Mke wa Rais Mama Salma Kikwete (pichani), ametunukiwa tuzo ya heshima na Chama cha uzazi na malezi bora Tanzania (UMATI) kutokana na kazi anazozifanya za kutoa elimu kwa mtoto wa kike na kuhakikisha kuwa vifo vya kina mama wajawazito na watoto vinapungua hapa nchini.
Aidha Mama Kikwete pia amekabibidhiwa kadi namba moja ya kuwa mwanachama wa maisha wa UMATI.
Hafla hiyo ya kumkabidhi tuzo Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) imeenda sambamba na ufunguzi wa mkutano mkuu wa mwaka wa siku mbili wa UMATI unaofanyika katika hoteli ya Blue Pearl jijini Dar es Salaam .
Akikabidhi tuzo hiyo Makamu Mwenyekiti wa UMATI Charles Mugondo alisema kuwa wameamua kumpa tuzo hiyo ili kuonyesha kuwa ni mwenzao kutokana na kazi anazozifanya za kuisaidia jamii ya kitanzania.
“Tumeona umuhimu wa kazi unazozifanya, hivyo basi tumeamua kukupatia tuzo hii ambayo ni ushahidi tosha wa kuonyesha kuwa unawajali watoto wa kike nchini tunakupongeza kwa hilo na tunakuomba uendelee zaidi kuwasaidia vijana hasa wasichana wa Tanzania,” alisema Mugondo.
Akiongea mara baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo Mama Kikwete alishukuru na kusema kuwa hakutegemea kupewa tuzo lakini anaamini kuwa wameangalia vigezo vya utoaji wa tuzo na kuona kuwa anastahili kupewa .
“Huwa napenda kunukuu maneno ya Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete kuwa Nyumba tunayoishi ni moja hakuna haja ya kugombania fito hii inamaanisha kuwa kazi tunayoifanya ni moja hivyo basi tunakatikiwa kushirikiana ili tuweze kuwahudumia wananchi” , alisema Mama Kikwete.
UMATI ni chimbuko la huduma ya uzazi wa mpango nchini hususani katika huduma za afya ya uzazi na harakati za kumkomboa na kumwezesha mtoto wa kike ili aweze kujitambua na kujimudu katika maisha yake.
No comments:
Post a Comment