Tangazo

May 17, 2012

TANZANIA MWENYEKITI WA KAMATI YA DUNIA YA SAYANSI NA TAALUMA YA MABADILIKO YA TABIA NCHI

Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Bw. Richard Muyungi (katikati)  baada tuu ya kupewa Uenyekiti wa Kamati ya Dunia ya Sayansi na Mabadiliko ya Tabia Nchi, huko Durban Africa ya Kusini na kuanza kazi rasmi katika mkutano unaoendelea nchini Ujerumani. (Picha na Evelyn Mkokoi)
***************
Na Evelyn Mkokoi- Afisa Habari OMR
Bonn, Ujerumani

Tanzania kwa mara ya kwanza imepata nafasi kwa  miaka miwili ijayo  ya kuongoza   Kamati ya umoja wa mataifa ya sayansi na taaluma ya mabadiliko ya tabia nchi,  chini ya mkataba wa Umoja wa Mataifa wa  mabadiliko ya tabia Nchi. Kamati imeanza kazi rasmi jana wiki hii,  wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 36 wa mabadiliko ya tabia nchi. Hayo yameelezwa leo katika mahujiano maalum na ofisa Mkuu wa programu ya Uendeshaji ya Sekretarieti ya Mkataba huu Bi Hanna Hoffmann, hapa Bonn, Ujerumani.

Bi Hanna Ameeleza kuwa Bw. Richard Muyungi ambae ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya mazingira kutoka katika ofisi ya Makamu wa Rais amepewa dhamana hiyo na nchi zote duniani wanachama wa mkataba huu kutokana na uzoefu wake mkubwa katika  diplomasia ya  mabadiliko ya tabianchi na upeo wa kutosha  juu ya taaluma nzima ya sayansi ya mabadiliko ya tabianchi. 

“Bw. Muyungi  ni mwana diplomasia aliyebobea katika masuala ya mabadiliko ya tabianchi, ana elimu ya kutosha katika eneo hili na ni mzoefu sana na amekuwa akihudhuria na kuongoza mkutano mingi ya mabadiliko ya tabianchi hasa zaidi akiongoza kundi la nchi zinazoendelea, hivyo naamini kabisa, uteuzi wake ni muafaka na ataongoza vizuri kamati hii na masuala yote muhimu  kama ulivyoona mwenyewe alivyoongoza  leo mkutano kuhusu  kilimo  na mabadiliko ya tabianchi .” Alisisitiza.

Bi Hanna aliongeza kuwa Kundi la nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania ina nafasi kubwa zaidi ya kujifunza na kutumia njia za kuhimili na kukabilina na mabadiliko ya tabia nchi zaidi kutokana na nafasi yake ya uwenyekiti wa Kamati hii.

Kwa Upande wake Bw. Richard Muyungi ameeleza kuwa uteuzi huu uliofanyika rasmi Desemba mwaka jana na nchi zote wanachama huko Durban  Afrika ya kusini, na kuanza rasmi leo, ni heshima   kwa nchi  na nafasi ya pekee kwa Tanzania kuweza  kujifunza mengi  na kupata fursa  mbali mbali za kuweza  kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi zinazoikabili  Tanzania  ikiwemo uhaba wa mvua, mafuriko, kuongezeka kwa kina cha bahari na,  mvua zisizotarajiwa, na baadhi ya maeneo ya  nchi kuelekea kuwa janga kutokana na mabadiliko haya.

Mkutano huu unaoendelea hapa  mjini Bonn Ujerumani, ni sehemu ya maandalizi ya Mkutano wa Dunia wa mabadiliko ya tabia nchi, ambao utawakutanisha wakuu wa nchi duniani utakaofanyika mjini Doha,Qatar, Novemba mwaka huu. Aidha utatoa mchango katika mkutano wa wakuu wa nchi kuhusu Maendeleo endelevu (Rio+20) utakaofanyika huko Rio, nchini Brazil baadaye mwezi Juni.

Pamoja na masuala ya Kilimo na mabadiliko ya tabianchi,  Kamati hii pia inatafuta muafaka kuhusu suala la matumizi ya sekta ya misitu katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kuzingatia maslahi ya nchi zenye misitu inayonyonya gesi hizi, na taratibu za kusimamia na kutekeleza miradi ya kupunguza hewa ukaa  katika nchi zinazoendelea bila kuathiri maendeleo ya nchi hizi. 

Aidha katika mkutano huu, Masuala ya upatikanaji wa fedha ili kukabiliana na mabadilkio ya tabianchi kwa nchi maskini duniani na suala la nchi zilizoendelea kuongeza juhudi za kupunguza gesijoto zinazosababisha mabadiliko ya tabianchi yamepewa kipaumbele.


No comments: