Tangazo

April 25, 2013

WAJUA KUWA ‘Room to Read’ NI SHIRIKA LINALOSAIDIA KUBORESHA NA KUINUA KIWANGO CHA ELIMU NCHINI TANZANIA


Moja ya madarasa katika Shule ya Msingi Dihinda iliyopo kata ya Mvomero ambalo limejengwa na Shirika la Room to Read.

*Ni shirika pekee lenye mradi wa kuimarisha uwezo wa kusoma, kuandika na kuhesabu kwa watoto.

*Tayari limefanikisha ujenzi wa vyumba vya madarasa 60 katika shule za msingi 15 wilayani Mvomero.

*Sasa laelekeza nguvu zake wilayani Bagamoyo na kukusudia kujenga madarasa 40 na maktaba 20.

Room to Read ni Shirika la Kimataifa lisilo la kibiashara linalojishughulisha na kuboresha na kuinua elimu kwa kujenga vyumba vya madarasa na maktaba pamoja na kusambaza vitabu vya kujisomea wanafunzi sambamba na kuhamasisha usawa wa kijinsia kwa kuwasaidia wanafunzi wa kike waliopata masomo na kuwainua kitaaluma katika nchi kadhaa duniani.

Kwa sasa shirika hili limefungua tawi hapa nchini Tanzania likiwa na program kadhaa za kusaidia kuboresha na kuinua kiwango cha elimu katika shule za msingi.

Mo blog ilipata fursa ya kuzungumza na Mkurugenzi Mkazi wa shirika hilo nchini Tanzania, ambaye alitoa maelezo ya kina kuanzia historia ya shirika hilo, kuanza kwa shughuli zake hapa nchini, mafanikio yaliyopatikana na hatimaye mikakati ya shirika hilo katika siku za usoni.

Theodory Mwalongo ni Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Room To Read ambalo ni Shirika la Kimataifa lenye Makao yake makuu huko San Francisco nchini Marekani ambako lilianzishwa mwaka 2000.
Baadhi ya Wanafunzi wilayani Mvvomero wakijisomea katika moja ya Maktaba iliyojengwa na Shirika la Room to Read Tanzania.

Akizungumzia shirika hilo Theodory Mwalongo anasimulia…………………!!

Lilianzia huko nchini Nepal na mwanzilishi wake alikuwa anaitwa John Wood ambaye alikuwa na Mkurugenzi wa Masoko wa Shirika la Microsoft na katika shughuli zake aliweza kupita Nepal akaona mahitaji makubwa ya watoto ya vitabu.

Akaamua kuacha kazi yake ya kutangaza biashara ya kompyuta huko Asia akaamua kurudi Marekani akawa anakusanya vitabu na kuvipeleka Nepal, lakini alipopeleka vitabu vile ikawa hakuna mahali pa kuviweka kwa sababu hakukuwa na madarasa hali ilikuwa ni mbaya sana.

Basi akaanzisha wazo la kujenga kwanza madarasa, kujenga vyumba vya maktaba na baadae kupeleka vitabu.

Basi hatimaye shirika limeena katika nchi nyingi ambapo kwa sasa Room To Read inafanya kazi zake katika nchi 10 duniani na kwa hapa Afrika ipo katika nchi 3 ambazo ni Afrika Kusini, Zambia na Tanzania.

Hapa Tanzania shirika limepata usajili wake mwezi wa 9 mwaka 2010 lakini rasmi limeanza shughuli zake mwaka 2011 kwa kazi za kuboresha elimu ya msingi.

Shirika lina programs nne (4); ya kwanza ni kuboresha miundo mbinu ya shule tukimaanisha ujenzi au ukarabati wa vyumba vya madarasa, kuwawezesha watoto kupata mahali pazuri pa kujifunzia lakini waalimu pia mahali pazuri pa kufundishia.
Jengo lililokamilika la shule ya msingi Kanga Wilayani Mvomero tarafa ya Turiani ambalo limejengwa na shirika la Kimataifa la Room to Read.

Sambamba na program hiyo ni uanzishaji wa maktaba katika shule za msingi. Maktaba hizi zinawekwa vitabu vya hadithi vya watoto na vitabu vya maarifa mengine kama vile mazingira, jinsia, afya, haki za binadamu na kadhalika.

Kwa hiyo katika uanzishaji wa maktaba tuna program ya tatu ambayo inalenga uchapaji wa vitabu vya hadithi. Kwa hiyo tunagundua watunzi mahiri na wachoraji wanatunga vitabu vya hadithi za watoto na kuviweka katika maktaba hizo.

Pia katika program hii ya kuboresha elimu ya msingi, tuna program ya kushirikiana na walimu katika shule za msingi, waratibu kata na maafisa elimu wa shule za msingi kuimarisha uwezo wa kusoma, kuandika na kuhesabu kwa watoto.
Mwanafunzi akijisomea katika maktaba mpya ya kisasa na yenye hewa safi iliyojengwa na shirika la Room to Read.

Hivyo hizi program 4 nilizozitaja yaani kuboresha miundo mbinu katika shule za msingi, uanzishwaji wa maktaba, kuboresha kusoma, kuandika na kuhesabu na kuchapisha vitabu kunalenga katika shule za msingi tu. Lakini tuna program moja kubwa ambayo inalenga kuwawezesha wasichana waliokosa kwenda elimu ya sekondari kuendelea na masomo.

Tuna maeneo matatu, kwa kuwasaidia wasichana ambao wametoka katika familia ambazo zina kipato cha chini kuwalipia ada na mahitaji mengine. Lakini pia kusaidiana na shule husika kuwasaidia wasichana kuwainua kitaaluma, wale ambao uwezo wao wa kufanya vizuri katika masomo uko chini, basi Room To Read inashirikiana na waalimu kuweka mikakati ya namna ya kuwainua kufanya vizuri katika masomo.

Na tatu kuna program ya kuwasaidia Stadi za maisha kuwawezesha wajitambue, waweze kufanya maamuzi sahihi na wajue ni kwa nini wako shuleni. Hivyo basi tungesema tuna program kuu mbili, kuimarisha elimu ya msingi na program ya wasichana katika sekondari.
Pichani ni Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Room to Read Tanzania Bw. Theodory Mwalongo akizungumza na baadhi ya wanafunzi wilayani Mvomero wakati wa kukabidhi majengo ya Maktaba za kujisomea pamoja na madarasa.
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Room to Read Tanzania Bw. Theodory Mwalongo akisoma hotuba yake katika sherehe za kukabidhi majengo ya madarasa na Maktaba katika Wilaya ya Mvomero tarafa ya Turiani.

Mwalongo anaendelea kutueleza Room to Read kwa Tanzania limefanya nini…………………?

Sasa katika Tanzania baada ya kupata usajili tulianza katika katika wilaya ya Mvomero katika tarafa ya Turiani.

Katika kukamilisha hizo program tulizozitaja hapo juu, kwa mwaka 2012 tuliweza kujenga madarasa 60 katika shule za msingi 15. Katika madarasa hayo 60, vyumba 45 ni vya kusomea darasa la kwanza, la pili hadi la tatu na vyumba 15 vilijengwa maalum kwa ajili ya kuanzishwa maktaba.

Mradi huu mkubwa ambao uligharimu karibu shilingi bilioni moja na laki tano (1.5bn) tulishaka kabidhi serikalini, kwa serikali ya wilaya ya Mvomero tarehe 22 mwezi Machi katika sherehe kubwa ya kufana ambapo Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Ndugu Anthony Mtaka ndio alikuwa mgeni rasmi katika makabidhiano hayo.

Madarasa hayo yameaanza kutumika tayari na maktaba hizo zinatumika na wananchi wamefurahia sana kitendo hiki. Kwanza tumepunguza msongamano mkubwa sana katika madarasa yale kwa sababu kabla ya hapo unakuta chumba kimoja cha darasa kina wanafunzi zaidi ya 60 lakini sasa angalao tumepunguza msongamano huo.
Wanafunzi wa shule ya msingi wilayani Mvomero tarafa ya Turiani wakiimba na kufurahia baada ya kukabidhiwa rasmi darasa zuri lenye hewa safi pamoja madawati mapya lililojengwa na shirika la Room to Read.

Lakini kikubwa ni kuwa kwa mara ya kwanza katika historia ya maeneo yale ni shule kuwa na maktaba, watoto wanafurahia sana kutumia vyumba vile vya kujisomea kwa sababu kuna vitabu vya hadithi na kadhalika. 

Walimu nao wamepata unafuu mkubwa wa kuwa na nafasi za kuweza kufundisha. Lakini pia halmashauri ya wilaya imelipokea vizuri kwamba kwa kweli tumepunguza mzigo mkubwa ambao halmashauri inapambana nao kujenga vyumba vya madarasa.

Naweza kusema Room To Read ipo hapa Tanzania kusaidiana na serikali na wadau wengine kuinua ubora wa elimu hapa Tanzania.

Sasa hivi tumeanza katika mkoa wa Pwani ambako tutaanza na wilaya ya Bagamoyo, ambako mwaka huu tunategemea kuzifikia shule 20 ambapo tunategemea kujenga vyumba vya madarasa 40 na vyumba vya maktaba 20.

Tutakuwa na program ya kuboresha wasichana na huo mradi wa kusaidia watoto kujua kusoma na kuandika.
Hii ndio hali halisi ya baadhi ya madarasa katika shule za wilayani Mvomero tarafa ya Turiani hapo awali.

Mkurugenzi Mwalongo wa Room to Read hakusita kutoa rai kwa serikali………………..!!!

Rai yangu ni kuiomba serikali kushirikiana na sisi kuhamasisha wananchi waweze kuchangia fursa ambazo ziko ndani ya uwezo wao, kama vile kuchangia mchanga, mawe, matofali hata nguvu kazi, lakini pia halmashauri ishirikiane na sisi kuhakikisha majengo yake yanakuwa katika ubora unaotakiwa na shirika liweze kufuata viwango vya serikali vilivyowekwa.

Naamini kwa mshikamano huo wa serikali, wananchi na sisi tunaweza tukasaidia kuboresha elimu katika Tanzania.
 

No comments: