Katibu Mkuu wa UN, Ban Ki-moon |
Ujumbe wa pamoja kutoka kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw Ban
Ki-moon na Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO Bi Irina Bokova kwa katika
kuadhimisha Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari.
Uhuru wa kujieleza ni moja ya haki yetu muhimu sana. Ni haki inayoweka msingi kwa uhuru mwingine na heshima ya binadamu. Vyombo vya habari vilivyo huru ni muhimu katika kufanikisha hili. Huu ndiyo ujumbe wa Siku hii ya Uhuru wa Vyombo vya Habari.
Uhuru wa Vyombo vya Habari unajumuisha uhuru wa kutoa mawazo,uhuru wa kupata na kueneza taarifa na mawazo kwa njia yoyote bila mipaka, kama ilivyoelezwa kwenye Ibara ya 19 ya Tamko la Haki za Binaadamu.
Uhuru huu ni muhimu kwa kusaidia kuwepo kwa jamii zenye mafaniko na tija. Mabadiliko katika nchi za Kiarabu yameonyesha nini kinachoweza kutokea pale shauku ya kupata haki inapopewa nguvu na vyombo vya habari vya kizazi cha kisasa na vile vya kawaida.
Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, Irina Bokova |
Uhuru mpya wa vyombo vya habari unatoa matumaini ya kubadili jamii katika mfumo wa uwazi zaidi na uwajibikaji. Unafungua namna mpya za kuwasiliana na kupeana taarifa na weledi. Kelele kubwa zinasikia---hasa kutoka kwa vijana---sauti ambazo hazikuwa zikisikika siku za nyuma. Hii ndiyo imepelekea kauli mbiu ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari mwaka huu yaani: Uhuru wa Vyombo vya Habari Unasaidia Kubadili Jamii.
Uhuru wa Vyombo vya Habari pia unakabiliwa na changamoto nyingi duniani. Mwaka uliopita, UNESCO ililaani mauaji ya wanahabari 62 ambao walikufa kwa kutimiza wajibu wao. Waandishi hawa hawawezi kusahaulika na waliofanya udhalimu huu ni lazima waadhibiwe.
Kwa kadri uenezaji habari unavyozidi kufanyika kwa njia ya teknolojia za kisasa zaidi, waandishi wanaotumia taratibu za utawanyaji habari za kizazi cha kisasa, wakiwemo wale wanaoblogi, wanadhalilishwa, wanashambuliwa na kuuawa kwa wakitimiza wajibu wao. Hawa pia wanapaswa kulindwa sawasawa na wanahabari wanaotumia taratibu za uanahabari wa kawaida.
Mkutano wa Kwanza wa Pamoja wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa kuhusiana na Usalama wa Wanahabari na Suala la Watu Wanaofanya Uhalifu Bila Kuadhibiwa ulifanyika katika makao makuu ya UNESCO tarehe 13 na 14 mwezi Septemba mwaka 2011.
Tulitoa Mpango Kazi kwa Umoja wa Mataifa kujenga mazingira huru na salama zaidi kwa wanahabari na wafanyakazi wa vyombo vya habari kokote waliko. Wakati huo huo, tutaendelea kuimarisha misingi ya kisheria kwa ajili uwepo wa vyombo huru vya habari, hasa katika nchi zilizoko kwenye mchakato wa mabadilko au zinazojijenga upya baada ya kuwa kwenye hali ya migogoro. Katika kipindi ambacho upatikanaji wa taarifa ni mkubwa sana, ni lazima tuwasaidie vijana wapate ujuzi unaohitajika na weledi katika masuala ya habari.
Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari ni fursa yetu ya kupandisha bendera katika mapambano ya kuleta uhuru wa vyombo vya habari. Tunazitaka nchi, asasi za kitaalamu za habari na asasi za kijamii kote duniani kujiunga na Umoja wa Mataifa katika juhudi za kutetea haki ya kujieleza kwa njia za kisasa na zile za kawaida kwa kufuata taratibu zinazokubalika kimataifa. Huu ndiyo msingi wa haki za mtu mmoja mmoja, jamii zenye tija na ndiyo nguvu ya kuleta mabadiliko katika jamii.
No comments:
Post a Comment