Tangazo

May 23, 2014

ATC kung'ara angani

Mwenyekiti na Rais wa Kampuni za Al Hayat Development and Investment LLC ya Oman, Sheikh Salim Bin Abdullah Al Harthy (kushoto) akiwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa ATC, Kapteni Milton Lazaro, katika mkutano na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam.

NA MWANDISHI  WETU
SHIRIKA la Ndege Tanzania (ATC) lipo karibu kuanza kung’ara hewani baada ya mwekezaji kutoka Oman kuwa tayari kuwekeza kwenye shirika hilo na sasa anasubiri serikali kukamilisha taratibu zake.

Miongoni mwa taratibu zinazosubiriwa ni kwa serikali kulipa madeni makubwa ambayo ATC ilikuwa inadaiwa ili kuweka mizania sawa ya vitabu vya hesabu za fedha.

Mwenyekiti na Rais wa Kampuni za Al Hayat Development and Investment LLC ya Oman, Sheikh Salim Bin Abdullah Al Harthy, alisema wana dhamira ya dhati ya kuwekeza hapa nchini na hasa katika ATC.

“Tunatarajia kuwekeza kwenye maeneo tofauti katika sekta za mafuta na uendelezaji wa maeneo ya fukwe, lakini lengo letu kuu ni kuwekeza ATC,” alisema Sheikh Salim na kuwa awamu ya kwanza watatumia sh, bilioni 160.

“Mpango wetu ni kujenga kituo cha mafunzo ya masuala ya ndege, ofisi nzuri kwa ajili ya ATC, kununua ndege na kufanya shughuli nyingine za maendeleo. Tunatarajia kufanya haya katika kipindi kifupi kijacho," alisema.

Alifafanua kuwa kuna wakati Kampuni ya Al Hayat ilikaa kimya kuhusu uwekezaji huo na kuwa ilifanya hivyo ili kutoa nafasi kwa serikali kukamilisha taratibu zake ikiwemo kupitia makubaliano yaliyofikiwa kati ya kampuni hiyo na ATC.

Alisema watendaji wa kampuni ya Al Hayat wamekuwa wakitembelea Tanzania mara kwa mara ili kufuatilia suala zima katika uwekezaji kwenye ATC.

Sheikh Salim alisema ni kutokana na hali hiyo ndiyo maana hata ule mpango wa kununua ndege aina ya Bombadier, Air Bus na Embraer  ulisimama kidogo kwa kuwa mkataba rasmi wa uwekezaji bado haujafikiwa na kutiwa saini.

Alisema safari hii wamekuja tena kuitikia wito wa ATC ili kuendeleza makubaliano yaliyofikiwa na kuwa taratibu zikikamilika watatia saini mkataba na kuanza uwekezaji.

Sheikh Salim alisema suala hili limechukua muda mrefu kutokana na taratibu husika zinazohusu pande zote, lakini anasisitiza azma ya kuwekeza iko pale pale kwa kuwa linahusisha mambo mbalimbali ikiwemo ya kisheria.

Hata hivyo, anasema kuna uwezekano mkubwa ndani ya miezi sita tangu sasa kila kitu kitakuwa kimekamilika na ATC itarudi kung’ara angani kwa kuwa  serikali inatoa ushirikiano mkubwa na wa kutosha.
Kuhusu utoaji wa huduma, Sheikh Salim anasema lengo ni kuhakikisha inafika katika mikoa mingi kadri iwezekanavyo na nchi jirani,  na kufanya safari za mbali katika nchi kama Uingereza na India.

Baada ya kukaribishwa na Sultani Qaboos kufanya ziara Oman, Rais Jakaya Kikwete alikutana na wafanyabiashara wan chi hiyo na kuwakaribisha kuja kuwekeza kwenye maeneo mbalimbali.

Hivyo uwekezaji wa Al Hayat umetokana na jitihaza zilizofanywa na Rais Kikwete katika ziara yake nchini humo.

Kwa sasa ATC inafanya safari zake katika mikoa ya Mtwara, Mwanza,  Tabora, Kigoma, Dar es Salaam, Mbeya na katika nchi za Burundi na Comoro. Hivi karibuni itaanzisha safari za Zanzibar na Kilimanjaro.

No comments: