Tangazo

March 18, 2013

Tume ya Katiba: Ufafanuzi wa Tume kuhusu Mkazi wa Kudumu na mabadiliko ya tarehe ya Uchaguzi wa Wajumbe ngazi ya Kijiji na Mitaa

Mwenyekiti wa Tume, Jaji Warioba
Na Mwandishi Wetu
 
Tume ya Mabadiliko ya Katiba imewakumbusha wananchi wanaopenda kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya kutumia siku mbili zilizobaki kuwasilisha maombi yao kwa Maofisa Watendaji wa Vijiji na Mitaa na kusisitiza kuwa siku ya mwisho ya kuwasilisha maombi hayo ni  siku ya Jumatano, tarehe 20 Machi mwaka huu (2013).

Wananchi wanaopenda kuwa Wajumbe wa Mabaraza hayo wawasilishe maombi yao yakiwa na taarifa zifuatazo: Majina Kamili; Jinsi; Umri; Eneo analoishi kwenye Kijiji/Mtaa; Kiwango cha Elimu; na Kazi yake.
 
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Tume leo (Jumatatu, Machi 18, 2013), wananchi wamekumbushwa kuwa mwombaji anatakiwa kuwa na sifa zifuatazo: Awe ni Raia wa Tanzania na awe na umri wa miaka 18 au zaidi na awe na uwezo wa kusoma na kuandika.

Sifa nyingine ni pamoja na kuwa mkazi wa kudumu wa kijiji, mtaa au shehia husika na awe ni mtu mwenye hekima, busara na uadilifu na pia awe mtu mwenye uwezo wa kujieleza na kupambanua mambo.
 
Katika hatua nyingine, Tume hiyo inayoongozwa na Jaji Jospeh Warioba imefafanua kuhusu sifa ya ukazi wa kudumu kwa waombaji na kusema kuwa sifa hiyo haina maana kuwa mwananchi anapaswa kumiliki nyumba katika mtaa au kijiji husika.
 
"Tume inapenda kuwafahamisha wananchi kuwa mkazi wa kudumu ni mwananchi yeyote anayeishi katika mtaa au kijiji husika na sio lazima awe anamiliki nyumba katika mtaa au kijiji hicho," imesema sehemu ya taarifa hiyo iliyosambazwa kwa vyombo vya habari.
 
Kuhusu wananchi kuhakiki majina ya waombaji, Tume hiyo imewataka wananchi walioomba kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya kuhakiki majina katika orodha ya majina ya waombaji wote itakayobandikwa katika eneo la wazi au mbao za matangazo katika Mtaa, Kijiji au Shehia husika kwa siku saba kuanzia tarehe 22 hadi tarehe 28 mwezi machi mwaka huu.
 
Katika taarifa hiyo, Tume pia imesema imefanya mabadiliko madogo katika mwongozo wake (uliotolewa hivi karibuni) katika tarehe za vikao vya mitaa na vijiji vitakavyowachagua Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba. Kwa mujibu wa mwongozo uliotolewa na Tume mwezi uliopita, vikao hivi vilipaswa kufanyika kati ya tarehe 30 mwezi Machi mwaka huu (2013) na tarehe 3 Aprili mwaka huu (2013).

"Kwa mujibu wa mabadiliko mapya, vikao hivyo sasa vitafanyika kati ya tarehe 30 Machi mwaka huu (2013) hadi tarehe 5 Aprili mwaka huu (2013). Kwa msingi huu kila kijiji au mtaa kitachagua tarehe atika vikao hivyo, wananchi watapiga kura za siri kuwachagua wananchi wanne kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya," imeongeza sehemu ya taarifa hiyo.

Kufuatia mabadiliko haya, Tume imeongeza, Vikao Maalum vya Kamati za Maendeleo za Kata vya kuwachagua wajumbe wanne kutoka miongoni mwa wananchi waliochaguliwa na vijiji na mitaa navyo vimesogezwa mbele na sasa vitafanyika kati ya tarehe 7 Aprili mwaka huu (2013) na tarehe 10 Aprili mwaka huu (2013). Awali, vikao hivi vilipangwa kufanyika kati ya tarehe 5 Aprili mwaka huu (2013) na tarehe 9 Aprili mwaka huu (2013).

Tume inawaomba wananchi kushiriki na kuendesha mchakato wa kuwapata Wajumbe kwa amani na utulivu na kuzingatia mwongozo uliotolewa na tume.

No comments: