Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete yuko
njiani kwenda Washington, Marekani kuhudhuria Mkutano wa Wakuu wa Nchi Tajiri
Zaidi na Zenye Viwanda (Group of Eight – G-8) kwa mwaliko wa Rais wa Marekani
Mheshimiwa Barack Hussein Obama.
Rais
Kikwete na ujumbe wake waliondoka nchini usiku wa jana, Jumanne, Mei 15, 2012
kwenda Marekani kupitia Nairobi, Kenya na London,
Uingereza.
Rais
Kikwete ni mmoja wa Marais wanne wa Afrika ambao Rais Obama amewaalika
kuhudhuria Mkutano wa G-8 ambao unafanyika Jumamosi kwenye eneo la mapumziko ya
marais wa Marekani, Camp David, katika Jimbo la Maryland.
Hata
hivyo, shughuli za kikao hicho zinaanza rasmi kesho wakati Waziri wa Mambo ya
Nje wa Marekani, Bibi Hillary Clinton atakapokutana na viongozi wa nchi wataohudhuria
mkutano wa mwaka huu wa G-8.
Mbali
na Rais Kikwete, marais wengine wa Afrika walioalikwa na Rais Obama kuhudhuria
mkutano huo ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) Mheshimiwa Thomas Boni Yayi,
Rais wa Ghana Mheshimiwa Atta John Mills na Waziri Mkuu wa Ethiopia Mheshimiwa
Meles Zenawi.
Rais
Kikwete amealikwa kushiriki katika mkutano wa mwaka huu wa G-8 ili kutoa uzoefu
wake katika mapambano ya kuendeleza kilimo na kuleta usalama wa chakula katika
Tanzania na Afrika kwenye kikao ambacho kitazungumzia “Hali ya Kilimo Duniani
na Usalama wa Chakula” ambacho Rais Obama atakuwa mwenyekiti wake na ambacho
Rais Kikwete atazungumza kwa dakika 10.
Rais
Kikwete amealikwa kwa sababu ya uongozi wake katika masuala ya maendeleo ya
kilimo ambao ameuonyesha kwenye uanzishwaji wa program mbali mbali hapa nchini
na katika Afrika zikiwamo za ASDP
(Agricultural Sector Development Programme), Kilimo Kwanza na SAGCOT (Ukanda wa Maendeleo ya Kilimo
Kusini mwa Tanzania).
Rais
Kikwete pia ni miongoni mwa viongozi wa Afrika walioko mbele katika kuendeleza
programu ya kilimo ya Grow Africa Partnership
ambako nchi saba za Afrika zinashirikiana na wadau wa kimataifa kuendeleza
kilimo katika Afrika.
Mkutano
huo wa G-8 unafanyika wakati kuna habari za uwezekano wa kutokea kwa upungufu
wa chakula na hata kuzuka kwa baa la njaa katika baadhi ya nchi za Afrika.
Wakati
wa ziara hiyo ya siku tano, Rais Kikwete pia atakutana na kufanya mazungumzo na
maofisa wa Shirika la Millenium Challenge Corporation (MCC), wakiongozwa na
Mtendaji Mkuu wake, Bwana Daniel Yohanes.
Tanzania ni
miongoni mwa washirika wakuu wa MCC, ambacho ni chombo cha jitihada za
maendeleo cha Serikali ya Marekani na ambacho kwa sasa kinatekeleza miradi
mbali mbali ya miundombinu yenye thamani ya dola za Marekani milioni 698 katika
Tanzania.
Katika
Marekani, Tanzania inaelezwa kama nchi mfano wa mafanikio katika utekelezaji wa
miradi ya MCC na Rais Kikwete anasifiwa kwa utekelezaji wa miradi hiyo unaongozwa
na uwazi na ufanisi wa kiwango cha juu.
Imetolewa na:
Kurugenzi
ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
16 Mei, 2012
No comments:
Post a Comment