sauti za Busara pia litaendelea na uendeshaji wa kongamano la Movers and Shaker kwa ajili ya wenyeji na wageni ambao ni wataalam wa sanaa.

Kongamano hilo litatoa fursa ya majadiliano, kubadilishana uzoefu wa uendelezaji wa mawazo ya ubunifu katika ukanda wa nchi za Afrika ya Mashariki na kwingineko Duniani.

Aidha jamii imehimizwa kuandaa matukio mbalimbali ya ziada yakiwemo matukio ya vikundi vya Ngoma za kiutamaduni, Maonyesho ya mavazi, mashindano ya ngalawa na maonyesho ya vikundi vikongwe vya taarabu kwa wenyeji.

Tangu kuanzishwa kwa Tamasha la Sauti za Busara hapa nchini hapo mwaka 2004, Tamasha hilo limefanikiwa kuwapandisha jukwaani wasanii mbalimbali akiwemo Samba Mapangala & Orchestra Virunga.

 Wengine ni Natacha Atlas, Didier Awadi, Bassekou Kouyate, Jagwa Music, Tumi & The Volume, Freddy Masamba, Thandiswa, Mlimani Pack Orchestra, Culture Music Club, Orchestra Poly Rythmo na wengineo wengi. Tamasha linafanya muziki wa moja kwa moja (Live).

Kuanzia mwezi huu wa Aprili wasanii wanaweza kufanya maombi ya moja kwa moja kupitia tovuti yetu ya Sauti za Busara na mwisho wa kutuma maombi ni kushiriki ni Julai 30, 2012.

Hata hivyo bado Sauti za Busara zinatafuta wasanii vijana  wanaochipukia pamoja na Wasanii Wakongwe ili mushiriki katika tamasha hilo kwa lengo la kuwaunganisha Waafrika.

Wasanii wametakiwa kutuma maombi yao kupitia tovuti ya www.busaramusic.org na kabla ya Julai 31,2012.

No comments: