*************************
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Jakaya Mrisho kikwete, mchana huu Juni 4, 2012 amekutana na Wabunge wa Tanzania katika Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki jijini Arusha.
Mhe. Rais, ambaye aliwakaribisha Wabunge hao kwa chakula cha mchana katika hoteli ya Ngurdoto Mountain Lodge, aliwapongeza kwa kuchaguliwa kwao kuiwakilisha Tanzania katika Bunge hilo la Jumuiya, na kuwataka wasimamie na kutetea maslahi ya nchi wakiwa huko.
Pia Rais amewataka Wabunge hao kuwa karibu na Serikali katika kushauriana namna ya kukabiliana na changamoto zitazojitokeza katika kazi zao, na kuwakumbusha kwamba majukumu ya Bunge hilo la Jumuiya ni kusimamia makubaliano (treaty) yaliyoyoorodheshwa katika kuundwa kwake na kuendeshwa.
Alisema: “Msome vyema na kuyaelewa makubaliano (treaty) hayo yote na vipengele vyake na msaidie kuiendeleza Jumuiya ambayo wanachama wote watanufaika nayo, na siyo upande mmoja.
“Tumewapeleka pale kwa ajili ya maslahi ya Tanzania hivyo mjue kuna kazi nyingi kweli, hasa katika kujadili yale yote yaliyokubaliwa katika makubaliano ya jumuiya” alisema.
Mhe. Rais alikutana na Wabunge wote wa Tanzania katika Bunge la Jumuiya ya Mashariki isipokuwa mmoja, Bi. Nderkindo Perpetua Kessy ambaye hakufika kwa sababu iliyoelezwa kuwa ni mgonjwa.
Waliofika ni pamoja na Mwenyekiti wa Wabunge wa Tanzania kwenye Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki, Alhaj Adam Omar Kimbisa na Katibu wake, Mh Shy-Rose Saddrudin Bhanji.
Wengine waliofika ni Mhe. Anjela Charless Kizigha, Mh. Maryam Ussi Yahya, Dkt Twaha Issa Taslima, Mhe. Abdullah Ali Hassan Mwinyi, Mhe Bernard Musomi Murunya na Mhe. Charles Makongoro Nyerere.
..……..Mwisho……….
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
DAR ES SALAAM.
04 Mei, 2012
No comments:
Post a Comment