Tangazo

May 10, 2013

Mama Salma Kikwete awataka wazazi kutobagua watoto wao katika ufanyaji wa kazi za nyumbani

Mlezi wa Tanzania Girl Guides ambaye pia ni Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akiongea na viongozi wa Chama hicho kwenye Makao Makuu yao huko Mwananyamala wakati alipowatembelea tarehe 10.5.2013. PICHA NA JOHN LUKUWI
Na Anna Nkinda – Maelezo

10/5/2013 Wazazi nchini wametakiwa kuwafundisha watoto wao kazi zote za nyumbani bila ya kuwabagua kwamba  hawa ni watoto wa kike na hawa ni watoto wa kiume hiyo itawasaidia kuweza kujitegemea hasa wanapokuwa katika mazingira ya tofauti na nyumbani.

Wito huo umetolewa leo na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete alipotembelea ofisi za makao makuu ya Chama cha Girls Guide zilizopo Mwananyamala  jijini Dar es Salaam.

Mama Kikwete ambaye pia ni Mlezi wa chama hicho alisema kuwa  hivi sasa wanawake  wanatakiwa kuondokana  na mfumo dume kuwa ukiwa na watoto wa kike na wa kiume ndani ya nyumba  kazi zote zinatakiwa kufanywa na mtoto wa kike pekee.

“Mzazi unatakiwa kuhakikisha kuwa watoto wako bila ya kuangalia jinsia wanafanya kazi sawa sawa  kama ni kupika leo iwe zamu ya huyu na kesho zamu ya mwingine  hii itamsaidia mtoto wa kiume  akienda shule ya bweni kukumbuka kuwa nyumbani nilikuwa naosha kikombe, nadeki nyumba, nafua nguo, nashona kifungo na kuweza kufanya mwenyewe.

Lakini leo hii mtoto wa darasa la saba hawezi kufanya kazi yoyote ya nyumbani  kwani hata mama yake naye hana  muda wa kumfundisha”, alisema Mama Kikwete.

Alisema kuwa kama  wakiwafundisha watoto vizuri kutokana na muongozo uliopo katika madarasa ya boy skauti na girl guide watakuwa wamewakomboa  hata kama siyo wote lakini wale wachache ambao hawakupata mafunzo nyumbani watapata  mazingira ambayo yatawasaidia  kujitegemea katika maisha yao.

Kwa upande wake Grace Makenya ambaye ni mdhamini wa Chama alimshukuru Mama Kikwete kwa kuwatembelea na kusema kuwa watoto wengi ambao ni wanachama wa gilrs uides wameweza kufanya vizuri katika mitihani yao ya darasa la saba na wanawake walioolewa wameweza kuzitunza ndoa zao vizuri hii ni kutokana na mafunzo wanayowapatia.

Makenya alisema kuwa miradi waliyonayo ni jiko la kutumia mionzi ya jua, hosteli kwa shule za Sekondari za kutwa na mradi wa lishe bora kwa watoto wenye utapiamlo, afya ya uzazi na maambukizi mapya ya Virusi Vya Ukimwi (VVU), mimba zisizotarajiwa kwa wasichana wadogo na utoaji wa elimu ya Ukimwi kwa jamii.

Chama hicho ambacho kimeenea  Dunia nzima hapa nchini kilianza mwaka  1928 huku kikiwa na dira ya kuwa na  wasichana ambao wanauelewa wa matukio ya kitaifa na ulimwengu, wenye kujiamini na kujitegemea na kuwa tayari kuhudumia jamii na wenye hamu ya kufanya kazi na watu wengine.

No comments: