Tangazo

October 12, 2012

WATANZANIA WAASWA KUCHANGIA UJENZI WA VITUO VYA KUIBUA NA KUKUZA VIPAJI VYA WATOTO

Mwenyekiti wa Ujenzi wa kanisa la AICT kilungule Kimara Bw. Paul Luchemba (katikati) akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari kuhusu harambee ya ujenzi wa kituo cha kuibua uwezo na vipaji tofauti vya watoto  kitakachokua na uwezo wa kuchukua watoto zaidi ya 500 na kugharimu kiasi cha shilingi milioni 350.Wengine ni mwinjilisti John Kihamba (kulia) na Bw. Mozes Mbushi. Picha na Aron Msigwa - MAELEZO
*****************************
Na. Aron Msigwa – MAELEZO.

Wito umetolewa kwa watanzania kujenga tabia ya kuchangia ujenzi wa miradi mbalimbali ya kulea na kukuza vipaji vya watoto ili kujenga taifa lenye maadili na  wataalam wa baadaye katika masuala mbalimbali.

Wito huo umetolewa leo  jijini Dar es salaam na Mwenyekiti wa Ujenzi wa Kanisa la African Inland Church Tanzania  (AICT) Kilungule Makoka, Kimara Bw. Paul Luchemba alipokutana na waandishi wa habari kueleza mkakati wa kanisa hilo kuendesha harambee  kubwa ya  ujenzi wa kituo cha kuibua uwezo na vipaji tofauti vya watoto kitakachogharimu kiasi cha shilingi milioni 350.

Amesema  gharama za ujenzi wa kituo hicho kitakachojengwa mtaa wa Kilungule Makoka, Kimara zitahusisha uchimbaji wa kisima, ujenzi wa miundombinu ya maji pamoja na kukamilisha ujenzi wa kanisa la Kilungule lililopo Kimara.

Ameongeza kuwa lengo la kuwataka watanzania kushiriki katika harambee ya ujenzi wa kituo hicho linatokana na Kanisa hilo kuona idadi kubwa ya watoto katika  eneo la Kilungule Kimara k ambao wanahitaji msaada wa malezi na kufundishwa mbinu mbalimbali za kujitambua  pamoja na kuwepo kwa mkakati maalum wa kuibua vipaji vya watoto ili kujenga taifa lenye  maadili kuanzia ngazi ya familia.

Bw. Luchemba amefafanua kuwa kituo hicho kitakapokamilika kitakuwa na uwezo wa kuwahudumia watoto zaidi ya 500 kutoka eneo la Kilungule na maeneo mengine bila kubagua itikadi za kidini na kuongeza kuwa kituo hicho ni kwa ajili ya watoto wa Tanzania na kitakuwa na wataalam maalum wa masuala ya watoto watakaowapatia mafunzo  mbalimbali, ushauri pamoja na kuibua vipaji vyao.

“Ninawaomba watanzania wote kuunga mkono harambee ya ujenzi wa kituo hiki  cha pekee kitakachogharimu kiasi cha shilingi milioni 350 na kitakua na uwezo wa kuwajengea watoto ubunifu kutokana na vipaji vitakavyoibuliwa na wataalam waliobobea katika masuala ya wototo” amesema.

Aidha aidha amewaomba watanzania bila kujali maeneo wanayotoka kuchangia ujenzi wa kituo hicho kwa kuwasilisha michango yao makao makuu ya AICT – Dayosisi ya Pwani, Magomeni au kushiriki katika harambee kubwa itakayofanyika siku ya jumapili ya tarehe 14 mwezi huu katika kanisa la AICT mtaa wa Kilungule Makoka, ambapo mgeni rasmi katika harambee hiyo atakuwa mbunge wa Sengerema (CCM) Mh. William Ngeleja

No comments: