Tangazo

May 24, 2012

Wassira azomewa mkutanoni

Steven Wassira
Na Mwandishi wetu, Bunda

JINAMIZI la zomeazomea limezidi kumwandama mbunge wa jimbo la Bunda, Steven Wassira, ambapo jana tena alizomewa na wananchi baada ya kushindwa kujibu maswali waliyomuuliza.

Wassira alikumbwa na zahma hiyo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya stendi ya zamani ya mjini Bunda.

Katika mkutano huo, Wasira aliulizwa maswali matatu na kijana mmoja aitwaye Joashi Kunaga ambayo baadhi yalionekana kumkasirisha.

Maswali hayo pamoja na kumtaka aeleze ni kwa nini eneo la Shule ya Msingi Balili limechukuliwa na aliyekuwa mkuu wa wilaya, Chiku Galawa, ambaye sasa ni mkuu wa mkoa wa Tanga na wananchi walishalalamika lakini yeye hajawahi kulizungumzia.

Swali la pili kijana huyo alitaka kufahamu ukosefu wa maji katika Hospital ya DDH Bunda ambako sasa hivi wagonjwa wanalazimika kutoa maji majumbani mwao huku wakati ziwa liko km 11 toka mjini Bunda.

Katika swali lake la tatu alimuuliza kuwa katika mkutano huo alikuwa anahutubia kama mbunge, waziri au kada wa CCM kwani alitakiwa kufahamu kuwa Bunda ina wachama wa vyama vingi.

Mwingine aliyeuliza swali ni mwenyekiti wa mtaa wa Nyerere, Maxmilian, aliyetaka kujua ni kwani nini halmashauri imetengeneza milango ya shule za sekondari za kata kwa shilingi laki nne kwa kila mlango.

Baada ya kuulizwa maswali hayo Wassira alisimama katika hali iliyoonyesha kuwa ana hasira na kuaanza kujibu maswali hayo kwa ukali.

Wassira alianza kujibu swali la kwanza la Kunaga akisema kuwa hawezi kulisemea hilo ni la watu wa ardhi kwa madai kuwa kama mtu alikuwa na pesa zake akaomba akapewa yeye hawezi kulizungumzia.

Kuhusu suala la maji alisema kuwa maji yapo katika mchakato na kwamba wananchi watarajie kupata maji muda si mrefu jibu ambalo wananchi walilikataa na kudai kuwa ahadi zake kuhusu maji zimekuwa za uongo tangia mwaka 2007 hadi leo amekuwa akisema uongo.

Akijibu kuhusu hoja ya yeye kuhutubia kama mbunge au waziri, Wassira alionekana kujawa na hasira na kuuliza kwa ukali, “Kwani Wenje alikuja kuhutubia hapa hivi karibuni kama nani?”

Jibu hilo lilizidi kuwachefua wananchi ambao walianza kuzomea huku wakiimba: “People’s Power.”

Wengine walisikika wakisema: “Afadhali Esther Bulaya kuliko wewe.”

Jambo ambalo lilifanya polisi waliokuwepo kuanza kujiandaa kwa lolote na ndipo Wasira alipochukia na kuamua kuondoka majira ya saa 11 huku akiacha wananchi wakiwa bado na maswali ya kumuuliza.

Hata hivyo baada ya kuondoka wananchi hususan kundi kubwa la vijana lililokuwepo mkutanoni hapo liliendelea kuimba: “People’s Power.” Huku wakinyoosha vidole viwili vinavyotumiwa na Chama cha CHADEMA na wengine wakilitaja sana jina la mbunge wa viti maalumu vijana Bulaya ambaye sasa anaonekana kuwa kipenzi cha Wanabunda kutokana na msimamo wake bungeni wa kutetea mambo mbalimbali likiwemo suala la kero ya maji ambalo ni tatizo kubwa kwa wananchi wa mji wa Bunda na vitingoji vyake.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi mara baada ya Wassira kuondoka, baadhi ya wananchi walimtuhumu mbunge huyo kushindwa kujibu maswali aliyoulizwa wakisema kuwa kitendo hicho kinaonyesha alivyochoka kutokana na umri wake.

Wananchi hao walimshutumu Wassira wakisema kuwa aliishawaona wananchi wa Bunda ni watu wa kudanganywa lakini safari hii wamechoshwa na hadithi zake.

“Huyu mzee ni msanii; juzi alipoona anataka kufanya mkutano hapa aliwaita waandishi wa habari wa TV na magazeti wale wanaomsapoti akaandaa na mtambo wa kuchimba mtaro ambao ulichimba km chache na akachukua wajumbe wa bodi ya maji wakachukuliwa maoni na yeye akaongea lakini baada ya yeye kuondoka huko Nyabehu ule mtambo haupo tena na kazi hiyo haiendelei sasa leo anakuja kutupatia hadidu za rejea,” alisema mkazi mmoja Chacha Maswi mkazi wa kijiji cha Nyabehu.

Hata hivyo mkutano huo ulihudhuriwa na watu wachache tofauti na siku nyingine lakini pia ukilinganisha na ule aliohutubia mbunge wa Nyamagana Eziekiel Wenje mwezi uliopita na wananchi wakakubali kunyeshewa mvua wakimsikiliza.

Hali kadhalika idadi hiyo ya watu waliohudhuria mkutano huo wa Wassira pia haikufikia ile ya waliokuwepo juzi wakati Bulaya akikabidhi kombe la timu ya vijana wa Bunda mjini.
Chanzo: Tanzania Daima Mei 24.2012

No comments: