Na Mwandishi wa Jeshi la Polisi- Zanzibar
ZANZIBAR JUMATATU JUNI 4, 2012. VIONGOZI wanne wa Kundi la Uamsho waliohusika katika uchochezi wa vurugu za wiki iliyopita mjini zanzibar, leo wamejisalimisha kwa Makachero wa Jeshi la Polisi na kuhojiwa kwa masaa kadha kabla ya kuachiwa kwa mashariti.
Taarifa ya Afisa Habari Mkuu wa Jeshi la Polisi Zanzibar Inspekta Mohammed Mhina, imewataja viongozi waliojisalimisha kuwa ni Shekhe Suleiman Juma(62) mkazi wa Makadara na Shekhe Fikirini Majaliwa(47), mkazi wa Jang’ombe.
Taarifa hiyo imewataja wengine waliojisalimisha kuwa ni pamoja na Katibu wa Jumuia ya Uamsho Sheikhe Abdallah Saidi(45), mkazi wa Misufini pamoja na Afisa Usalama wa Jumuiya hiyo Bw. Haji Sadifa(51), mkazi wa Mwembenjugu.
Viongozi hao pamoja na mpambe wao, walijisalimisha mapema asubuhi leo kwa Viongozi wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Mangaribi Zanzibar na kuhojiwa kwa muda kabla ya kupelekwa Makao Makuu ya Upelelezi Zanzibar kwa mahojiano zaidi na baadaye kuachiliwa kwa dhamana.
Tangu kutokea kwa vurugu zilizopelekea kukamatwa kwa baadhi ya wafuasi wa kundi la Uamsho mjini Zanzbar na kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zao, viongozi hao watatu pamoja na mpambe wao walikuwa hawajapatikana.
Mara baada ya vurugu hizo za wiki iliyopita, Kamishna wa Polisi Zanzibar CP Mussa Ali Mussa, alisema kuwa Jeshi la Polisi litahakikisha kuwa wale wote waliochoche vurugu hizo wanakamatwa na kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka yao.
Katika vurugu hizo zilizodumu kwa muda wa siku tatu, pia zilizopelekea kuchomwa moto kwa baadhi ya makanisa na mali nyingine za madukani kuporwa na nyingine kuharibiwa na wafuasi wa kikundi hicho.
Jeshi la Polisi Visiwani hapa limeendelea kutoa wito kwa viongozi wengine walioshiriki katika vurugu hizo kujisalimisha wenye Polisi badala ya kusubiri kutafutwa.
Hadi sasa watuhumiwa 78 wakiwemo viongozi wa kundi la Uamsho, wamekamatwa na kufikishwa mahakamani ambapo baadhi yao wameachiliwa kwa dhamana na wengine wakipelekwa rumande kwa kukosa wadhamini wenye kuaminika hadi Juni 11, mwaka huu kesi yao itakapotajwa tena.
No comments:
Post a Comment