Tangazo

June 14, 2013

BURIANI LANGA KILEO


Msanii wa Muziki wa Kizazi Kipya ambaye ni chimbuko la Coca-Cola Pop Star mwaka 2004, Langa Kileo (28) amefariki dunia jana.

Taarifa zilizo ifikia Daily Mitikasi Blog zinaaarifu kuwa Langa amefikwa na umauti katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alikokuwa amelazwa kwa Matibabu.

Chanzo cha taarifa hiyo kinaeleza kuwa Marehemu Langa alikuwa amelazwa hospitalini hapo kufuatia Malaria kali iliyomshika na kukimbizwa Hospitalini hapo kwa matibabu zaidi.

Langa alishiriki shindano la Pop Star akiwa na wenzake wengine wawili Sara Kaisi 'Shaa' na Witness Mwaijaga 'Witness' na waliunda kundi lilioenda kwa jina la Wakilisha.

Wakiwa na kundi la Wakilisha Marehemu langa na Wenzake hao walitamba sana kwa nyimbio mbili za 'Unaniacha Hoi' na 'Kiswanglish'.

Baadaye Sarah Kaisi (Shaa) alijitoa. Lakini Langa na Witness walifyatua kibao cha ‘No Chorus’.

Baada ya hapo Langa alifyatua kibao chake cha kwanza akiwa mwanamuziki binafsi, ‘Matawi ya Juu’ ambacho Dj John Dilinga (JD) aliwahi kuelezea ni moja ya kazi nzuri kutoka kwake, licha ya dosari za matumizi ya lugha.

Kibao chake hicho cha  'Matawi ya Juu' na video ya wimbo huo ikaingizwa katika mashindano ya MTV Base na baade kushinda tuzo ya Kisima nchini Kenya.

Aliwahi fanya kazi na wasanii mbalimbali wa nchini kama Fid Q na nje ya nchi kama vile kundi la Necessary Noise, Naaziz na Wyre (Kevin Wyre).

maisha ya Langa kimuziki yalianza kuporomoka pale alipoachia albam yake ya 'Langa' na kushindwa kuuza baada ya kukataliwa na wasambazaji na kuamua kujiingiza katika maisha ya uteja ya utumiaji wa madawa ya kelevya.

Baada ya jitihada za familia yake aliweza kuondoka katika maisha hayo ya uteja na alipo toka aliachia nyimbo za 'Bombokiata' na 'Mteja Aliyepata Nafuu'.

Langa alizaliwa mnano mwaka 1985 jijini Dar es Salaam akiwa tunda la wanandoa Vanessa Kimei na mumewe Mengisen Kileo.

Alipata elimu ya msingi katika shule ya Msingi Olympio na baade  Sekondari ya Loyola, zote za jijini Dar es Salaam.

Akiwa kidato cha pili alihamishiwa Kampala, Uganda katika Shule ya Vienna na baadaye Shule ya Hillside International Academy, huko huko Uganda. Baadaye alirejea nchini na kujiunga na masomo ya Stashahada ya Masoko katika Chuo cha Biashara Dar es Salaam (CBE), Kampasi ya Dodoma.

 MJUE MAREHEMU LANGA KILEO 'LANGA'

Ni mtaalamu na mwanamuziki stadi wa Hip Hop nchini aliyeweka wazi kuathiriwa na matumizi ya dawa za kulevya.

 Ili kuonyesha anachukizwa, Langa alilieleza jarida moja la burudani kwamba anakusudia kuanzisha Taasisi ya kupiga vita matumizi ya dawa za kulevya.

Alisema matumizi ya dawa hizo yaliathiri shughuli zake za muziki na hakuwa na jambo lolote endelevu katika muziki wake.

Kimuziki Langa alianzia kundi la Wakilisha akiwa na Witness Mwaijega na Sarah Kaisi, ambapo walikuwa washiriki wa mashindano ya muziki ya Cocacola Pop stars, yaliyofanyika nchini Afrika Kusini.

Wakiwa na kundi hilo walifanikiwa kufyatua kibao cha ‘Hoi’, ambacho kiliteka wapenzi wa muziki.

Baadaye Sarah Kaisi (Shaa) alijitoa. Lakini Langa na Witness walifyatua kibao cha ‘No Chorus’.

Baada ya hapo Langa alifyatua kibao chake cha kwanza akiwa mwanamuziki binafsi, ‘Matawi ya Juu’ ambacho Dj John Dilinga (JD) aliwahi kuelezea ni moja ya kazi nzuri kutoka kwake, licha ya dosari za matumizi ya lugha.

Hata hivyo Langa alionyesha yeye ni bora na ana kipaji cha muziki. Amekuwa shujaa kwa kuendesha kampeni kali za kupinga matumizi ya dawa za kulevya kwa vijana. Serikali inapaswa kusaidia juhudi zake pamoja.

Huyu ni mmoja wa matunda ya shindano la muziki la Coca-Cola Pop Stars mwaka 2004 ambalo washindi wake waliounda kundi la Wakilisha.  Mbali ya Langa, wengine ni Sarah Kaisi `Shaa’ na Witness Mwaijaga `Witness’. Huo ndio uliokuwa mwanzo wa kung’ara kisanii kwa wakali hao, ingawa kwa sasa kundi hilo limesambaratika, kila mmoja akitamba kivyake.

Lakini kwa bahati mbaya, mmoja wao, Langa kwa miaka ya hivi karibuni hakusikika kabisa, jambo lililomlazimu mwandishi wa makala haya kumtafuta sababu za ukimya wake.

Haikuwa kazi rahisi, lakini hatimaye Langa alipatikana na bila kutafuna maneno alisema kwamba, alishindwa kufanya kazi baada ya kuwa `teja’ aliyekubuhu.

Yaani alizama katika matumizi ya dawa za kulevya kiasi cha kupoteza kabisa mwelekeo si wa kisanii pekee, bali hata kimaisha.

“Siyo siri, kilichokuwa kimenifikisha katika hali hiyo ni dawa za kulevya. Kwa miaka mitano nilitumia sana Cocaine, Heroin, bangi na pombe. Namshukuru Mungu sasa nimerejea katika hali yangu.

“Siamini kama nimenusurika kwa sababu madawa yalinitesa, nikafanya mengi ya ajabu yaliyoichukiza familia yangu na marafiki ikiwa pamoja na kuwa mwizi na mkabaji mitaani na nyakati za usiku,” anasema Langa ambaye kundi lao la Wakilisha lilitamba na nyimbo kama `Unaniacha Hoi’ na `Kiswanglish’.

Anaeleza kwamba, kwake hayo ndiyo aliyoyaona maisha yanayomfaa, akidai awali alikuwa amechoshwa kuishi kwa masharti kutoka kwa wazazi wake waliokuwa wanampa mwongozo wa maisha, lakini bila kujua akadhani `anachungwa’.

Kwamba, umaarufu na ngekewa ya kuzishika pesa katika umri mdogo kupitia muziki vilimtia kiburi zaidi, na hivyo kuamua kujitenga kabisa na familia yake iliyomlea kwa mapenzi mazito.

“Niliamini naweza kujitegemea kupitia kazi yangu ya muziki, nikajichanganya mtaani,” anasema kijana huyo aliyetoa kibao chake cha kwanza, Matawi ya Juu mara baada ya kusambaratika kwa kundi la Wakilisha kutokana na kila mmoja kuamua kujitegemea kimuziki. Na kweli, Matawi ya Juu ilidhihirisha kuwa Langa ni moto wa kuotea mbali katika fani. Aliweza kusimama kwa miguu yake na kutikisa.

Mwenyewe anasema: “Jina hilo la Matawi ya Juu lilidhihirisha hivyo pale video ya kibao hicho ilipotajwa kuwania Tuzo za MTV Base kwa upande wa hapa Bongo miaka michache iliyopita, kisha kutwaa Tuzo ya Kisima nchini Kenya.

“Moto huo uliwafanya baadhi ya wasanii wakongwe katika gemu ya Bongo Fleva kunitafuta na kunipa majukumu ya kushiriki katika kazi zao, ikiwemo Chagua Moja ya Farid Kubanda `Fid Q’.

“Baada ya kuona wakongwe wamekubali vitu vyangu na kuanza kunishirikisha…nikapata pia safari za nje ya nchi. Huko Nairobi (Kenya) niliweza kufanya kazi na vichwa vikali vinavyounda Kundi la Necessary Noise, Naaziz na Wyre (Kevin Wyre).

Anasema mafanikio hayo yalimtuma kufyatua albamu yake ya kwanza aliyoipa jina la Langa, akiamini itampaisha zaidi kimaisha na kimuziki. Hata hivyo, mambo yalikwenda kinyume. Anasema alipoipeleka sokoni, wauzaji wakubwa waliigomea, hivyo kumpa wakati mgumu wa kuwaza na hatimaye kujikuta akiongeza kasi ya matumizi ya dawa za kulevya.

Siyo siri, kugoma kwa albamu yangu sokoni kulichangia kasi ya kutumia dawa za kulevya…niliona ni njia pekee ya kuondoa mawazo kwa sababu kazi iligoma, na home (nyumbani) nilishaharibu.

Sikufanya tena kazi kwa umakini na kila kazi niliyoitia haikufanya vizuri….” Anasema kwamba, baada ya mambo kumwendea mrama, ndipo alipoanza kuiba vitu nyumbani kwao kwa lengo la kuviuza na inapotokea amekosa, alidiriki hata kupiga debe katika vituo vya mabasi ili mradi apate fedha za kununua `unga’.

Haikuishia hapo, kwani anasema alijiingiza katika kundi la wahuni waliojihusisha na wizi na ujambazi. “Kwa ujumla nilipoteza mwelekeo. Maisha yangu yakawa ya kutembea na kisu kama kitendea kazi changu katika wizi,” anasema huku akitikisa kichwa kama ishara ya kujutia matendo aliyoyafanya kwa msukumo wa madawa ya kulevya. Anakumbuka akiwa mtumwa wa `unga’, aliingia katika mikasa kadhaa ikiwa pamoja na kupigana na polisi baada ya kunaswa na dawa hizo haramu.

Katika wizi, chochote alichokikuta mbele yake kilikuwa halali. Anasema alikwapua vitu magengeni, madukani na hata magari yaliyoegesha vibaya alinyofoa vioo na mashine zinazosaidia kupandisha na kushusha vioo ndani ya gari.

“Ni matukio ya aibu. Yanasikitisha…,” anasema Langa anayedokeza kwamba, akiwa mtumiaji wa `unga’, alikuwa anakutana na wasanii na watu wengine mashuhuri. Hata hivyo anakataa kuwataja, akidai ni siri yake. `Ufufuo’ wa Langa kutoka katika lindi la mateso ya dawa za kulevya ulipatikana kuanzia Machi mwaka huu, baada ya familia yake kumpeleka kijana wao kwa tiba maalumu ya kuachana na matumizi ya `madudu’ hayo. Na kweli, elimu imemwingia na kujikuta akirejea ufahamu wake wa kawaida.

Ametangaza kuachana na `unga’, pombe, sigara na badala yake amejikita zaidi katika mazoezi ya kurudisha mwili wake katika hali ya kawaida. Aidha, amekata shauri la kuirudia fani yake na tayari ana vitu vipya, Bombokiata na Mteja Aliyepata Nafuu.

Anasisitiza kwamba, kutokana na mateso aliyoyapata, anakusudia katika siku za baadaye afungue kituo chake cha tiba ya dawa za kulevya ili aweze kuwaokoa vijana wengine wanaoangamia kutokana na matumizi ya dawa hizo haramu zinazopigwa vita karibu kote duniani. “Nimenusurika, namshukuru Mungu.

Nami najipanga kutaka kuwasaidia wengine waachane na mateso ya dawa za kulevya. Pia nichukue fursa hii kuwaomba msamaha wote niliowakosea kwa namna moja ama nyingine wakati nikiwa `teja’,” anasema Langa, kijana mwenye umri wa miaka 25.

Je, historia ya maisha ya Langa ikoje? Anasema Desemba mwaka 1985 jijini Dar es Salaam akiwa tunda la wanandoa Vanessa Kimei na mumewe Mengisen Kileo. Alisoma Shule ya Msingi Olympio na Sekondari ya Loyola, zote za jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, akiwa kidato cha pili alihamishiwa Kampala, Uganda katika Shule ya Vienna na baadaye Shule ya Hillside International Academy, huko huko Uganda. Baadaye alirejea nchini na kujiunga na masomo ya Stashahada ya Masoko katika Chuo cha Biashara Dar es Salaam (CBE), Kampasi ya Dodoma.

Huyo ndiye Langa Kileo msanii wa muziki wa kizazi kipya ambaye baada ya kulewa umaarufu na kujikita katika matumizi ya dawa za kulevya, ameibuka na kujutia `ujanja pori’, sasa akitaka kujiingiza katika kampeni ya kuwaokoa vijana wengine waliozama katika `unga’.

 Anakusudia pia kurudi darasani kujiendeleza na masomo ya elimu ya juu. Je, atafanikiwa? Kwa hakika, hili ni jambo la kusubiri na kuona.

1 comment:

Erick Mchau said...

Stori nzuri na yenye mafunzo. Pumzika kwa amani Langa Kileo