Tangazo

September 25, 2013

MAMA KIKWETE AKIOMBA CHUO KIKUU CHA MONMOUTH MAREKANI KUFUNDISHA LUGHA YA KISWAHILI

Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akiongoza kikao cha pamoja kuhusu mashirikiano kati ya Taasisi ya WAMA na Chuo Kikuu cha Monmouth hasa katika masuala ya kuwaongezea uwezo wauguzi na wakunga. Mama Salma Kikwete aliongozana na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dr. Hussein Mwinyi. PICHA/JOHN LUKUWI 
****************************
Na Anna Nkinda – New York

Mke wa Rais Mama Salma Kikwete amekiomba chuo kikuu cha Monmouth cha mjini New Jersey nchini Marekani  kufundisha wanafunzi wake lugha ya Kiswahili kama lugha ya kigeni ili wakazi wa eneo hilo waweze kuitumia katika mawasiliano pale itakapohitajika.

Mama Kikwete ambaye pia  ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA)  ametoa  ombi hilo leo wakati akiongea na uongozi wa chuo hicho alipowatembelea yeye na ujumbe wake.

Alisema  hivi sasa lugha ya kiswahili  inakuwa kwa kasi na kutumika katika maeneo mengi hasa nchi za Afrika Mashariki na Kati hivyo basi nao wawafundishe wanafunzi wao ili wakienda katika nchi hizo iwe ni rahisi kwao kuwasiliana.

“Kiswahili ni lugha ya taifa letu la Tanzania ambayo tunaitumia katika mawasiliano, mkiwafundisha wanafunzi wenu lugha hii nao watawafundisha wenzao hivyo itakuwa ni rahisi kwao kuwasiliana hasa wakisafiri na kukutana na watu wanaotumia lugha hii”, alisema Mama Kikwete.

Kwa upande wake makamu rais wa chuo hicho Dk. Edward Christensen alimshukuru mama Kikwete kwa kutembelea chuo hicho na kusema kuwa ombi lake la chuo hicho kufundisha lugha ya Kiswahili wamelisikia na wataangalia jinsi gani watalifanyia kazi.

Aidha Dk. Christensen aliwaomba wakufunzi na watu wenye utaalamu wa mambo mbalimbali kutoka nchini Tanzania kwenda katika chuo hicho kufanya midahalo na wafanyakazi na wanafunzi wa chuo hicho.

Chuo hicho kinawanafunzi wapatao 6300 kutoka ndani na n je ya nchi 29 na kinatoa kozi mbalimbali zikiwemo za Sayansi na sanaa katika  ngazi ya cheti, shahada na shahada ya uzamili.
                                  *******************************************

CHUO KIKUU CHA MONMOUTH KUSHIRIKIANA NA TANZANIA KUSOMESHA WAUGUZI

Na Anna Nkinda , New York

Chuo Kikuu cha Monmouth cha mjini New Jersey nchini Marekani kimeahidi  kushirikiana na Serikali ya Tanzania kupitia wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii  kutoa mafunzo kwa wauguzi  ili kuweza upunguza tatizo la vifo vya kina mama wajawazito na watoto nchini.

Hayo yamesemwa jana na Rais wa  chuo hicho Dk. Paul Brown wakati akiongea na ujumbe maalum kutoka Tanzania ulioongozwa na Mke wa Rais Mhe. Mama Salma Kikwete uliotembelea chuo hicho.

Dk. Brown alisema wakufunzi  kutoka chuo hicho watatoa mafunzo kwa makundi ya watu wachache wachache kwa njia ya kubadilishana uzoefu wa kazi  (Exchange Program) ambao wataenda kuwafundisha wenzao hii itakuwa ni pamoja na wataalamu  kutoka chuo hicho kuja nchini na kuwafundisha manesi au manesi kwenda katika chuo hicho kujifunza.

“Tunaomba mtupatie mtaala wa  masomo  mnaotumia kuwafundishia wauguzi katika vyuo vyenu  ili tuweze kuupitia  kama kuna mahali pa kuboresha tutaboresha,  tutaboresha na  kuutumia wakati wa kufundishia”, alisema Dk. Brown.

Mafunzo mengine yatakafundishwa  ni kwa njia ya CD na mtandao (Skype) jambo ambalo litawafanya wakufunzi pamoja na wanafunzi kuweza kubadilishana utamaduni wa nchi zote mbili pia chuo hicho kitatoa ufadhilii wa masomo kwa watu watakaosomea fani ya uuguzi.

Chuo hicho pia kimemkabidhi Mhe. Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) vitabu 4000  ambavyo vitatumika kufundishia katika vyuo vya elimu ya juu hapa nchini kwa ajili ya masomo mbalimbali yakiwemo ya sayansi katika fani za uuguzi na fizikia .

Kwa upande wake Mama Kikwete aliushukuru uongozi wa chuo hicho kwa vitabu walivyowapatia na kuamua kushirikiana na Serikali ya Tanzania kupunguza tatizo la vifo vya kina mama wajawazito na watoto pia aliwaomba washirikiane katika ufanyaji wa tafiti mbalimbali .

“Vitabu mlivyotupatia vitapelekwa katika vyuo vilivyokusudiwa, naamini ushirikiano huu tuliouanzisha utatusaidia kujiendeleza katika mambo mbalimbali na kufikia malengo tuliyojiwekea”, alisema Mama Kikwete.

Naye waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk. Hussein Mwinyi alisema Serikali imejitahidi kuboresha huduma ya afya kwa wananchi wake na kuhakikisha kuwa vifo vya kina mama wajawazito na watoto wachanga vinavyotokea wakati wa kujifungua vinapungua na hadi sasa vifo hivyo vimepungua  kutoka 578 kwa kila vizazi hai 100000 hadi kufikia 454.

“Vifo vingi vya kina mama wajawazito na watoto vinavyotoea wakati wa kujifungua vinatokana na upungufu wa wataalamu wa afya tulionao wakiwemo wauguzi hivyo basi tunaomba tushirikiane katika hili ili muweze kutusaidia kutoa elimu ya ukunga na uuguzi kwa watu watakaohitaji kusoma fani hii”, alisema Dk. Mwinyi.

Alisema kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa afya Tanzania imeweza kupunguza maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU)  kutoka asilimia 5.7 kwa mwaka 2004 hadi asilimia 5.1 kwa mwaka 2011.

Chuo cha Monmouth baada ya kusikia kazi zinazofanywa na Taasisi ya WAMA moja wapo ikiwa ni kuboresha afya ya mama wajawazito na watoto waliamua kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika eneo la afya.

Mama Kikwete ameambatana na mmewe Mhe. Rais Dk. Jakaya Mrisho Kikwete nchini humo kwa ajili ya kuhudhuria mkutano wa 68 wa   nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa (UN).

No comments: