Tangazo

April 17, 2013

BREAKING NEWS: BI KIDUDE AFARIKI DUNIA

Habari zilizoifikia Blogu hii hivi punde ni kuwa Mwanamuziki mkongwe nchini wa muziki wa Taarabu, Fatuma Binti Baraka maarufu kwa jina la Bi. Kidude (pichani), amefariki dunia mchana huu huko Visiwani Zanzibar eneo la Bububu.

Daily Mitikasi Blog inaungana na waombolezaji na inawapa pole ndugu, jamaa, marafiki  na wanamuziki wote na wapenzi wa muziki nchini kufuatia msiba huu mzito.

Bwana alitoa Bwana ametwaa jina la Bwana lihimidiwe na ailaze roho ya marehemu Bi. Kidude mahala pema peponi Amina.

HISTORIA FUPI YA BI. KIDUDE
 FATMA binti Baraka 'Bi kidude' ni miongoni mwa wasanii wakongwe hapa nchini wenye historia ya kipekee. Licha ya kuwa na historia ya kipekee, msanii huyo mkongwe amejipatia umaarufu mkubwa ndani na nje ya nchi kupitia kazi yake ya sanaa.

Bikidude anaminika kwamba ndie msanii mkongwe kuliko msanii mwingine yoyote wa kike hapa nchini.

Msanii huyo ni muimbaji mwenye historia ya kipekee hapa nchini na kutokana na umahiri wake wa uimbaji na amefanikiwa kutembea nchi mbalimbali za Afrika, Ulaya na Asia kwa ajili ya kufanya kazi zake za muziki na kuitangaza taifa kwenye jumuia za kimataifa.

Katika siku za hivi karibuni, mkongwe huyo alikuwa akisumbuliwa na maradhi lakini kwa sasa hali yake inaendelea vizuri ingawa hajaanza kufanya shughuli zake za muziki.

Katika makala haya nitazungumzia historia fupi ya msanii huyo ambaye mwishoni mwa mwaka jana, serikali ilimtunukia nishani ya heshima kutokana na mchango wake mkubwa kwa taifa. Nishani hiyo alitunukiwa na Rais Jakaya Kikwete, Ikulu mjini Dar es Salaam.

Rais Kikwete alimtunuku Bikidude na wasanii wengine nishani ya sanaa na michezo ambayo hutolewa kwa wasanii na wanamichezo mashuhuri, ambao kazi zao za sanaa au michezo zimeipatia sifa kubwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Historia inaonyesha kwamba Bikidude ni mwimbaji wa muziki wa taarabu toka visiwani Zanzibar. Anaangaliwa kama malkia wa muziki wa taarab na unyago hapa nchini ambaye kipaji chake kiligunduliwa na kuimarishwa na mkongwe wa muziki wa aina hiyo Siti binti Saad kati ya miaka ya 1880 mpaka 1950.

Bikidude alizaliwa katika kijiji cha Mfagimaringo, akiwa ni mtoto wa mfanyabiashara wa nazi enzi za ukoloni nchini Zanzibar.

Mpaka sasa haijafahamika tarehe ya kuzaliwa ya bibi huyo kwasababu sehemu kubwa ya historia zinazo husu historia ya maisha yake hazioani na hivyo kuwepo na taarifa ambazo ni za kubuni.

Mwaka 2005, Bikidude alipewa tuzo ya heshima ya dunia WOMEX tuzo ambazo zilibuniwa mwaka 1999 na mbazo wanazawadiwa watu ambao wamepata mafanikio makubwa katika muziki au wametoa mchango mkubwa katika muziki, umuhimu wa mtu katika jamii na hata , mafanikio ya kibiashara na kwa upande wake ilitokana na mchango wake katika muziki na utamaduni wa Zanzibar.

Akiwa mdogo, Bikidude alisifiwa sana kutokana na sauti yake na katika miaka ya 1920 alianza kuimba na vikundi mbalimbali vya kiutamaduni.

Alipokuwa na umri wa miaka 13, baada ya kulazimishwa kuolewa aliamua kutoroaka na kuelekea Tanzania Bara.

Bikidude ni moja ya waimbaji wakongwe waliozunguka nchi zote za Afrika Mashariki akiimba taarab ambapo alitembelea miji mikubwa ya ukanda wa pwani pamoja na bara upande wa ziwa Victoria na Tanganyika.

Mwaka 1930, alirejea Dar es Salaam na kujiunga na kikundi cha Egyptian Taarab ambacho alidumu nacho kwa miaka mingi.

Katika miaka ya 1940 alirejea Zanzibar na kujenga nyumba yake iliyokuwa ya matope na kuanza maisha mapya hapo.

Alikuwa maarufu sana kwa shughuli za unyago ambazo ziliwaandaa masichana wadogo kuelekea katika ubalehe na kuingia katika maisha ya utu uzima.

Ni mtaalamu wa mambo hayo ya mila kongwe akifanya hivyo kwa wasichana akitumia mafunzo ya kitamaduni kuwaelekeza wasichana namna ya kuishi na waume zao na kuepuka migongano ya kifamilia na unyanyasaji wa mapenzi.

Sifa na jina la Bikidude lilikuwa na kusifika katika jamii yote ya Zanzibari na kuwa kielelezo cha utalii wa visiwa hivyo vya karafuu ambapo hoteli mbalimbali kubwa na zenye hadhi ya juu visiwani humo zimekuwa zikizipa majina migahawa ya hoteli jina la Bikidude, mfano 236 Hurumzi inatumia jina la mgahawa wake jina la 'Kidude'.

Moja ya nyimbo zake ambazo zilitamba na kumpatia umaarufu mkubwa mkongwe huyo ni Muhogo wa Jang'ombe ambao ulikamata kwenye mwambao wa Afrika Mashariki.
Bikidude ni hazina kubwa na mwalimu mzuri kwani inasemekana wasanii wengi wamepata mafunzo kutoka kwake.

Pamoja na umahiri wa msanii huyo lakini hajawahi kukumbwa na kashfa yoyote hadi sasa hivyo amekuwa na historia ya kipekee tofauti na wasanii wa sasa.

Wasanii wengine waliopewa nishani hiyo ni pamoja na kiongozi wa bendi ya muziki wa dansi ya Msondo Ngoma, Muhidin Gurumo, kiongozi wa zamani wa bendi ya Dar es Salaam International, marehemu Marijani Rajabu, aliyekuwa msanii maarufu wa maigizo na filamu nchini, marehemu Fundi Saidi 'Mzee Kipara' na mwanariadha mkongwe, John Steven Akwari.

Gurumo, Bi Kidude na Akwari walihudhuria hafla hiyo ya kuvishwa nishani zao na Rais Kikwete wakati nishani za Marijani na Mzee Kipara zilipokelewa na watoto wao.

Bikidude hakuweza kwenda eneo la kupokea nishani kutokana na hali ya afya yake kutokuwa nzuri. Ilibidi Rais Kikwete amfuate mahali alipokuwa ameketi na kumtunukia nishani yake.

Bikidude, amedumu kwenye fani ya uimbaji kwa zaidi ya nusu karne na kwa sasa ni msanii pekee wa taarab mwenye sifa zilizotukuka kutokana na ukongwe wake na umahiri wake katika kuimba taarab.

Gurumo alianza muziki 1960 na kushiriki katika bendi mbalimbali kama vile Nuta, Juwata, Ottu, Atomic Jacc, Kiko Kids, Jamhuri Jazz, Kilwa Jazz, Rufiji Jazz, Mlimani Park, Msondo Ngoma.

Ametunga nyimbo nyingi zinazoelimisha jamii kuhusu kuheshimu na kufanyakazi kwa juhudi na maarifa, kulinda uhuru wa nchi, kudumisha usawa, haki na amani na kuwaasa wazazi kutimiza wajibu wao kwa kulea watoto na vijana kutimiza wajibu wao.

Marehemu Marijani, maarufu kama Jabali la Muziki, alifariki dunia mwaka 1995. Alitoa mchango mkubwa katika tasnia ya muziki, alishiriki kutunga na kurekodi nyimbo zaidi ya 103, ambazo zilirekodiwa RTD, nyimbo zake zilikuwa na mafunzo mengi kwa jamii na zinaendelea kupigwa katika vituo mbalimbali vya redio nchini.

Mzee Kipara mwaka 1962 alijiunga na waigizaji wa Redio Tanzania, pia ameshiriki maigizo na tamthilia nyingi za kwenye televisheni kama vile Hujafa hujaumbifa, Fukuto, Radi, Gharika, Tufani na Tetemo.

Mzee Akwari aliweka historia ya pekee nchini mwaka 1968 pale aliposhiriki mbio za marathoni za Olimpiki na kuumia goti na kutoka malengelenge, lakini aliushangaza ulimwengu alipoendelea na kumaliza mbio hizo. Alipoulizwa, alisema 'mimi sikutumwa kuja kuanza mbio, nimetumwa kumaliza mbio'. Maneno hayo yamekuwa yakitumika kama mifano duniani.

No comments: