Tangazo

July 10, 2013

VIKUNDI VYA POLISI JAMII HANDENI VYAPATIWA MISAADA

Mkuu wa Polisi Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga SP. Zuberi Chembera (kushoto), akikabidhi tochi, betri na filimbi kwa vikundi vya Polisi Jamii na Uluinzi Shirikishi wilayani Handeni ili ziwasaidie katika shughuli za ulinzi.Tochi hizo ni msaada kutoka kwa  wafanyabiasha mbalimbali wilayani humo.   
*******************************
Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi-Handeni
 
Juhudi zinazochukuliwa na mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Inspekta Jenerali Saidi Mwema, za kutoa elimu juu ya Sera ya Polisi Jamii na Ulinzi Shikishi nchini kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali zinazaa matunda karibu kila pembe ya nchi yetu.
 
Hayo yamedhihirika baada ya Wafanyabiashara wilayani Handeni katika mkoa wa Tanga, kuamua kwa hiari yao kuwachangia Polisi kwa vifaa ambavyo navyo vinatolewa kwa vikundi vya Polisi Jamii wilayani humo.
 
Wafanyabiashara hao wametoa vitendea kazi kama vile, tochi na betrii ili ziwasaidie Polisi lakini pia Mkuu wa polisi wilayani Handeni SP Zuberi Chembera, kwa kujua umuhimu wa Polisi Jamii naye ameamua kutoa msaada huo kwa vikundi mbalimbali vinavyojishughulisha na ulinzi mitaani.
 
Akizungumza katika hafla fupi ya kukabidhi vifaa hivyo, Mkuu huyo wa Polisi wilayani handeni amesema kuwa ameamua kukabidhi sehemu ya misaada hiyo kwa kutambua kuwa Vikundi vya Ulinzi ni msaada mkubwa kwa Jeshi la Polisi katika kukomesha uhalifu nchini.
 
Amesema ofisi yake itajitahidi kutoa kila aina ya msaada kwa vikundi hivyo vya Polisi Jamii ili navyo viweze kuimarisha na kudumisha usalama katika maeneo yao .
 
Aidha SP Chembera ametoa wito kwa wananchi mbalimbali wilayani humo pia kuwaunga mkono katika kuvisaidia vikundi hivyo ambavyo amesema ni muhimu kuwepo ndani ya Jamii zetu katika kulinda usalama wa watu na mali zao kama ilivyo kwa jeshi la Polisi.

No comments: